Iringa. Serikali ya Mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, imezindua rasmi mbegu za miche ya viazi lishe, hatua inayolenga kuimarisha usalama wa chakula, kuboresha lishe na kuongeza kipato cha wakulima wa mkoa huo.
Uzinduzi huo umefanyika leo Jumatatu Machi 2, 2026 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa na kuongozwa na Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji, Dk Golyama Bahati.
Amesema mpango huo ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali kukuza kilimo chenye tija na chenye kuzingatia mahitaji ya lishe ya jamii.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa viazi lishe vinajulikana kwa kuwa na kiwango kikubwa cha vitamini A, kirutubisho muhimu katika kuimarisha kinga ya mwili na afya ya macho.
Kwa mujibu wa tafiti za lishe, gramu 100 za viazi lishe zinaweza kutoa zaidi ya asilimia 100 ya mahitaji ya kila siku ya vitamini A kwa mtoto mdogo.
Pia, Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa upungufu wa vitamini A ni miongoni mwa sababu kuu za matatizo ya macho na kupungua kwa kinga ya mwili kwa watoto katika nchi zinazoendelea hli hiyo imekuwa changamoto katika baadhi ya maeneo ya Tanzania, hasa vijijini.
Kupitia mradi wa HarvestPlus, wakulima wa Iringa wamepatiwa mafunzo ya kitaalamu kuhusu uandaaji wa vitalu, uzalishaji wa miche bora na mbinu sahihi za upandaji kwa lengo la kuongeza mavuno na ubora wa mazao.
Dk Bahati amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wakulima kwa kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora, mafunzo na masoko ya uhakika ili kuongeza thamani ya mazao yao.
“Tunahitaji wakulima wachukue hatua hii kama fursa ya kubadilisha maisha yao na viazi lishe si tu zao la chakula, bali ni zao la kimkakati katika mapambano dhidi ya utapiamlo,” amesema.
Baadhi ya wakulima wakizungumza na Mwananchi Digital Leo Jumatatu Machi 2, 2026, wameelezea matumaini yao juu ya zao hilo huku wakiamini kujiinua kiuchumi na kukuza kiwango cha lishe.
Rehema Mwaobo, mkulima kutoka Manispaa ya Iringa amesema mafunzo waliyopata yamewapa uelewa mpana kuhusu umuhimu wa lishe na namna ya kuongeza uzalishaji.
“Awali tulikuwa tunalima viazi kawaida bila kujua tofauti ya lishe lakini sasa tumeona faida yake kiafya na kibiashara na tunatarajia kupata mavuno bora na soko litakalotupa kipato kizuri,” amesema Rehema.
Naye Elias Monge kutoka Wilaya ya Kilolo amesema changamoto kubwa kwa wakulima ni mitaji na masoko, lakini anaamini ushirikiano kati ya Serikali na wadau utasaidia kutatua vikwazo hivyo.
Nao wadau wa lishe wanasema kuimarika kwa uzalishaji na matumizi ya viazi lishe kutachangia kupunguza tatizo la utapiamlo, hasa kwa watoto na wanawake wajawazito, huku ikiimarisha uchumi wa kaya kupitia kilimo chenye tija.
Serikali ya Mkoa wa Iringa imeeleza itaendelea kufuatilia utekelezaji wa mradi huo na kuhakikisha wakulima wanapata rasilimali na msaada unaohitajika ili mapinduzi ya kilimo cha lishe yawe endelevu.