Riyadh. Kituo cha CIA kilichopo ndani ya ubalozi wa Marekani mjini Riyadh, kimeripotiwa kushambuliwa na droni zinazodaiwa kutoka Iran, katika tukio linaloashiria kuongezeka kwa mvutano wa kijeshi katika Ukanda wa Ghuba.
Kwa mujibu wa vyanzo vya Saudi Arabia, droni mbili zilidondoka karibu na eneo la ubalozi na kusababisha moto mdogo pamoja na uharibifu wa mali, ikiwemo sehemu ya paa la jengo kuporomoka. Hata hivyo, hakuna taarifa za majeruhi, na wafanyakazi waliagizwa kubaki ndani kwa tahadhari.
Idara ya Ulinzi ya Saudi imesema madhara yalikuwa madogo na hayakuathiri moja kwa moja wafanyakazi wa kiusalama. Kwa upande wake, CIA haikutoa maelezo ya kina kuhusu uharibifu au hali ya kiusalama, ikieleza inaendelea kutathmini tukio hilo.
Serikali ya Marekani iliwataka raia wake kuepuka ubalozi huo hadi taarifa zaidi zitakapotolewa, huku huduma za kawaida na dharura zikiwa zimesitishwa kwa muda.
Shambulio hilo linafuatia operesheni ya kijeshi iliyoripotiwa kufanywa na Marekani na Israel dhidi ya Iran Februari 28, ambayo ilidaiwa kumuua kiongozi wa juu wa Iran, Ali Khamenei pamoja na maofisa waandamizi wa kijeshi. Tukio hilo lilichochea mashambulizi ya kulipiza kisasi kutoka Tehran, yakihusisha makombora na droni kulenga vituo vya kijeshi vya Marekani na washirika wake katika eneo la Ghuba.
Saudi Arabia pia imethibitisha kuwa droni hizo zilionekana karibu na kiwanda cha mafuta cha Ras Tanura Refinery, huku tahadhari ya usalama ikiimarishwa katika mataifa ya Ghuba.
Hadi sasa, takribani wanajeshi 50,000 wa Marekani wameripotiwa kupelekwa katika eneo la Ghuba. Wakati huo huo, wanajeshi wanne wa Marekani wamefariki dunia katika shambulio la droni huko Port Shuaiba, Kuwait, wakihusishwa na operesheni ya kijeshi iliyopewa jina la “Epic Fury,” inayolenga kukabiliana na tishio la makombora na droni za Iran.
Rais wa Marekani, Donald Trump, ameapa kulipiza kisasi kufuatia vifo vya wanajeshi hao.
CIA ni taasisi ya kijasusi ya Marekani yenye jukumu la kukusanya, kuchambua na kusambaza taarifa za kiintelijensia kwa rais na vyombo vya ulinzi. Hutumia mbinu mbalimbali, zikiwemo Humint (taarifa kutoka kwa watu), pamoja na teknolojia za kisasa kama picha za satelaiti na ufuatiliaji wa mawasiliano ya kielektroniki.
Aidha, CIA hufanya operesheni za siri nje ya Marekani, zikiwamo za kuzuia ugaidi, kuvunja mitandao ya kigaidi na kusaidia kulinda masilahi ya kimkakati ya taifa hilo. Katika historia yake, taasisi hiyo imehusika katika matukio makubwa ya kisiasa na kijeshi duniani, na imeendelea kuwa mhimili muhimu wa sera za usalama wa Marekani.
Tukio la Riyadh linaonyesha jinsi mzozo kati ya Marekani na Iran unavyoweza kuathiri usalama wa kimataifa, na kuongeza shinikizo kwa jumuiya ya kimataifa kutafuta suluhu ya haraka ya kidiplomasia.