Arusha. Benki ya CRDB kupitia taasisi yake ya CRDB Bank Foundation imesaini mkataba wa makubaliano ya miaka mitano (MOU) na Umoja wa Maofisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri Tanzania (Redeoa) kwa lengo la kuwawezesha wanachama kiuchumi na kuongeza ustawi wao kifedha.
Uwezeshaji huo unalenga kuwapa wanachama wa Redeoa elimu ya kifedha, mafunzo ya ujasiriamali, upatikanaji wa mikopo nafuu, pamoja na mitaji ya kuanzisha na kuendeleza miradi ya kipato ili kupanua vyanzo vya mapato ya maofisa elimu na kuhamasisha uwekezaji endelevu.
Makubaliano hayo yameingiwa jana Jumanne, Machi 3, 2026 kwenye mkutano mkuu wa 12 wa Redeoa unaoendelea jijini Arusha.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Mwambapa amesema mpango huo umeundwa kwa kuzingatia nafasi muhimu ya maofisa elimu katika kuhakikisha na kukuza ubora wa elimu nchini.
Amebainisha benki hiyo imetenga zaidi ya Sh20 bilioni kwa ajili ya miradi ya elimu, ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya shule, utoaji wa samani, miradi ya maji, kampeni za utunzaji wa mazingira, na miradi ya kiuchumi inayolenga walimu na maofisa elimu.
“Tunataka kuona maofisa elimu wanapanua vyanzo vya mapato yao kupitia miradi halali ya kiuchumi ndio maana tutatoa mafunzo ya kina kuhusu usimamizi wa fedha, uwekezaji, na matumizi sahihi ya mikopo ili kuhakikisha wanufaika wanapata matokeo chanya na endelevu,” amesema.
Mwambapa amesema mafanikio ya makubaliano hayo yatazingatiwa kwa kuangalia ongezeko la miradi ya kipato miongoni mwa maofisa elimu na ustawi wao wa kifedha kwa ujumla.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Elimu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Emmanuel Shindika, ameipongeza CRDB kwa kuonyesha imani kwa maofisa elimu.
Amesema fursa hizo za kifedha zitawawezesha kujiongezea kipato na kuimarisha hadhi yao kiuchumi lakini pia kuboresha utendaji kazi katika maeneo yao ya kazi.
Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, akizungumza katika mkutano mkuu wa 12 wa wanachama wa REDEOA, unaofanyika jijini Arusha kwa siku tano juu ya mpango wa benki hiyo kuwawezesha wanachama hao kiuchumi.
“Walimu na maofisa elimu wenye utulivu wa kifedha hufanya kazi kwa tija zaidi na kuwa na ustahimilivu na uthubutu katika majukumu yao ya kila siku,” amesema Dk Shindika.
Mwenyekiti wa Redeoa, Martin Nkwabi amesema makubaliano hayo yamekuja kwa wakati mwafaka, kwani wanachama walikuwa wanatafuta jukwaa la kifedha litakaloziwezesha kuanzisha na kuendeleza miradi ya uzalishaji mali.
Amesema mpango huo pia utahamasisha matumizi ya Tehama katika huduma za kifedha na usimamizi wa miradi.
“Lakini pia italeta utulivu kazini na kuepuka mikopo ya mara kwa mara kwa walimu kwa ajili ya kutafuta namna ya kujikimu katika mahitaji yao ya kila siku kipindi ambacho wanasubiri mishahara,” amesema.
Ofisa wa elimu kutoka Mkoa wa Kilimanjaro, Abel Mtupwa, amesema wanatarajia mpango huo kuunda utamaduni wa uwekezaji, akiba, na mipango ya maendeleo ya muda mrefu miongoni mwa wanufaika.
“Hatua hii tunatarajia italeta mabadiliko chanya katika ustawi wetu binafsi na maendeleo ya sekta ya elimu kwa ujumla, hasa tunapokuwa katika hali ya utulivu,” amesema.