MAKATBU WAKUU SADC WAPITIA MPANGO WA MAENDELEO WA KANDA. WABAINI CHANGAMOTO ZA UTEKELEZAJI

::::::::::

Kikao cha Makatibu Wakuu na Maafisa Waandamizi wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kupitia utekelezaji wa Mpango Mkakati Elekezi wa Maendeleo ya Kikanda (Regional Indicative Strategic Development Plan- RISDP) kimeanza leo tarehe 04 Machi 2026 jijini Pretoria, Afrika Kusini.

Ujumbe wa Tanzania katika kikao hicho cha utangulizi kuelekea Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC utakaofanyika Machi 12 na 13, 2026, unaongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa. 

Wakati wa hotuba za ufunguzi,  Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano ya Afrika Kusini, Balozi Tebogo Seokolo na Katibu Mtendaji wa SADC, Mhe. Elias Magosi walisisitiza umuhimu wa  mpango wa RISDP wa mwaka 2020 – 2030 kufanyiwa tathmini kwa lengo la kujiridhisha ufanisi wake na kubaini changamoto ili ziweze kupatiwa ufumbuzi kwa muktadha wa kuboresha utekelezaji wa mpango huo kwa kipindi cha miaka mitano iliyosalia 2026-2030.

Changamoto mbalimbali zimebainishwa katika utekelezaji wa mpango wa RISDP ambazo ni pamoja na uhaba wa rasilimali fedha; utofauti baina ya vipaumbele vya kitaifa na kikanda na kutorandana kwa sera zilizotungwa na utekelezaji halisi wa mpango wa RISDP.

Balozi Seokolo alieleza kuwa utekelezaji wa RISDP  ulipitia na unapitia changamoto nyingi kama vile madhara ya UVIKO-19, mabadiliko ya tabianchi, changamoto za kiusalama, uhaba wa nishati, usalama wa chakula na mabadiliko ya siasa za ulimwengu. Alibainisha kuwa, katika kukabiliana na changamoto hizo, SADC inahitaji mikakati thabiti na utekelezaji wa pamoja ili nchi wanachama ziweze kufikia malengo ya RISDP.