Mwanza. Wizara ya Viwanda na Biashara imesema Serikali haitaridhishwa na ongezeko la takwimu za usajili wa kampuni na leseni pekee, bali inataka kuona matokeo halisi yanayogusa maisha ya wananchi, ikiwamo ajira mpya na ukuaji wa biashara ndogo na za kati.
Akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) leo Jumanne, Machi 4, 2026, Waziri wa wizara hiyo, Judith Kapinga, amesema ni lazima ongezeko la usajili litafsiriwe kuwa fursa zaidi kwa vijana na ukuaji wa uchumi jumuishi.
“Serikali haitaridhika na takwimu za usajili na leseni pekee. Tunataka kuona matokeo halisi kwa wananchi… ongezeko la usajili na leseni linapaswa kutafsiriwa kuwa ajira mpya, ukuaji wa biashara ndogo na za kati, na fursa zaidi kwa vijana wetu,” amesema Kapinga.
Katika kikao hicho kitakachojadili taarifa ya utendaji ya Brela kwa kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2025/26 pamoja na mpango na bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27, Kapinga amesema taasisi hiyo ni ya kimkakati katika ujenzi wa uchumi rasmi akisisitiza si taasisi ya usajili pekee bali ni lango la mafanikio ya biashara nchini.
Hata hivyo, Kapinga ameitaka taasisi kuongeza jitihada za kurasimisha sekta isiyo rasmi kwa kuweka mazingira rafiki yatakayowavutia wafanyabiashara kuingia kwenye mfumo rasmi. Amesisitiza kuwa Brela si taasisi ya usajili pekee bali ni lango la mafanikio ya biashara nchini.
Awali, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Brela, Godfrey Nyaisa, amesema baraza hilo linawakutanisha menejimenti na watumishi kujadili masuala ya kimkakati, kusikiliza mawazo ya wafanyakazi, na kushughulikia changamoto zinazowakabili ili kuongeza mshikamano na tija kazini.
Baadhi ya wafanyakazi wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) leo Jumanne Machi 4, 2026 jijini Mwanza.
Amesema baraza hilo la pili katika mwaka wa fedha 2025/26 litajadili ajenda kuu mbili, ikiwemo kupitia na kuchambua taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya nusu mwaka.
“Taarifa inaonesha utekelezaji wa malengo umefikia asilimia 78, hali inayodhihirisha taasisi ipo kwenye mwelekeo sahihi wa kufikia malengo ya mwaka mzima,” amesema Nyaisa.
Kuhusu mapato, Brela imevuka lengo kwa kukusanya asilimia 105 ya makadirio, jambo linaloonesha uimara wa mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa rasilimali.
Nyaisa ameongeza kuwa Sh3.1 bilioni zimewasilishwa kwa Msajili wa Hazina, hatua inayothibitisha uwajibikaji katika usimamizi wa mapato ya umma.
Aidha, baraza hilo liliidhinisha mpango na bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27, ukiendana na vipaumbele vya kimkakati vya taasisi na Mpango Mkakati wa Brela wa miaka mitano (2026–2031) uliolenga kukuza uchumi shindani, kuongeza ajira kwa vijana, na kuimarisha maendeleo ya viwanda na sekta binafsi.
Mpango huo umejikita katika kuboresha huduma za usajili na utoaji wa leseni, kuimarisha mifumo ya kisheria na kitaasisi, kuendeleza miundombinu ya kidijitali, na kuongeza uwezo wa rasilimali watu.
Aidha, Brela itaendelea kuboresha sheria za usajili na leseni, kuimarisha mifumo ya Tehama, kutekeleza miradi ya kimkakati, na kufanya tafiti zitakazosaidia maamuzi ya taasisi.
Naye Ofisa Usajili wa Brela, Sophia Mtunzi, amesema kwa sasa wafanyabiashara wamerahisishiwa zaidi huduma kwa kuwa wanaweza kujisajili wenyewe kupitia mfumo wa mtandao hata kwa kutumia simu janja.
“Ukiwa na intaneti, unafungua akaunti kwenye tovuti ya Brela na unasajili jina la biashara, kampuni au nembo. Pia, tunatembelea mikoa mbalimbali kutoa elimu na kusajili wafanyabiashara papo kwa hapo,” amesema.