Wanadiplomasia, wadau wa maendeleo waipa Tanzania mbinu kukuza biashara

Dar es Salaam. Wadau wa maendeleo na wanadiplomasia wameishauri Tanzania kuchukua hatua za haraka kuboresha mazingira ya biashara ili kuvutia wawekezaji zaidi. Mapendekezo yao ni pamoja na kupunguza udhibiti wa taasisi nyingi, kuondoa urasimu, kuimarisha kituo cha huduma za pamoja na kuhakikisha utekelezaji wa mipango unafanyika kwa vitendo.

Wametoa maoni hayo katika mkutano wa wadau ulioandaliwa na Tume ya Mipango na Uwekezaji kupitia mapitio ya rasimu ya Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (Mkumbi II).

Maoni hayo yanakuja wakati Serikali imekiri kuwapo kwa changamoto 59 zinazoathiri ukuaji wa biashara na uwekezaji katika maeneo 11.

Akizungumza Machi 2, 2026, Waziri wa Ofisi ya Rais–Mipango na Uwekezaji, Kitila Mkumbo, amesema Serikali imependekeza hatua 246 za marekebisho ili kuboresha ufanisi wa kisheria, uratibu wa taasisi na utoaji wa huduma.

Amesema changamoto hizo zipo katika maeneo kama kuanzisha na kuendesha biashara, mitaji, mazingira ya kidijitali, nguvu kazi na stadi, masoko, miundombinu, utatuzi wa migogoro, ulinzi wa haki miliki, pamoja na uwajibikaji na ufuatiliaji.

Yusuf Seilsay kutoka Sierra Leone amependekeza kuimarishwa kwa kituo cha huduma za pamoja ili mwekezaji apate nyaraka zote muhimu sehemu moja, badala ya kuzunguka ofisi kama Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela)  na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Amesema mfumo huo unapaswa kurahisisha usajili wa miradi kwa muda mfupi, badala ya taratibu ndefu zinazochelewesha uwekezaji. Amesisitiza kuwa pamoja na rasilimali na miundombinu iliyopo, bila kupunguza urasimu maendeleo hayatapatikana.

Kutoka ubalozi wa Marekani, Jonathan Howard ametaka tathmini ya utekelezaji wa mapendekezo ya Mkumbi I, akieleza kuwa baadhi ya sera zilizotekelezwa kuelekea uchaguzi hazikuwa rafiki kwa wawekezaji wa kimataifa. Ametaja pia kusuasua kwa matokeo ya Tume ya Mageuzi ya Kodi iliyoanzishwa takribani miezi 18 iliyopita.

Kwa upande wake, Mwamina Ngwale kutoka Ubalozi wa Zambia amependekeza kuanzishwa kwa mfumo wa mtandaoni kushughulikia malalamiko ya bei na ushindani usio sawa, ili kurahisisha wafanyabiashara wa nje kupata haki. Pia amependekeza marekebisho ya ada za udhibiti ili ziendane na huduma inayotolewa, badala ya kutegemea ukubwa wa biashara.

Akijibu hoja hizo, Profesa Mkumbo amekiri kuwa urasimu na wingi wa mamlaka za udhibiti ni changamoto, akisema Serikali inapanga kupunguza idadi ya mamlaka hizo ili kuweka uwiano kati ya udhibiti na urahisi wa kufanya biashara.

Kuhusu kituo cha huduma za pamoja, amesema tayari kina taasisi takriban 14, lakini changamoto ni baadhi ya taasisi kutuma watumishi wasio na mamlaka ya mwisho ya kufanya maamuzi. Serikali imezitaka zipeleke maofisa wenye mamlaka kamili ili huduma zitolewe papo hapo, huku ikiahidi kuboresha zaidi utekelezaji wa mfumo huo.