WAKATI wadau na mashabiki wa soka nchini wakijiuliza lini teknolojia ya usaidizi wa mwamuzi (VAR) itaanza kutumika katika mechi za Ligi Kuu Bara kufuatia makosa ya kibinadamu yanayoonekana mara kwa mara, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limefichua kuwa zimebaki hatua mbili kabla ya kuanza kuitumia.
Ishu ya VAR ambayo imekuwa mjadala kwa sasa imeibuka kufuatia makosa ya kibinadamu ambayo yalijitokeza katika Dabi ya Kariakoo iliyopigwa Jumapili iliyopita huko Unguja, Zanzibar ambapo ilishuhudiwa bao la Seleman Mwalimu likikataliwa kwa Simba huku Prince Dube akidaiwa kuotea wakati akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga.
Ikumbukwe kuwa Juni 13, 2024 aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alisema Serikali inakusudia kuwasilisha pendekezo la kuondoa kodi kwenye vifaa vya teknolojia inayomsaidia mwamuzi kufanya marejeo ya picha (Video Assistance Referee-VAR) kuanzia mwaka mpya wa fedha 2024/2025.
Alisema pendekezo hilo litawezesha viwanja vyote nchini vinavyotumika kuchezwa ligi hiyo kufungwa VAR lengo likiwa ni kuhakikisha matokeo yanayopatikana yanakuwa ya haki.
Dk Mwigulu ambaye kwa sasa ni Waziri Mkuu aliyasema hayo wakati akisoma Bajeti Kuu ya Serikali ya 2024-2025.
Pia Julai 15, 2024, aliyekuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alizindua teknolojia hiyo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Vifaa hivyo vilivyotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) pamoja na Azam Media, na VAR ilitarajiwa kutumika kuanzia msimu wa 2024-2025 wa Ligi Kuu Bara.
Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi, Karim Boimanda alisema kuwa VAR ni jambo la TFF, lakini lina taratibu zake.
“Hadi nchi zipate leseni na FIFA (Shirikisho la Soka Duniani) kuanza kutumia VAR kuna hatua nyingi za kiufundi zinazohitajika,” alisema.
Hata hivyo, akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo akatoa ufafanuzi kuhusu changamoto za utekelezaji wa VAR nchini.
“Kuna uzinduzi na matumizi ya VAR kwa mujibu wa taratibu,” alisema Ndimbo.
“Utaratibu wa FIFA unahitaji mafunzo maalumu. Hauwezi kutumia teknolojia moja kwa moja kwenye mechi. Mafunzo yapo kwenye module 6 (ngazi sita). Tumefanya ngazi nne, zimebakia mbili na wakufunzi wa FIFA ndio wamekuwa wakitoa maelekezo ya kufanyika kwa mafunzo hayo. Ukimaliza, ndipo unakuwa umehitimu sasa kuanza kutumia VAR.”
Ndimbo alibainisha kuwa, matumizi ya VAR hayachagui mechi moja tu.
“Waamuzi wetu wapo kwenye kozi. Hata sisi TFF tunasubiri kufikia hatua inayofaa. Ukipewa kibali lazima upewe asilimia ya mechi ambazo unaweza kutumia,” alisema.
Aliongeza kwamba, mchakato huu ni wa muda mrefu kwani waamuzi lazima wapewe mafunzo ili wapate ujuzi wa kutosha.
“Waamuzi wa kati, pembeni na wale wanaoongoza mechi lazima wawe na mafunzo. Kuna muongozaji na kila mmoja ana jukumu lake maalumu. Wote hawa wanapaswa kuwa na ujuzi wa kutosha. Si jambo la haraka, bali ni mchakato unaoendelea,” alisema Ndimbo.
Kwa viwanja vikubwa, ‘setup’ yaani kufunga VAR inakadiriwa kugharimu zaidi ya Sh280 milioni hadi Sh420milioni kwa uwanja mmoja. Hii inajumuisha vifaa vya kamera, kompyuta na software za kuchambua video, mafunzo ya waamuzi na watendaji pamoja na matengenezo ya kiufundi.
Hata hivyo, gharama ya mwanzo ni sehemu ya uwekezaji mkubwa unaohitajika ili kuhakikisha mfumo unafanya kazi kwa ufanisi.
TFF ina mpango wa kuanza kutumia VAR kwenye viwanja vikubwa kama Benjamin Mkapa, kisha kueneza hatua kwa hatua kwenye viwanja vingine.
Miongoni mwa mataifa ya kwanza na vinara katika matumizi ya VAR kwa Afrika ni Morocco ambapo mechi zao nyingi za Ligi na mashindano mengine ya ndani zinatumia teknolojia hiyo huku wakitumia kamera 8 hadi 12 kufanikisha hilo kwenye viwanja vingi.
Jalal Bouzrara ambaye ni mwandishi wa michezo nchini humo, alisema kwa kiasi kikubwa teknolojia hiyo imekuwa msaada nchini kwao.
“Najua haiwezi kuwa haraka kila sehemu kuwa na VAR lakini ni mchakato na kwa sababu tayari imeanza kutumika katika ngazi ya juu ya soka la Afrika basi inaweza kushuka chini na kuondokana na makosa mengi ambayo yamekuwa yakijitokeza,” alisema.
Katika michuano ya CAF, teknolojia ya VAR imekuwa ikitumika kuanzia hatua ya robo fainali. Hii imesaidia kuhakikisha uamuzi sahihi unaotolewa na waamuzi na kupunguza malalamiko kutoka kwa timu na mashabiki.