Makatibu Wakuu wa Nchi Wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanaosimamia masuala ya mtangamano wamekutana katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha, ikiwa ni muendelezo wa maandalizi ya Mkutano wa 25 Wakuu wa Nchi Wanachama wa EAC utakaofanyika tarehe 7 Machi 2026 jijini Arusha.
Kikao hicho cha Makatibu Wakuu ambacho ni sehemu ya Mkutano Maalum wa 59 wa Baraza la Mawaziri wa EAC, pamoja na masuala mengine umepokea na kujadili agenda na taarifa mbalimbali zilizowasilishwa na mkutano wa Ngazi ya Wataalamu uliofanyika tarehe 2 hadi 3 Machi 2026. Agenda na taarifa hizo zitawasilishwa na kujadiliwa kwenye Mkutano wa Mawaziri utakaofanyika tarehe 5 Machi 2026 jijini Arusha.
Akifungua mkutano huo Dkt. Caroline W. Karugu PhD, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki nchini Kenya, na Mwenyekiti wa mkutano huo, ameeleza kuwa Jumuiya imeendelea kupiga hatua kubwa ya maendeleo huku ikizingatia ustawi wa watu wake kwa kuwezesha shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo biashara na uwekezaji na utoaji wa huduma za kijamii.
Aliongeza kusema kuwa licha ya kujivunia mafanikio hayo yanayotokana na uongozi imara wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya, juhudi zaidi zinahitajika katika kuendelea kuibua na kutekeleza mikakati itakayosaidia kutatua changamoto mpya zinazoibuka ambazo zinaweza kukwamisha utekelezaji wa programu mbalimbali za Jumuiya.
Amebainisha baadhi ya mikakati hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya uchukuzi na mawasiliano ambayo itachagiza kasi ya ukuaji wa uchumi jumuishi na kuongeza uzalishaji wa bidhaa na huduma katika Jumuiya.
Miongoni mwa agenda zilizopokelewa na kujadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na; uzinduzi wa Mkakati wa Saba wa Maendeleo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (2026/27 – 2030/31), uteuzi wa Katibu Mkuu wa Jumuiya, uondoshwaji wa vikwazo vya biashara visivyo vya kiforodha (NTB’s), hali na utaratibu wa utoaji wa michango ya Jumuiya kutoka nchi wanachama, uteuzi wa Majaji wa Mahakama ya Jumuiya na Mkataba wa Ulinzi wa Pamoja wa EAC.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umeongozwa na Balozi Stephen P. Mbundi Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki akiambatana na Viongozi wengine Waandamizi wa Serikali wakiwemo Bw. Elia Mwandumbya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Aristides Mbwasi Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Samwel M. Maneno Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakurugenzi na Maafisa waandamizi wa Serikali.
.jpg)














