Wataalamu wataja sababu za changamoto za afya ya akili kwa wanaume

Tanga. Wataalamu wa afya ya akili wameeleza sababu zinazowafanya wanaume kukumbwa na changamoto za afya ya akili, hali inayochangia baadhi yao kufikia hatua ya kujiua, wakiamini hiyo ndiyo njia pekee ya kupata unafuu.

Sababu hizo zimetolewa leo, Jumatatu, Machi 2, 2026, wakati wa warsha ya afya ya akili kwa wanaume iliyowakutanisha wadau mbalimbali mkoani Tanga, baada ya kubainika kuwa tatizo la afya ya akili ni kubwa katika mkoa huo.

Warsha hiyo imeandaliwa na taasisi ya Gateway Rehabilitation Centre, inayojihusisha na huduma za afya ya akili, matibabu kwa waraibu wa dawa za kulevya na uhamasishaji wa jamii kuhusu ustawi wa kisaikolojia.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), takriban mtu mmoja kati ya sita hupitia changamoto ya afya ya akili katika maisha yake, huku zaidi ya asilimia 70 ya vifo vinavyotokana na kujiua vikiwa ni wanaume.

Aidha, tafiti zinaonesha kuwa asilimia 60 ya wanaume wenye changamoto za afya ya akili hawatafuti msaada wa kitaalamu, jambo linaloongeza madhara kwa mtu binafsi, familia na jamii.

Kutokana na hali hiyo, wadau na wataalamu wa afya ya akili wameona umuhimu wa kuwepo kwa jitihada za makusudi za kuimarisha huduma za afya ya akili ili kuokoa maisha na kujenga jamii imara.

Wameomba Serikali kuendelea kuipa kipaumbele sekta hiyo na kuimarisha huduma zake hadi ngazi ya jamii.

Akizungumza katika warsha hiyo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Japhet Simeo, amesema mitazamo ya kijamii inayomtaka mwanaume kuwa jasiri na kutoonesha hisia inachangia kwa kiasi kikubwa tatizo hilo.

“Hii inamnyima mwanaume fursa ya kushirikisha mambo mazito yanayomsibu kwa mtu mwingine. Matokeo yake, anabaki na msongo mkubwa wa mawazo, unaopunguza ufanisi kazini, katika familia na hata ustawi wake wa kisaikolojia,” amesema Simeo.

Ameongeza kuwa mabadiliko ya kijamii na kiuchumi yameleta mkanganyiko kwa wanaume wengi, hasa katika suala la majukumu ya kifamilia.

“Leo mwanaume amefundishwa kuwa yeye ndiye mlezi mkuu wa familia, lakini anakutana na mazingira ambayo mke pia anafanya kazi. Maswali yanabaki je, kipato cha mke ni cha familia au ni cha kwake binafsi? Wengi wanabaki na maswali yasiyo na majibu na kuamua kunyamaza ili kulinda amani,” ameeleza.

Simeo ametaja pia presha za kisiasa, kijamii na kiuchumi kuwa mzigo mkubwa kwa wanaume, akibainisha kuwa wengi hujihusisha na kazi hatarishi kama ujenzi wa madaraja, kazi za migodini na kupanda kwenye minara ya umeme, hali inayowaweka katika mazingira magumu zaidi.

Daktari wa afya ya akili katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo, Wallace Karata, amesema hali ya kiuchumi ni kichocheo kikubwa cha matatizo ya afya ya akili kwa wanaume.

“Mwanaume ni mbeba majukumu katika familia. Anapokosa kipato au anapokutana na changamoto kazini, afya yake ya akili huathirika. Wengi hujiuliza watafanyaje nyumbani, na wengine hufikia hatua ya kukata tamaa,” amesema Dk Karata.

Amesisitiza umuhimu wa wanaume kuwa na ujasiri wa kushirikisha changamoto zao badala ya kubeba mizigo peke yao.

“Hatufundishi mwanaume atoroke familia au ajinyonge. Tunataka ajue afanye nini anapokutana na changamoto, atafute msaada na azungumze,” ameongeza.

Kwa upande wake, ofisa kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Shaban Miraji, amesema afya ya akili kwa muda mrefu imeonekana kama jambo la kigeni, hali iliyosababisha kupuuzwa kwake.

“Tunajali sana afya ya mwili, kila mmoja ameenda hospitali kupima malaria au magonjwa mengine. Lakini ni wangapi wamewahi kupima afya ya akili? Wengi hawajawahi,” amesema Miraji.

Ameeleza kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya afya ya akili na matumizi ya dawa za kulevya, akisema baadhi ya watu hutumia pombe au dawa za kulevya kama njia ya kukwepa msongo wa mawazo.

“Mtu anaweza kuwa na msongo wa mawazo kutokana na madeni au migogoro ya kifamilia, akaamua kunywa pombe au kutumia dawa kama tramadol bila ushauri wa daktari. Hapo changamoto ya afya ya akili inazidi,” amesema.

Miraji ameonya kuwa matumizi ya bangi, hasa aina ya skanka yenye kiwango kikubwa cha kemikali kama THC, yanaweza kuchochea au kuimarisha dalili za magonjwa ya akili, ikiwemo kuona au kusikia vitu visivyokuwepo.

Naye Meneja wa Programu wa Gateway Rehabilitation Centre, Amina Mbowe, amesema taasisi hiyo imebaini kuwa wanaume wengi hukumbwa na msongo wa mawazo, unyogovu, wasiwasi na matumizi mabaya ya dawa za kulevya, lakini ni kundi linalotafuta msaada kwa kiwango cha chini.

“Tumelenga kuongeza uelewa, kuvunja unyanyapaa na kuhamasisha wanaume kutafuta msaada mapema. Tunatoa elimu kuhusu msongo wa mawazo, unyogovu, wasiwasi na mbinu za kukabiliana nazo,” amesema Mbowe.

Ameongeza kuwa kupitia wataalamu wa afya ya akili, washiriki wanapatiwa elimu kuhusu utambuzi wa magonjwa ya akili, madhara ya matumizi ya dawa za kulevya na mikakati ya kuzuia vitendo vya kujiua.