Afariki dunia kwa kudumbukia kisimani, Zimamoto watahadharisha

Mbeya. Mtoto Bryson Frank (15), mkazi wa mtaa wa Majengo, kijiji cha Iwalanje jijini Mbeya amefariki dunia baada ya kudumbukia kisimani wakati akifanya usafi, huku Jeshi la Zimamoto na Uokoaji likitoa tahadhari kwa wananchi.

Picha nyingine wananchi wakishuhudia mwili wa Bryson Frank aliyefariki kwa kudumbukia kisimani wakati akifanya usafi



Tukio hilo limetokea Machi 3, 2026 saa 6 mchana, huku ikielezwa Frank alikuwa akimsaidia aliyepewa kazi hiyo, Victor Mika, ambapo aliingia kisimani kwa ajili ya kufuata ndoo iliyodumbukia ndani.

Akithibitisha tukio hilo, Ofisa Opereshani wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mkoa wa Mbeya, Mrakibu Gervas Fungamali amesema walipata taarifa kutoka kwa msamaria mwema kuhusu uwapo wa kijana kutumbukia kisimani.

Picha nyingine wananchi wakishuhudia mwili wa Bryson Frank aliyefariki kwa kudumbukia kisimani wakati akifanya usafi.



Amesema baada ya jeshi hilo kufika eneo la tukio walikuta tayari amefariki dunia na mwili kuhifadhiwa katika Hospitali ya Igawilo jijini Mbeya, akibainisha marehemu alikuwa akiishi na bibi yake.

“Tulifanikiwa kumnasua kisimani japokuwa alikuwa ameshafariki na mwili upo Hospitali ya Igawilo kwa taratibu nyingine, niwaombe wananchi kuchukua tahadhari haswa wakati huu wa mvua nyingi.


“Mamlaka ya hali ya hewa imeshatangaza uwapo wa mvua, wananchi wote wenye visima vifunikwe, wanaoishi maeneo hatarishi wawe makini sawa na waendesha vyombo vya moto,” amesema Fungamali.

Ameongeza Jeshi hilo limejipanga kutoa huduma wakati wote kwa kuwa wanavyo vifaa bora na vya kisasa vinavyoweza kufika sehemu yoyote akiomba ushirikiano wa wananchi inapotokea majanga.