Kiungo Twiga Stars afunguka faida, hasara kusogezwa WAFCON 2026

KIUNGO wa Timu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars, Maimuna Hamis ‘Mynaco’ amesema kusimamishwa kwa mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa wanawake (WAFCON) yana faida na hasara kwa upande wa wachezaji.

Twiga Stars iko UAE ikishiriki mashindano ya kujipima nguvu ya Pink Ladies Cup ambayo yalikuwa ni maandalizi ya WAFCON yaliyotarajiwa kuanza Machi 17, 2026 nchini Morocco, kabla ya kusogezwa mbele.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mynaco alisema kusogezwa mbele WAFCON kunampa nafasi kocha kujipanga zaidi na kuangalia wapi kikosi chake kina upungufu ili arekebishe.

Aliongeza kuwa, kupitia mashindano mbalimbali na mechi za kirafiki zinawafanya wachezaji waendelee kuzoea ugumu wa mechi na timu wanazokutana nazo.

“Faida ni kubwa kuliko hasara na kwa upande wetu wachezaji tumelichukulia jambo hilo kwa uzuri kwa sababu hivi sasa tumepata muda mzuri zaidi wa kujiandaa na kadri tunavyocheza kocha anaona makosa na haraka tunayafanyia kazi mazoezini,” alisema Mynaco na kuongeza.

“Tunapocheza na timu kama Ghana tupo nao kwenye mashindano, Urusi ni wakubwa, ndio kipimo kizuri kwetu na sidhani kama kusogezwa kwa ratiba ina hasara kwetu wachezaji labda gharama na muda.”

Ikiwa UAE, Twiga Stars ilianza kupoteza kwa mabao 4-1 dhidi ya Urusi, juzi ilitarajia kucheza mechi ya pili dhidi ya Hong Kong, lakini wapinzani walijiondoa kutokana na hofu ya kiusalama inayosababishwa na mzozo unaoendelea baina ya Iran, Israel na Marekani.

Katika WAFCON 2026 ambayo tarehe mpya inatarajiwa kutangazwa hapo baadaye, Twiga Stars imepangwa kundi B itakapokabiliana na Afrika Kusini, Ivory Coast na Burkina Faso.

Hii ni mara ya tatu Twiga Stars inacheza WAFCON, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2010 ilipoishia hatua ya makundi na 2024 pia ilipomaliza mkiani kwenye kundi C na pointi moja.

Kupangwa kundi hilo Twiga Stars kunaiweka kwenye changamoto kubwa, hasa dhidi ya Afrika Kusini ambao ni miongoni mwa timu bora barani Afrika na wenye uzoefu mkubwa wa mashindano ya kimataifa.

Hii ni mara ya tatu Tanzania kupangwa kundi moja na Afrika Kusini, Oktoba 31, 2010 zilipokutana kwa mara ya kwanza Stars ilitandikwa mabao 2-1 na 2024 zilitoshana kwa sare ya 1-1.

Hata hivyo ubora wa wachezaji wa Tanzania hasa wale wanaokipiga ligi mbalimbali duniani kunaifanya kundi hilo kuwa gumu kutokana na nafasi za kufuzu Kombe la Dunia la Wanawake 2027.

Kwa mujibu wa mfumo wa mashindano, timu nne zitakazofuzu hatua ya nusu fainali zitapata tiketi za moja kwa moja kushiriki Kombe la Dunia 2027, huku timu zitakazoishia  hatua ya robo fainali zikipewa nafasi ya kuwania tiketi mbili za mchujo.