Arusha. Mahakama ya Rufani ya Tanzania imemuachia huru baba aliyekuwa amehukumiwa kifungo cha maisha kwa kosa la kumlawiti mwanaye wa miaka minne, baada ya kubaini dosari kubwa za kisheria na mapungufu ya ushahidi.
Uamuzi huo ulitolewa Machi 2, 2026 na jopo la majaji watatu Zephrine Galeba, Benhajj Masoud na Eliezer Feleshi na nakala ya hukumu kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama.
Baba huyo, mkazi wa Kijiji cha Mlua, Kondoa mkoani Dodoma, alishtakiwa kwa kosa la ulawiti kinyume na Kifungu cha 154(1) cha Kanuni ya Adhabu, akidaiwa kulitenda mwaka 2021. Awali alihukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Kondoa, na rufaa yake ya kwanza Mahakama Kuu Dodoma ilithibitisha hukumu hiyo.
Katika kesi ya awali, upande wa mashtaka uliita mashahidi watano na kuwasilisha kielelezo kimoja. Ilidaiwa kuwa mshtakiwa alikuwa akimfanyia mwanaye ukatili wa kimwili na baadaye tuhuma za ulawiti ziliibuka, zikajadiliwa katika mkutano wa kijiji Desemba 2021. Mtoto alipelekwa hospitalini ambako uchunguzi ulidai kubaini dalili za ukatili wa kingono.
Katika utetezi wake, mshtakiwa alikana shtaka hilo na kudai alikamatwa akiwa shambani kufuatia mgogoro mwingine. Alidai alipigwa na wanamgambo na hata kulawitiwa yeye pamoja na mwanaye, madai ambayo hayakupingwa na mashahidi waliomkamata kwa kuwa hawakuitwa mahakamani.
Katika rufaa ya pili, alidai kuwa shtaka lilikuwa na kasoro kwa kutobainisha tarehe mahsusi ya tukio, kinyume na matakwa ya Kifungu cha 135 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA). Pia alieleza kuwa mahakama za chini zilipuuza utetezi wake na kuthibitisha kosa bila ushahidi wa kuondoa shaka.
Upande wa Jamhuri uliunga mkono rufaa hiyo, ukikiri kuwa hati ya mashtaka haikuendana na ushahidi uliotolewa, kwani mashahidi walitaja Desemba 21, 2021 kama siku ya tukio, lakini shtaka lilieleza tarehe tofauti mwaka 2021 bila kurekebishwa chini ya Kifungu cha 251 cha CPA. Ilielezwa kuwa kasoro hiyo ilimnyima mshtakiwa fursa ya kuandaa utetezi wake ipasavyo.
Katika hukumu, Jaji Feleshi alisema kutobainishwa kwa tarehe sahihi na kushindwa kurekebisha shtaka kulisababisha utata uliomuathiri mshtakiwa. Aidha, majaji walibaini kuwa mashahidi muhimu hawakuitwa na kulikuwa na mkanganyiko kuhusu mazingira ya kukamatwa kwa mshtakiwa na kupelekwa hospitalini kwa mtoto.
“Kwa kuzingatia kanuni kwamba mashaka katika kesi ya jinai huamuliwa kwa faida ya mshtakiwa, tunashindwa kuona namna kosa lilithibitishwa bila shaka yoyote,” ilieleza sehemu ya hukumu hiyo.
Mahakama pia ilieleza kuwa utetezi wa mshtakiwa haukutathminiwa kwa uzito unaostahili na mahakama za chini, jambo lililoacha mashaka ambayo hayakuondolewa.
Kutokana na misingi hiyo, Mahakama ya Rufani iliruhusu rufaa, ikafuta hukumu ya kifungo cha maisha na kuamuru mshtakiwa aachiwe huru isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine halali za kisheria.