Tutuba afunguka kuhusu uuzaji wa dhahabu, thamani ya Shilingi

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kuna uwezekano mkubwa wa Serikali kupata gawio kubwa kutoka katika taasisi hiyo kutokana na mauzo ya dhahabu inayohifadhiwa, huku ikibainisha imevuka malengo ya kununua kabla ya muda uliopangwa.

BoT imeeleza hayo ikiwa ni siku chache tu tangu kuibuka kwa mjadala mkali kufuatia kauli ya Serikali kuwa imekuwa ikiuza sehemu ya akiba yake ya dhahabu. Wapo waliokosoa hatua hiyo wakidai dhahabu haipaswi kuuzwa, huku wengine wakinong’ona kuwa huenda ni ishara ya Serikali kukabiliwa na changamoto ya ukwasi.

Kufuatia mjadala huo, Mwananchi lilifanya mahojiano maalumu na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, ambaye amefafanua kwa kina sababu za hatua hiyo, kwa misingi ya kisheria na kiuchumi.

“Hili suala la dhahabu naona linawapa watu mawazo tofauti lakini dhahabu inayonunuliwa na benki kuu ni dhahabu fedha (monetary gold) na kuitunza ni jukumu moja wapo la benki huu,” amesema Tutuba katika mahojiano hayo yaliyohusisha masuala mbalimbali ya sekta ya fedha.

Amesema kifungu cha tano cha sheria ya benki kuu kimeipatia jukumu la kutunza akiba ya fedha za kigeni ambayo inaweza kutunzwa kwa sarafu tofauti na kifungu cha 51 cha sheria hiyo kimetaja kiwango kinachopaswa kuhifadhiwa, na kifungu kidogo kinachofuata kinaeleza namna ya utunzaji.

Tutuba amesema sheria hiyo imeipa mamlaka BoT kutunza akiba katika mfumo wa dhahabu fedha na nyingine ni sarafu, noti na hati fungani za nchi mbalimbali au kutumia utaratibu wa karatasi za mikataba maalumu (derivatives).

“Tulipoanza kununua mpango huu tulichukua dhahabu kama sehemu ya akiba zetu na idara yetu ya masoko ya fedha inafanya kazi saa 24 kwa sababu uwekezaji unaweza kufanyika asubuhi kwenye sarafu moja usiku tukauza,” amesema Tutuba.

Amesema benki kuu ya Tanzania inawekeza mahali popote duniani kwani kifungu cha 51 cha sheria kinawaelekeza kuwa kwa kadri watakavyoona inafaa wanaweza kuwekeza akiba popote, hivyo suala la kuuza dhahabu halitakiwa kuwasumbua watu sana, ni mpango wa kawaida.

“Huu mradi umeanza  Oktoba Mosi, 2024 maana nimeona wengine wanasema dhahabu ilikuwepo tangu enzi za Nyerere imetunzwa sasa inataka kuuzwa, sio kweli na wanaosema hivyo hawaelewi,” amesema Tutuba.

Amesema wakati wanaanza ununuzi walitarajia kukusanya tani 20 ndani ya miaka mitatu lakini hadi kufikia  Februari 25, 2026 ambayo ni sawa na mwaka mmoja na nusu tangu kuanza mradi huo walikuwa wamefikia tani 19.6 ndiyo maana wakaanza kuuza.

“Baada kufikia kiwango hicho, tukajiuliza je, utaacha kununua, tukasema tusiache kununua kwa kuwa wakati tunaanza programu tulitaka pia kurasimisha soko la ndani la dhahabu kwa sababu tuliona wale wachimbaji na wauzaji (dealers), wakati mwingine wanakosa soko la kuuzia dhahabu zao,” amesema Tutuba.

Gavana wa benki Kuu ya Tanzania (BoT) Emmanuel Tutuba, akiwa katika mahojiano maalumu yalifanyika katika ofisi ndogo za BoT jijini Dar es salaam. Picha na Michael Matemanga.



Amesema katika mpango huo kuna lengo lingine la uwekezaji kwanza inananuliwa bei ikipanda wanauza hivyo hainunuliwi tu ili itunzwe milele, imenunuliwa kama sehemu ya biashara na kuuunga mkono wafanyabiashara.

Tutuba amesema kulingana na uchambuzi wa vihatarishi huwezi kutunza mali zako zote katika sarafu moja na dhahabu inabadilika sana bei, hivyo kuna ukomo umewekwa na sasa iliyopo inafika kama theluthi moja kwa maana ya thamani kutokana na ongezeko la bei.

“Kuwa na zaidi ya theluthi moja ni hatari hivyo baada ya uchambuzi tukaamua kuwa tutapunguza ili kiwango kitakachouzwa kiwekezwe kwenye maeneo mengine, ili kupata faida zaidi na kutoathiri mfumo wa manunuzi ambao tulikuwa tumeuweka,” amesema.

Amesema ni muhimu wananchi wakasoma sheria za BoT hususani kifungu cha tano kinachoelezea majukumu yake kisha namba 51 juu ya utunzaji na namba 52 kinachoeleza hiyo akiba inauzwa au kutumika kwa utaratibu gani.

“Hatua hii (ya kuuza dhahabu sasa) itaifanya hata Serikali kupata gawio kubwa zaidi mwaka huu kwa sababu kuna dhahabu tuliinunua kwa bei ndogo, tukiiuza sasa kwa bei kubwa tunapata faida, sisi kila mwaka huwa tunatoa gawio serikalini,” amesema

Mbali na ununuzi wa dhahabu Tutuba amesema Benki Kuu ya Tanzania imewekeza akiba za nchi katika maeneo mengi ndani na nje ya nchi ikiwemo hati fungani za Serikali ya Marekani, China na hata kwenye hisa akitolea mfano wa Afrexim Bank ambayo BoT ina hisa zaidi ya asilimia moja ya hisa zote.

“Tumewekeza kwenye maneno mbalimbali ndiyo maana anasema mtu ambaye anaweza kujadili iwapo BoT inatakiwa kuuza au kutokuuza anapaswa ajiridhishe na afahamu uwekezaji kwenye masoko ya fedha unafanyika vipi.”

 “Ukiwa makini muda ambao bei inapanda ndiyo wakati wa kuuza na pesa unayoipata utanitumia kununua bei ikishuka kwa kuwa wakati huo pesa yako unakuwa tayari umeiwekeza kwenye maeneo ambayo unapata faida zaidi,” amesema.

Katika mahojiano hayo Tutuba amesema Shilingi ya Tanzania inaendelea kufanya vizuri licha ya kuwa kuna misimu ambayo thamani inatetereka na kuna muda inaendelea kuimarika akitolea mfano kuwa kuna wakati inafika hadi 2,800 lakini baadaye inashuka tena hadi 2,400.

“Ukilinganisha sasa na tulikotoka, msimu kama huu mwaka juzi ilikuwa Sh2,800 lakini miezi hii tuko 2,500 hivyo unaona Shilingi imeimarika lakini ukilinganisha na mwaka jana. Hii inatokana na uwepo wa vyanzo vya fedha hizo sokoni kwa kuuza bidhaa nje ya nchi ikiwemo bidhaa za kilimo na dhahabu.”

Amesema jambo zuri zaidi ni kuwa mwaka huu utalii umekuwa hauna msimu muda wote ni kama mapato yanalingana, huku akisisitiza kuwa mifumo ya usimamizi wa thamani ya sarafu Tanzania umeendelea kuwa mizuri ikilinganishwa na nchi nyingine.

“Mpaka sasa Shilingi yetu imeendelea kuwa imara, kupatikana na hata ukwasi wa fedha za kigeni upo wa kutosha, lakini mtu anapoamua kutumia fedha za kigeni ndani ya nchi ni kimsingi ni kosa na Sheria ya BoT kifungu cha 26 kinasema Shilingi ya Tanzania ndiyo itakuwa fedha pekee halali kwa malipo ya ndani ya nchi, ukitumia fedha nyingine unafanya kosa”

Amesema kosa hilo lina adhabu ya mpaka Dola 3000 (Sh7.6 milioni) ni kama ndogo lakini lengo si kuwaadhibu watu bali kuwapa ufahamu, mtu akielewe kwa nini atumie Shilingi ya Tanzania kwanza kwa kuwa ni tunu ya nchi lakini pia ndiyo inayotunza thamani ya bidhaa na huduma Tanzania.

Kuhusu Tanzania kuhuisha thamani ya sarafu ya Tanzania, Tutuba amesema kwa sasa hakuna mpango wa kufanya hivyo kwa kuwa thamani iliyonayo sasa ni imara na haina athari hasi kwa uchumi wa nchi.