TADB, Wizara ya Mifugo na Uvuvi Wazindua Vituo 23 vya Kukusanya Maziwa (MCCs)

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi imezindua rasmi Vituo 23 vya Kukusanyia Maziwa (MCCs) vilivyojengwa na kuboreshwa kupitia Mradi Shirikishi wa Wasindikaji na Wazalishaji wa Maziwa Tanzania (TI3P), hatua inayolenga kuimarisha mnyororo wa thamani wa maziwa na kuongeza tija kwa wafugaji nchini.

Uzinduzi huo wa kitaifa umefanyika katika Kituo cha Kukusanyia Maziwa cha Nshamba, Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera, ukiongozwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Bashiru Ally Kakurwa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri amesema mradi wa TI3P umeleta mageuzi chanya katika sekta ya maziwa kwa kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa maziwa na kupanua fursa za masoko kwa wafugaji wadogo, wa kati na wakubwa. Alieleza kuwa vituo vya kukusanyia maziwa ni miundombinu ya kimkakati inayowezesha uhifadhi wa maziwa katika viwango vinavyokubalika, kupunguza upotevu wa mazao na kuongeza thamani kabla ya usindikaji.

Mradi wa TI3P unafadhiliwa na Gates Foundation na kutekelezwa na TADB kwa kushirikiana na Heifer International Tanzania pamoja na Land O’Lakes Venture37, ukiwa na lengo la kuwaunganisha wazalishaji na wasindikaji katika mfumo jumuishi na endelevu.


Mafanikio ya Utekelezaji

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Frank Nyabundege, amesema tangu kuanza kwake, TI3P umewezesha utolewaji wa zaidi ya Shilingi bilioni 41 kama mikopo kwa wadau wa sekta ya maziwa.

Amesema mitamba 3,254 yenye thamani ya Shilingi bilioni 10.8 imenunuliwa ili kuongeza uzalishaji, huku viwanda 15 vya usindikaji vikifadhiliwa kwa zaidi ya Shilingi bilioni 22, hatua iliyoongeza uwezo wa kitaifa wa uchakataji wa maziwa.

Kwa mujibu wa Nyabundege, wafugaji 92,831 wamefikiwa moja kwa moja kupitia huduma za kifedha, mafunzo na huduma za ugani, huku ruzuku fungamanifu (Matching Grants) ya Shilingi bilioni 1.448 ikitolewa kwa wazalishaji na wasindikaji.

Aidha, vyama 45 vya wazalishaji wa maziwa (FPOs) vimeanzishwa na kuimarishwa, vikikusanya wastani wa lita 19,047 kwa siku. Vituo 23 vilivyojengwa na kuboreshwa katika Kanda ya Ziwa, Nyanda za Juu Kusini na Zanzibar vina uwezo wa kukusanya lita 45,500 kwa siku, vikihudumia wafugaji 4,016 katika mikoa nane na wilaya 18.

Ziara ya Miradi Mkoani Kagera

Katika ziara yake mkoani Kagera, Waziri alitembelea Chama cha Ushirika cha Maruku, Bukoba Mjini, na kushuhudia utekelezaji wa mpango wa “Kopa Ng’ombe, Lipa Maziwa” unaolenga kuongeza kipato kwa vijana na wanawake.

Kupitia chama hicho chenye wanachama 118, wanachama 24 wamenufaika na mitamba 24 yenye mimba pamoja na ruzuku ya Shilingi milioni 18 kupunguza mzigo wa marejesho ya mikopo. Pia kituo hicho kimekarabatiwa kwa zaidi ya Shilingi milioni 10.4 na kupatiwa tanki la kuhifadhia maziwa la lita 2,000. Wafugaji hao wameunganishwa na soko la uhakika la Kahama Fresh Limited.

Katika Kituo cha Nshamba chenye wanachama 541, TADB imewezesha uanzishwaji wa MCC yenye uwezo wa kukusanya lita 2,000 kwa siku pamoja na jenereta ya dharura. Aidha, katika Ushirika wa UWAWAMA wilayani Karagwe, wanachama 76 wamenufaika na mitamba 110 yenye mimba na ruzuku ya Shilingi milioni 85 kupunguza marejesho ya mikopo.

Mwelekeo wa Serikali

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa uwekezaji katika sekta ya mifugo kwa lengo la kuongeza thamani ya mazao ya mifugo, kukuza ajira na kuinua kipato cha wananchi vijijini.

TADB imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na Serikali, washirika wa maendeleo na sekta binafsi ili kuhakikisha mafanikio ya mradi wa TI3P yanaimarisha uchumi wa viwanda unaotegemea uzalishaji bora na ushiriki mpana wa wafugaji katika mnyororo wa thamani wa maziwa.