Winga Msauzi amtuliza Mzize miezi minne ya majaribu

SIKU chache baada ya kukutana na Clement Mzize, huko Afrika Kusini ambapo straika huyo wa Yanga alienda kwa ajili ya matibabu ya goti, nyota wa zamani wa timu hiyo, Mahlatse Makudubela ‘Skudu’ amemtuliza mshambuliaji huyo chipukizi kwa hali aliyokutana nayo msimu huu.

Skudu, anayekipiga kwa sasa Siwelele FC ya Sauzi, amesema kuwa Mzize bado ana nafasi kubwa ya kufanya makubwa katika soka la Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla licha ya kukumbwa na majeraha yaliyomweka nje kwa muda mrefu msimu huu.

“Najua mashabiki watakuwa na hofu baada ya Clement kuumia tena wakati wa maandalizi ya mechi ya mwisho ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Kabylie,” amesema Skudu na kuongeza;

“Naamini kwamba atarejea akiwa imara zaidi, nilikuwa na wakati naye mzuri nilipomtembelea (Afrika Kusini) na nilimweleza kwamba hiki ni kipindi kifupi na atarejea katika hali yake ya kawaida.”

Mzize alikumbana na jeraha hili Septemba 27, 2025, katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wiliete Benguela ya Angola na kuanza mchakato mrefu wa matibabu pamoja na upasuaji wa Desemba 2025, kabla ya kurudi tena kwenye kikosi cha Yanga.

Baada ya kurejea mshindi huyo wa tuzo ya Bao Bora la Mwaka 2025 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), alijitonesha wakati wa maandalizi ya mechi ya mwisho ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya dhidi ya JS Kabylie.

Skudu aliendelea kwa kusema Mzize; “Najua kipaji alinacho kwa sababu tumecheza wote Yanga na kwa umri wake bado ana nafasi ya kufanya makubwa. Wakati bado upo. Tunapaswa kumpa moyo, kumpa muda na kumuunga mkono kila hatua ya safari yake.

Kwa mujibu wa daktari wa klabu ya Yanga, Moses Etutu, Mzize atakuwa nje ya uwanja hadi kufikia mwisho wa msimu huu na hivyo kutarajiwa kurudi kucheza tena katika msimu ujao wa mashindano

Yanga kwa sasa imesaliwa na washambuliaji watatu wa kati ambao ni mzawa Emmanuel Mwanengo aliyetua kutoka TRA United, Prince Dube na Laurindo Aurelio ‘Depu’ aliyekuwa Poland.