Tanzania, Ghana zakubaliana haya | Mwananchi

Dar es Salaam. Tanzania na Ghana zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kimkakati hususan katika mageuzi ya kiuchumi, ajira kwa vijana na maendeleo ya uchumi wa kidijitali.

Makubaliano hayo, yamefikiwa leo Jumatatu, Machi 1, 2026 katika mazungumzo baina ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Rais wa Ghana, John Mahama yaliyofanyika Ikulu Arusha.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Tanzania imeeleza viongozi hao wamejadili umuhimu wa kuongeza thamani ya rasilimali za ndani badala ya kuendelea kuuza malighafi.

Rais Mahama amesema hatua zinazochukuliwa na Ghana katika kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini na kakao, kwa lengo la kuongeza mapato ya ndani na kukuza uchakataji wa ndani.

Kwa upande wake, Rais Samia amesema Tanzania inaendelea kuharakisha mkakati wa uchumi wa viwanda, ikiwemo kuongeza thamani ya mazao ya kimkakati kama pamba na kuimarisha uchakataji wa madini, na kuongeza kuwa Tanzania ina nafasi muhimu ya kujifunza kutoka Ghana katika usimamizi wa rasilimali na sera za uchumi wa ndani.

Kuhusu suala la ajira kwa vijana, marais hao wamekubaliana kuongeza ushirikiano katika maendeleo ya ujuzi, ubunifu na ujasiriamali, na kusisitiza umuhimu wa kuweka mazingira bora ya uwekezaji yatakayozalisha ajira endelevu kwa vijana wa pande zote mbili.

Katika eneo la uchumi, Rais Samia amesisitiza dhamira ya Tanzania ya kuimarisha mifumo ya fedha za kidijitali na usalama wa mitandao, kama sehemu ya mkakati wa kujenga uchumi shindani na jumuishi.

Amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya Tehama na kukuza ubunifu wa vijana, huku akieleza kuwa uzoefu wa Ghana katika sekta ya teknolojia ya fedha na ulinzi wa miundombinu ya kimtandao ni eneo muhimu la kujifunza na kushirikiana, ili kuongeza ujumuishwaji wa kifedha na ufanisi wa huduma za kifedha nchini.

Halikadhalika, viongozi hao wamepongeza hatua ya kuimarisha usafiri wa anga wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kati ya Tanzania na Ghana, wakisema hatua hiyo itarahisisha biashara, utalii na mwingiliano wa watu kati ya nchi hizo mbili, na kuongeza kuwa safari hizo za moja kwa moja zitachochea biashara sio tu ya Tanzania na Ghana, bali pia ndani ya Bara la Afrika.

Rais wa Ghana yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja. Leo Machi 2, 2026 anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mwaka wa Mahakama, na maadhimisho ya miaka 20 ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, yenye makao yake makuu jijini Arusha.