Waziri Gwajima ahimiza jamii kubadili mitazamo, kuvunja vikwazo

Arusha. Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima, amesisitiza umuhimu wa jamii kubadili mitazamo na kuvunja vikwazo vinavyokwamisha usawa wa kijinsia na ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu katika jamii.

Amesema Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya kisheria, kisera na kitaasisi ili kuhakikisha hakuna mwananchi anayeachwa nyuma katika safari ya maendeleo.

Dk Gwajima amesema hayo leo Jumatatu, Machi 2, 2026, akizungumza katika jukwaa la nne la kimataifa la usawa wa kijinsia, ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu na ushirikishwaji wa kijamii.

Amesema ni muhimu jamii kubadili fikra potofu zilizojengeka na kuondoa vikwazo vinavyokwamisha makundi maalumu na kuweka mazingira yatakayofungua fursa sawa kwa wote.

Amesema jukwaa hilo, lililowakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo watunga sera, watafiti, wanaharakati, mashirika ya kiraia na washirika wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi, ni muhimu katika kujenga jamii jumuishi inayothamini usawa, haki na maendeleo endelevu.

“Ajenda ya Maendeleo ya Taifa ya Tanzania imejengwa kwa imani kwamba hakuna jamii inayoweza kupiga hatua endelevu iwapo sehemu ya watu wake itaendelea kutengwa. Mfumo wetu wa sera za muda mrefu, ikiwemo Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, utaendelea kuimarisha misingi ya kisheria na kisera inayolinda usawa na ujumuishwaji,” amesema.

Akizungumzia mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji, amesema Serikali imezindua Mpango wa Pili wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (NPAVAWC II) wa mwaka 2024/25–2028/29, unaolenga kupunguza vitendo vya ukatili, kuimarisha utekelezaji wa sheria na kuboresha huduma kwa waathirika.

Amesema Serikali imeendelea kupanua vituo vya huduma jumuishi kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia (One Stop Centres) katika mikoa mbalimbali, pamoja na kuzindua mkakati mpya wa miaka mitano wa kupambana na ukeketaji, hususan katika mikoa yenye viwango vya juu vya vitendo hivyo kama Arusha, Manyara, Mara na Singida.

Kuhusu ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu, amesema Sheria ya Watu Wenye Ulemavu (Sura ya 183) pamoja na Mkakati wa Kitaifa wa Elimu Jumuishi (2021/22–2025/26) vinaweka msingi wa kuhakikisha upatikanaji wa huduma, elimu jumuishi na ushiriki kamili wa watu wenye ulemavu katika jamii.

“Mafanikio ya jukwaa hilo yatapimwa kwa mabadiliko halisi katika jamii, yakiwemo huduma bora kwa waathirika wa ukatili, shule jumuishi, vijiji vinavyokataa ukeketaji na miundombinu inayowezesha watu wenye ulemavu kujitegemea,” amesema.

Awali, Mkurugenzi wa World Vision Tanzania, James Anditi, amesema jukwaa hilo limeshirikisha wadau kutoka nchi 23 duniani, likiongozwa na kaulimbiu isemayo “kubadili mitazamo, kuvunja vikwazo na kufungua fursa.”

Amesema jukwaa hilo limekutanisha wadau kujadili namna bora ya kuimarisha usawa wa kijinsia, kulinda haki za watu wenye ulemavu na kuhakikisha kila mtu anashirikishwa kikamilifu katika mchakato wa maendeleo bila ubaguzi.

“Tumekuwa na kongamano la kimataifa linalohusika na usawa wa jamii hasa wenye ulemavu na kuwapatia usawa katika maendeleo. Tunapoangalia mambo ya kijinsia na ulemavu, hatuwezi kusonga mbele kama taifa tusipowapa wenzetu nafasi ya kushirikishwa.

“Tunashukuru Serikali kwa ushirikiano wake, na tunatakiwa sisi wadau tuungane kuhakikisha usawa unakuwepo kwa makundi yote,” amesema mkurugenzi huyo.