……………..
Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni imefuatilia matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo miwili katika sekta ya miundombinu yenye thamani ya Shilingi Bill 5.
Akizungumza jijini Dar es salaam wakati akiwasilisha mafanikio ya utendaji kazi kwa kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2025,Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni Christian Nyakizee amesema kuwa katika ufuatiliaji huo wa ujenzi wa barabara ya Gemma na Nyaishonzi Kata ya Bunju imebainika kuwepo na ongezeko la muda wa utekelezaji wa miradi hiyo kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya hewa,kuchelewa kwa malipo na ombi la msamaha wa kodi.
Aidha Nyakizee amesema malalamiko 72 yalipokelewa katika kipindi hicho ambapo 25 yalihusu vitendo vya rushwa na 47 hayakuhusu vitendo vya rushwa.
“Malalamiko 25 yaliyohusu rushwa uchunguzi wake unaendelea na upo katika hatua mbalimbali huku malalamiko 45 ambayo hayahusu rushwa walalamikaji walishauriwa’amesema Nyakizee
Ameeleza kuwa katika kipindi hicho pia kesi 19 zinaendelea mahakamani ambapo kati ya kesi hizo,mpya 1 ilifunguliwa na kesi 4 zilitolewa maamuzi na Jamhuri ilishinda zote.
Kuhusu mikakati ya mwezi Januari hadi Machi mwaka huu,Mkuu huyo wa TAKUKURU Mkoa Kinondoni amesema kuwa wataendelea kufuatilia matumizi ya fedha za serikali katika miradi mbalimbali lakini pia kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kuzuia rushwa.
Hata hivyo amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na TAKUKURU kutoa taarifa pindi wanapobaini uwepo wa vitendo vya rushwa kwenye maeneo yao ili ziweze kufanyiwa kazi kwa haraka kwa watakaobainika.