Arusha. Tanzania imeanza mchakato wa kujadili jinsi ya kurudi katika itifaki muhimu inayoruhusu watu binafsi kushtaki Serikali moja kwa moja mbele ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR).
Kwa mujibu wa Ibara ya 34(6) ya Itifaki, nchi wanachama za nchi za umoja wa Afrika, nchi wanachama zinatakiwa kutoa tamko la hiari la kuridhia itifaki au kuruhusu mashirika au watu binafsi kufungua kesi moja kwa moja katika Mahakama hiyo.
Kwa sasa, ni nchi nane tu ambazo zimeruhusu mashauri ya moja kwa moja kutoka kwa watu binafsi au asasi za kiraia, ambazo ni Burkina Faso, Gambia, Ghana, Guinea-Bissau, Malawi, Mali, Niger na Tunisia.
Tanzania iliridhia Itifaki ya Mahakama mwaka 2006 na mwaka 2010 ikaweka tamko la hiari chini ya Ibara ya 34(6), kuruhusu watu binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali kufungua kesi moja kwa moja dhidi yake katika Mahakama hiyo.
Hata hivyo, mwaka 2019, Serikali iliondoa tamko hilo, ikieleza wasiwasi wa kisheria na taratibu, ikiwemo hoja kwamba baadhi ya waliotaka haki walipita njia nyingine za ndani kabla ya kufikia Mahakama.
Akizungumzia swala hilo jana jijini Arusha katika ufunguzi rasmi shughuli za mwaka wa kimahakama 2026 wa AfCHPR, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainab Katimba amesema Tanzania imeanza majadiliano ya ndani kuhusu namna ya kurejea katika tamko hilo.
Amesema Tanzania kama nchi mwenyeji wa Mahakama hiyo na Taifa linalojali ulinzi wa haki za binadamu, itaendelea kuimarisha mifumo yake ya kisheria ya ndani sambamba na kuunga mkono utekelezaji wa majukumu ya Mahakama.
“Kama mwenyeji wa Mahakama hii, Tanzania itaendelea kuunga mkono mamlaka ya mahakama hii, na dhamira yetu inaonekana wazi kupitia juhudi tunazofanya katika kutekeleza maamuzi yanayotolewa hapa.”
“Ingawa Tanzania ilijiondoa katika Ibara ya 34(6), taarifa njema ni kwamba tumeanza kushughulikia changamoto zilizopelekea uamuzi huo, na tuko katika hatua nzuri ya majadiliano ya namna ya kurejea katika utekelezaji wake,”amesema Katimba.
Sherehe hiyo pia iliadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Mahakama hiyo yenye makao yake makuu jijini Arusha.
Wakili wa Serikali, Ally Possy amesema, “Ofisi yangu ya Wakili Mkuu wa Serikali huwa tunaendesha mashauri yanayoikabili Tanzania katika Mahakama hii, lakini pia kwa umuhimu wetu kama mwenyeji na mdau, tumekuwa tukishiriki katika shughuli mbalimbali kama kuleta mashauri, kutekeleza hukumu na kushirikiana katika mafunzo.
Amesema kwa mwaka huu wanatarajia kuwasilisha mashauri kadhaa, huku pia wakipanga kufahamisha Mahakama kuhusu hatua ambazo Tanzania imechukua katika kuboresha mifumo yake ya kisheria, ikiwa ni pamoja na huduma za msaada wa kisheria na sheria za uendeshaji wa mashauri.”
“Tunatarajia kuendesha mashauri kadhaa hapa mahakamani kwa mwaka huu, lakini pia kuna mambo tunadhani tunahitaji kuifahamisha Mahakama kuhusu nafasi yetu na hatua ambazo Tanzania tumepiga katika kuboresha sheria zetu, ambapo maamuzi yake yakitoka ndani tunategemea kama ipo ndani ya utawala wa kisheria, na yale ambayo hayako tunaijulisha,” amesema.
Kuhusu kipengele cha kuruhusu watu binafsi kuleta mashauri moja kwa moja, Wakili Possy amesema Tanzania ipo katika majadiliano ya kina kama taasisi, ili kuhakikisha maslahi mapana ya taifa yanazingatiwa.
“Kuhusu kipengele cha watu binafsi kuleta mashauri, ni hatua tunayoangalia na tuko kwenye majadiliano kama taasisi, na tunaainisha maeneo ya masilahi ya Tanzania kwa ujumla,” amesema
Katika hotuba yake mgeni rasmi, Rais wa Ghana, John Mahama amesema licha ya Afrika kubarikiwa kwa rasilimali nyingi za asili, maendeleo endelevu yanategemea kuthamini na kulinda haki za watu wake.
“Natumia fursa hii kuziomba nchi ambazo bado hazijaridhia au kuweka tamko hilo zisiogope kufanya hivyo, Kuheshimu haki za binadamu hakutaleta udhaifu kwa Taifa iwapo kweli linawathamini watu wake kama rasilimali muhimu kwa maendeleo ya Afrika.”
Aidha, ameitaka Mahakama hiyo kuimarisha mifumo yake ya kisheria na utekelezaji wa maamuzi yake ili kuongeza uaminifu na kuwa kimbilio la Waafrika wanaotafuta haki.
Awali, Rais wa Mahakama hiyo, Blaise Tchikaya, amesema taasisi hiyo inaendelea na maboresho ya kuimarisha utekelezaji wa hukumu zake na kurahisisha taratibu za fidia, kufuatia wasiwasi kuhusu kupungua kwa hadhi yake.
Tangu kuanzishwa kwake, alisema Mahakama imesajili, kusikiliza na kutoa maamuzi katika mashauri zaidi ya 390 mafanikio yaliyowezekana kwa ushirikiano wa nchi wanachama na msaada wa Serikali ya Tanzania kama mwenyeji.
Hata hivyo, ametaja changamoto kuu kuwa ni uidhinishaji mdogo wa Ibara ya 34(6) na uelewa hafifu kuhusu mamlaka ya Mahakama na taratibu za rufaa miongoni mwa nchi za Afrika.
Akizungumzia dhamira mpya ya Tanzania, John Deya, Mkurugenzi Mtendaji wa Pan African Lawyers Union (PALU), amesema tangazo hilo ni nzuri lakini akasisitiza umuhimu wa utekelezaji wa vitendo.
“Tamko la Tanzania kuanza mchakato huu limeleta matumaini makubwa, Sasa kinachohitajika ni utekelezaji wa dhahiri ili kuimarisha uaminifu, kwani suala hili limekuwa likizungumzwa kwa muda mrefu,” amesema.
Wakati huo huo, takwimu zinaonyesha kupungua kwa kasi kwa idadi ya mashauri yanayowasilishwa mahakamani, jambo linaloibua maswali kuhusu ufanisi wake kama chombo kikuu cha haki za binadamu barani Afrika.
Mwaka 2025, mashauri mapya nane pekee ndiyo yalisajiliwa idadi iliyopungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na mashauri 66 yaliyowasilishwa mwaka 2019.
Tanzania, Ghana zakubaliana haya
Kabla ya Rais Mahama kufungua shughuli hiyo, alipokewa na mwenyeji wake, Samia Suluhu Hassan, katika Ikulu ndogo ya Arusha ambako walifanya mazungumzo na kukubaliana kuimarisha ushirikiano wa kimkakati, hususan katika mageuzi ya kiuchumi, ajira kwa vijana na uchumi wa kidijitali.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ya Tanzania, viongozi hao walijadili umuhimu wa kuongeza thamani ya rasilimali za ndani badala ya kuuza malighafi.
John Mahama amesema Ghana inaendelea kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini na kakao ili kuongeza mapato ya ndani na kukuza uchakataji wa ndani.
Kwa upande wake, Rais Samia amesema Tanzania inaharakisha mkakati wa uchumi wa viwanda, ikiwemo kuongeza thamani ya mazao ya kimkakati kama pamba na kuimarisha uchakataji wa madini, akibainisha kuwa kuna mengi ya kujifunza kutoka Ghana katika usimamizi wa rasilimali na sera za uchumi wa ndani.
Kuhusu ajira kwa vijana, marais hao walikubaliana kuongeza ushirikiano katika maendeleo ya ujuzi, ubunifu na ujasiriamali, pamoja na kuweka mazingira bora ya uwekezaji yatakayozalisha ajira endelevu.
Katika eneo la uchumi wa kidijitali, Rais Samia amesisitiza kuimarishwa kwa mifumo ya fedha za kidijitali na usalama wa mitandao, akieleza kuwa uzoefu wa Ghana katika teknolojia ya fedha na ulinzi wa miundombinu ya kimtandao ni muhimu katika kuongeza ujumuishwaji wa kifedha na ufanisi wa huduma.
Viongozi hao pia walipongeza kuimarika kwa safari za anga za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL)kati ya Tanzania na Ghana, wakisema zitachochea biashara, utalii na mwingiliano wa watu, si kwa nchi hizo tu bali pia ndani ya Bara la Afrika.