KOCHA Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves, amethibitisha kwamba, nahodha msaidizi wa kikosi hicho, Dickson Job, hatakuwa sehemu ya mechi ya kesho Alhamisi dhidi ya Singida Black Stars kufuatia kuumia enka.
Kwa mujibu wa Pedro, Job aliyeumia enka katika Dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba iliyomalizika kwa timu hizo kushindwa kufungana wikiendi iliyopita, anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa takribani miezi miwili.
Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mechi ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa mkoani Singida kesho Machi 5, 2026 dhidi ya Singida Black Stars, Pedro amesema mbali na Job, pia hali ya Pacome Zouzoua haipo vizuri.
“(Job) ameumia na atakuwa nje kwa miezi miwili au inaweza kuwa tofauti kidogo,” amesema Pedro raia wa Ureno.
“Kuhusu Pacome kiukweli bado hajakaa sawa, lakini tutaona baada ya mazoezi ya leo, na ni kweli tuna idadi kubwa sana ya majeruhi ila haizuii sisi kujituma,” alithibitisha kocha huyu.
Job ambaye amekuwa mchezaji muhimu wa kikosi cha kwanza Yanga, alianza mechi hiyo ya dabi akiwa nahodha, akaumia dakika ya 34 ambapo madaktari waliingia uwanjani kumtibia, kisha akafanyiwa mabadiliko, akaingia Bakari Nondo Mwamnyeto ambaye ndiye nahodha mkuu wa kikosi hicho.
Kukosekana kwa Job katika mechi ya Ligi Kuu Bara kesho dhidi ya Singida Black Stars itakayochezwa mkoani Singida, kunatoa nafasi kwa Pedro kumtumia Mwamnyeto au Frank Assinki eneo la beki wa kati sambamba na Ibrahim Bacca.
Kwa upande wa Pacome, aliumia Februari 15, 2026 katika mechi ya mwisho Kundi B kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Kabylie ambayo Yanga ilishinda 3-0. Tangu hapo, hajacheza mechi nne zikiwamo tatu za Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo, JKT Tanzania na Simba, moja ikiwa ya Kombe la FA dhidi ya Cosmopolitan.