Arusha. Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), limepewa jukumu la kupitia upya mfumo wa michango ya kifedha ya nchi wanachama na kupendekeza upya makadirio inayopaswa kulipwa itakayolingana na uwezo halisi wa kiuchumi wa kila nchi.
Hatua hiyo imekuja kufuatia kuchelewa mara kwa mara kwa baadhi ya nchi kuwasilisha michango yao ya uanachama, hali iliyosababisha shinikizo kubwa la kifedha ndani ya jumuiya hiyo na kuathiri utekelezaji wa programu na miradi muhimu ya maendeleo ya kikanda.
Kwa mujibu wa takwimu rasmi, hadi kufikia Januari 31, 2026, EAC ilikuwa inaidai jumla ya dola za Marekani 89,372,865 (zaidi ya Sh228.8 bilioni) kama michango ambayo haijawasilishwa na baadhi ya nchi wanachama.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inaongoza kwa kuwa na deni la dola milioni 27 (sawa na Sh69 bilioni) ikifuatiwa na Burundi dola milioni 22.7 (sawa na Sh58.1 bilioni), Sudan Kusini dola milioni 21.8 (sawa na Sh55 bilioni) na Somalia dola milioni 10.5 (sawa na Sh25.6 bilioni).
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jana Jumanne, Machi 3, 2026, Katibu Mkuu wa EAC, Veronica Nduva, amesema hadi sasa ni Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda pekee ndizo zilizokamilisha kwa wakati michango yao hadi mwaka wa fedha 2025/2026.
Kutokana na ongezeko la presha ya kifedha, wakuu wa nchi wa EAC wameelekeza baraza la mawaziri kuanza mapitio ya kina ya mfumo wa sasa wa mchango sawa kwa kila nchi, ambapo kila mwanachama huchangia dola milioni saba kwa mwaka katika bajeti ya jumuiya.
“Tumeamua hivyo baada ya kutambua nchi zetu wanachama nane haziko katika kiwango kimoja cha ukuaji wa uchumi au uwezo wa kukusanya mapato.
“Pendekezo linalojadiliwa linalenga kutengeneza sera mpya na kuanzisha mfumo mwingine wa mchango ulio sawa na wa haki zaidi, unaozingatia uwezo wa kiuchumi wa kila nchi badala ya kiwango kimoja kwa wote.”
Amesema suala hilo tayari linajadiliwa kwa kina na baraza la mawaziri kama ajenda ya kisera huku wakitarajia hadi Machi 7, 2026, mwelekeo mahsusi utakuwa umewekwa kwa ajili ya kupitisha fomula endelevu na jumuishi ya ufadhili.
Nduva amesema jumuiya imechagua njia ya diplomasia badala ya hatua za shinikizo katika kushughulikia madeni hayo.
“Hatujatoa matamko ya vitisho wala shinikizo lolote badala yake, tunaendelea kushirikiana kidiplomasia na nchi wanachama kuelewa changamoto zao na kuhimiza utekelezaji wa wajibu wao wa kifedha,” amesema.
Amesema changamoto za kifedha si za EAC pekee, bali ni la mashirika mengi ya kikanda na kimataifa ambayo nao wanakumbwa na hali kama hiyo hasa wakati nchi wanachama zinapokabiliwa na mdororo wa uchumi au misukosuko ya kisiasa.
“Michango haitakiwi kutugawa kwani leo nchi moja inaweza kuwa katika wakati mgumu kiuchumi na kesho ikawa nyingine hivyo mshikamano wa kisiasa na kiuchumi ndiyo msingi wa mafanikio ya EAC,” amesema.
Aidha baraza la mawaziri sasa linatarajiwa kuwasilisha mapendekezo ya mfumo endelevu wa michango utakaoiimarisha jumuiya kifedha bila kudhoofisha umoja wa nchi wanachama.
Akitoa maoni yake, mfanyabiashara wa mipakani kutoka Namanga, Fredrick Laswai, amesema mfumo wa mchango unaozingatia kipato cha kila nchi unaweza kuwa suluhisho la muda mrefu endapo utatekelezwa kwa uwazi, uwajibikaji na dhamira ya dhati ya kuimarisha mtangamano wa kikanda.
Awali, katika kikao cha mtandao cha Mkutano wa Tatu wa Bunge la Tano la Bunge la Afrika Mashariki (EALA), EAC iliwasilisha bajeti ya dola milioni 109.3 (sawa na Sh279.8 bilioni) kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri na Waziri wa Masuala ya EAC wa Kenya, Beatrice Askul Moe, alisema asilimia 62 ya bajeti hiyo dola milioni 67.76 (sawa na Sh173.3 bilioni) itatokana na michango ya nchi wanachama, huku washirika wa maendeleo wakitarajiwa kuchangia asilimia 38 iliyobaki dola milioni 41.58 (sawa na Sh106.5 bilioni).
Alieleza vipaumbele vikuu kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ni pamoja na kuimarisha amani, usalama na utulivu wa kisiasa katika ukanda huo ambayo ni nguzo muhimu katika kukuza mtangamano wa kiuchumi na kulinda ajenda ya maendeleo ya muda mrefu ya Jumuiya.