Kesi ya Dk Manguruwe: Askari JWTZ aeleza alivyotapeliwa Sh8 milioni

Dar es Salaam. Shahidi wa 22 wa upande wa Jamhuri katika kesi ya kuendesha biashara ya upatu inayomkabili Mkurugenzi wa Kampuni ya Vanila International Ltd, Simon Mkondya (40) maarufu Dk Manguruwe na mwenzake, ameieleza jinsi alivyotapeliwa Sh8 milioni na mshtakiwa huyo kupitia kilimo cha vanila.

Shahidi huyo, Iddy Mndeme, ambaye ni Askari wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi Tanzania (JWTZ) ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Jumatano, Machi 4, 2026 wakati akitoa ushahidi katika kesi hiyo.

Mndeme alidai alitoa Sh8 milioni kwa ajili ya kilimo cha vanila na kwamba mavuno ya mzao hilo aliyowekeza kwa msimu mmoja, angepata Sh70 milioni.

Mkondya na mwenzake, Rweyemamu John (59), ambaye ni Meneja na Mkaguzi wa fedha wa kampuni hiyo, wanakabiliwa na mashtaka 126 yakiwemo ya kuendesha biashara ya upatu na utakatishaji fedha yanalomkabili Mkondya pekee yake.

Askari huyo ametoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini, anayesikilza kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 31523 ya mwaka 2024.

Akiongozwa kutoa ushahidi wake na wakili wa Serikali Winiwa Kasala, shahidi huyo alidai aliifahamu Kampuni ya Vanila kupitia kwa rafiki zake ambao nao ni askari wa jeshi hilo.

Alidai Januari 28, 2023 alisikia taarifa za Kampuni ya Vanila kupitia kwa rafiki zake hao ambao walimueleza manufaa kuhusu uwekezaji kiuchumi kupitia kampuni hiyo.

“Wanzetu walitueleza kuhusu uwekezaji wa vanila na jinsi utakaponufaika na mmoja wa watu waliokuwa wakijadili kuhusu uwezekano huo ni Seif Shauri Shemshuza,” alidai Mndeme na kuongeza

“Na kutokana na maelezo ya hawa wenzangu, Machi 22, 2023 mimi na Shemshuza tulienda na ofisi za Kampuni ya Vanila zilizopo katika jengo la Sky City na kumkuta dada mmoja, jina lake sikumbuki lakini alituambia ni ofisa masoko na akatupa elimu ya uwekezaji, lakini sisi tulipendezwa na kilimo cha vanila” alidai Mndeme

Alidai kesho yake yaani Machi 23, 2023, walirudi ofisi hapo kwa ajili ya kufanya uwekezaji, na Mndeme alipewa akaunti namba ya benki ya CRDB yenye jina la Kampuni ya Vanila kwa ajili kwenda kulipia Sh8 milioni kwa ajili ya kilimo cha vanila.

Amesema kisha alirudi ofisini hapo kuwapatia risiti ya malipo ambapo waliipkea na kuitoa kopi na kisha kusaini mkataba kwa ajili ya uwekezaji.

“Mimi na mwenzangu, tulitoka ofisi za vanila na kwenda Shakilango kuchukua mzigo na baada ya hapo tulienda katika benki ya NMB iliyopo Ubungo na kuhamisha fedha kutoka NMB kwenda akaunti ya CRDB ya Kampuni ya Vanila, kiasi cha Sh8 milioni,” alidai.

Alifanya uhamisho wa fedha hizo kwa ajili ya kilimo cha Vanila na baada ya hapo walirudi katika ofisi za kampuni hiyo ambapo walikutana na meneja masoko na kumpa risiti na kisha kusaini mkataba wa kilimo cha vanila.

Alidai meneja huyo alimwambia mkataba wake utaanza kufanya kazi baada ya wiki mbili, baada ya muda huo kupita aliwasiliana naye kufahamu zaidi kinachoendelea.

Alielezwa kilimo cha zao lake ni cha mwaka mmoja na miezi sita na kwamba kitaanza Machi 2023 hadi Septemba 2024, ambapo vanila zingekuwa tayari kuvunwa na kuuzwa.

“Yule dada alisema vitalu kwa ajili ya kilimo hicho vipo Zanzibar, hivyo wanaruhusiwa kwenda kutembelea huko ili kujua maendeleo yake,” alidai Mndeme

Alidai katika uwekezaji wake wa Sh8 milioni, angepata faida ya Sh70 milioni.

Alidai yeye na mwenzake Mei 2023 walienda Zanzibar kuangalia shamba la vanila na kupokelewa na wahudumu wa kampuni ya vanila.

“Wahudumu walitupeleka na kila mtu alionyeshwa kitalu chake, lakini vitalu hivyo, vilikuwa havina majina, lakini mimi nilikubaliana nao,” alidai

Alivyorudi Dar es Salaam, alichukua namba za simu za Instagram kwa ajili ya mawasiliano na aliyekuwa anapokea simu na kuzungumza naye alikuwa Mkondya ambaye alimtaja kuwa mvumilivu na mazao yanakwenda vizuri.

Alidai baada ya mwaka mmoja na nusu kupita, alimpigia simu Mkondya kuhusu mavuno yake, alimwambia walipata changamoto ya mvua kubwa ambayo iliharibu mazao, hivyo aliomba awe mvumilivu zaidi.

“Baada ya kuona hakuna mavuno, shahidi huyo alimwambia Mkondya amrudishie fedha zake na yeye alimwambia aandike barua kwenda kampuni ya vanila ili arudishiwa fedha zake.”

Hata hivyo, hakurudishiwa fedha hizo, hivyo kwenda kuripoti kituo cha polisi.

Shahidi alimtambua mshtakiwa mahakamani na pia aliomba mahakama ipokee kielelezo cha risiti ya benki ya malipo aliyofanya kwenda kampuni ya vanila.

“Mahakama inapokea risiti hii na kuwa kielelezo namba 17 cha upande wa jamhuri,” amesema Hakimu Mhini.

Baada ya shahidi hiyo kumaliza kutoa ushahidi, aliulizwa maswali ya dodoso na wakili wa washtakiwa, Benedict Mtulo na sehemu ya mahojiano ni kama ifuatavyo

Wakili: Nani alikushawishi kuwekeza katika kampuni hii?

Shahidi: Shemshuza na ofisa Masoko

Wakili: Ni kweli ulitoa fedha wa hiyari yako na wala hukulazimishiwa na mtu yoyote?

Wakili: Ni kweli kwamba ulivyoambiwa kuna faida kubwa, ulishawishika kupata fedha nyingi bila kufanya kazi ngumu?

Wakili: Ni kweli ulijiunga ili upate faida ya haraka bila kufanya kazi ngumu?

Shahidi: Mimi nilijishughulisha ndio maana nikawekeza pesa kwenye kampuni yao.

Wakili: Kabla ya kuingia katika mradi huu, ulifanya utafiti kujua hii kampuni?

Shahidi: Ndio nilifanya utafiti kwa kumuuliza yule dada akasema kampuni imesajiliwa na ni halali.

Shahidi: Pia niliona matangazo kwenye vyombo vya habari, ikiwemo Clouds Media Group, hapo niligundua ni kampuni halali, hivyo naweza kuwekeza.

Wakili: Mkataba wako na Kampuni ya Vanila umeuwasilisha mahakamani?

Wakili: Ulisema ulikwenda Zanzibar kuoneshwa kitalu chako, kwa hiyo hii kampuni wakati unalipia ulikuwa unajua kuwa ilikuwa tayari ina mashamba kwa ajili ya kilimo?

Wakili: Kumbe kutokurudishiwa fedha zako kwa wakati kulikuwa kuna tatizo kwenye kampuni, ni kweli?

Wakili: Kwa hiyo kusingejitokeza matatizo hayo ambayo Mkondya alikueleza, pengine ungepata fedha zako kwa wakati?

Wakili: Mbona hujaleta mkataba hapa mahakamani?

Wakili: Sasa tutajuaje kama ulienda Polisi kabla ya mkataba wako kuisha?

Shahidi: Siwezi kuenda kinyume na mkataba, mkataba ulipoisha bila kupata fedha zangu za uwekezaji ndio nilienda Polisi.

Wakili:  Utatudhibitishiaje kama uliambiwa ukiwekeza Sh8 milioni unapata faida ya Sh70 milioni?

Shahidi: Kwa mujibu wa nyaraka zao na hata kipeperushi chao ninacho hapa kinaeleza kuwa ukiwekeza Sh8 milioni unapata Sh70 milioni.

Mpaka sasa mashahidi 22 kati ya 177 wa upande wa jamhuri wameshatoa ushahidi dhidi ya washtakiwa hao.

Katika mashtaka hayo 126, mashtaka 117 ni ya kuendesha biashara ya upatu yanayowakabili washtakiwa wote wawili na mashtaka tisa ni ya kutakatisha fedha yanayomkabili Mkodya pekee yake.