Kauli ya Dk Nchimbi imegusa changamoto za kisiasa Tanzania

Kauli ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Emmanuel Nchimbi ya kwamba; “mambo ya kugombana kivyama siyapendi, naona ni ujinga tu,” imeibua mjadala mpana kuhusu mwenendo wa siasa nchini na wajibu wa viongozi katika kulinda umoja wa kitaifa.

Kauli hiyo aliitoa wakati wa salamu za rambirambi kwenye mazishi ya Polycarp Kardinali Pengo akisisitiza umuhimu wa Watanzania kuacha misuguano ya kisiasa isiyo na tija.

Katika maelezo yake, Makamu wa Rais alisisitiza kuwa Tanzania ni nchi moja na kila mwananchi ana nafasi na wajibu wa kuitumikia kwa kadiri ya uwezo wake.

Alionya dhidi ya tabia ya wanasiasa au wanachama wa vyama mbalimbali kuendeleza migogoro kwa misingi ya tofauti za kiitikadi, akieleza kuwa vyama vya siasa vimeundwa kwa mujibu wa Katiba na vinapaswa kuheshimiwa kwa usawa. Kwa mtazamo wake, kujiunga na chama chochote cha siasa ni njia halali ya kutaka kuitumikia nchi, na mwisho wa siku lengo ni moja utumishi kwa taifa.

Kauli hii inagusa kiini cha changamoto ya siasa zetu; ushindani unaovuka mipaka ya hoja na kuingia katika uhasama. Ni ukweli usiopingika kwamba katika nyakati tofauti, kumekuwapo kauli kali na matendo yanayoashiria ubaguzi wa kisiasa, hata katika baadhi ya maeneo ya kiutendaji.

Hali hiyo hujenga hisia miongoni mwa wananchi kuwa haki na fursa hutegemea itikadi badala ya misingi ya kisheria na usawa.

Kwa kukemea “ujinga wa kugombana kivyama,” Makamu wa Rais anatoa ujumbe unaokumbusha kuwa tofauti za kisiasa si uadui. Ushindani wa kisiasa unapaswa kuwa wa hoja, sera na mikakati ya maendeleo, si mashindano ya kudhalilishana au kunyimana haki.

Pale ambapo viongozi wanatumia nafasi zao kuendeleza migawanyiko, wanadhoofisha mshikamano wa kitaifa na kuondoa imani ya wananchi kwa taasisi.

Makamu wa Rais alikumbusha pia kuwa alipokuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), alikuwa akiwakemea wanachama waliokuwa wakitoa kauli za kudhalilisha vyama vya upinzani.

Kauli hii inaashiria msimamo kwamba heshima kwa wapinzani si udhaifu, bali ni uthibitisho wa kukomaa kisiasa. Demokrasia haiwezi kustawi bila kutambua uhalali wa mawazo tofauti.

Ndani ya mwezi mmoja, Makamu wa Rais ametoa kauli kadhaa zenye mwelekeo wa kuhimiza maridhiano na utulivu.

Miongoni mwao ni wito wa kusubiri matokeo ya Tume ya Uchunguzi kuhusu matukio yaliyopita badala ya kuendelea kuyajadili kwa jazba. Hii inaendana na dhana ya uongozi unaotafuta suluhu kupitia taasisi na taratibu rasmi, badala ya kuhamasisha mjadala usio na kikomo unaoweza kuamsha maumivu mapya.

Uchambuzi wa kauli yake unaonyesha kuwa anasisitiza siasa za staha na uwajibikaji. Anapotaja kuwa “utumishi ni utumishi,” anaweka mbele maslahi ya taifa kuliko maslahi ya vyama.

Huu ni mtazamo unaohitaji kuungwa mkono na viongozi wote, bila kujali itikadi zao. Taifa linapojengwa kwa misingi ya kuheshimiana, ushindani hugeuka kuwa chachu ya ubunifu na maendeleo badala ya chanzo cha mpasuko.

Hata hivyo, kauli pekee hazitoshi. Kinachohitajika ni utekelezaji unaoendana na maneno hayo kuhakikisha kuwa taasisi za umma zinatoa huduma bila upendeleo, wanasiasa wanawajibika kwa kauli zao na sheria zinatumika kwa usawa. Hapo ndipo ujumbe wa kupinga “ujinga wa kugombana” utakapokuwa na maana ya vitendo.

Kwa ujumla, kauli ya Makamu wa Rais ni ukumbusho muhimu katika kipindi ambacho ushindani wa kisiasa unaweza kugeuka kuwa chanzo cha taharuki.

Tanzania imejengwa juu ya misingi ya umoja, amani na mshikamano. Kulinda misingi hiyo ni wajibu wa kila kiongozi na kila mwananchi. Tofauti za kisiasa zipo na zitaendelea kuwepo, lakini zisigeuke kuwa sababu ya kuvunja daraja la kitaifa.

Mwenendo wa kuheshimiana na kujenga hoja ndio utakaoifanya demokrasia yetu iwe imara na yenye tija kwa kizazi cha sasa na kijacho.