Watanzania waishio Mashariki ya Kati watakiwa kufanya haya kujinusuru…

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imewataka Watanzania wanaoishi au waliopo katika nchi za Mashariki ya Kati kuwa waangalifu na kufuata maelekezo yanayotolewa na mamlaka za nchi husika, kufuatia kuzorota kwa hali ya usalama katika ukanda huo.

Tahadhari hiyo inakuja baada ya kuibuka kwa mapigano makali ya makombora kati ya Iran na Israel, kufuatia kifo cha Kiongozi Mkuu wa Iran, Ali Khamenei, kilichoripotiwa kutokea Februari 28, 2026 baada ya shambulizi la pamoja la Marekani na Israel.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baada ya tukio hilo Iran na Israel zimekuwa zikirushiana makombora, huku Iran ikishambulia maeneo yanayohusishwa na kambi za kijeshi za Marekani katika nchi mbalimbali za ukanda huo ikiwemo Bahrain, Kuwait, Qatar, Falme za Kiarabu na Saudi Arabia, hatua iliyoelezwa kuwa ni ya kulipiza kisasi.

Hali hiyo imezua hofu kubwa ya kiusalama si tu Iran na Israel, bali katika ukanda mzima wa Mashariki ya Kati kutokana na majibizano hayo ya kijeshi.

Katika taarifa iliyotolewa leo Jumanne, Machi 3, 2026, wizara hiyo imewataka Watanzania waliopo katika ukanda huo kuepuka safari zisizo za lazima za kwenda au kutoka Mashariki ya Kati kwa kipindi hiki, na kubaki katika makazi yao kadri inavyowezekana.

 Pia wametakiwa kufuata maagizo ya mamlaka za maeneo wanayoishi, kuwa waangalifu wakati wote na kuepuka maeneo yenye shughuli za kijeshi au kiusalama. Aidha, wametakiwa kutumia njia rasmi za mawasiliano kupata taarifa sahihi na kuhifadhi pasipoti pamoja na vitambulisho vya Tanzania katika sehemu salama na inayopatikana kwa urahisi endapo kutatokea dharura.

“Serikali inawasihi Watanzania walioko Mashariki ya Kati kujisitiri kwa uangalifu na kuendelea kufuatilia mawasiliano rasmi ya ubalozi na ya dharura,” imeeleza taarifa hiyo.

Kadhalika, Watanzania wameombwa kujisajili kupitia mfumo maalumu wa wizara kwa ajili ya ufuatiliaji wa karibu na uratibu wa msaada wa kibalozi endapo utahitajika.

Kwa masuala ya dharura au maelezo zaidi, wizara imewataka raia kuwasiliana na balozi za Tanzania zilizo katika miji ya Kuwait, Doha, Abu Dhabi, Ankara, Tel Aviv na Riyadh.

Serikali imesisitiza kuwa inaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya usalama katika eneo hilo na kutoa ushauri kwa raia waliopo au wanaopanga kusafiri kwenda katika nchi za Oman pamoja na mataifa mengine ya ukanda huo, ikibainisha kuwa katika nyakati za taharuki, usaidizi wa kibalozi ana kwa ana unaweza kuwa na mipaka kulingana na eneo na hali halisi ya kiusalama.