Meneja Singida BS atuma salamu Yanga

MENEJA Mkuu wa Singida Black Stars, Othmen Najjar amesema kikosi kipo tayari kwa mtihani wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga itakayochezwa Alhamisi hii Machi 5, 2026, akiweka wazi maandalizi yao yamejikita zaidi katika umakini, nidhamu na matumizi sahihi ya nafasi.

Najjar amekiri wazi kwamba, takwimu haziko upande wao, akieleza kuwa Yanga imeshinda mechi sita mfululizo dhidi ya Singida Black Stars katika mashindano yote. Hata hivyo, amesema historia hiyo haiwapi presha, bali inawapa motisha ya kupindua aina ya matokeo ambayo wamekuwa wakiyapata dhidi ya vigogo hao.

“Sote tunajua ubora wa Yanga, hivyo itakuwa mechi ngumu, naamini matokeo ya mechi iliyopita yameongeza kitu kwa upande wetu, ni wazi kwamba itakuwa mechi tofauti kabisa na iliyopita lakini hii ni nafasi kwa wachezaji kuonyesha yale ambayo tumekuwa tukiyafanyia kazi,” alisema na kuongeza;

“Nina uhakika kwamba tunao ubora wa kushindana na Yanga, ninachotamani zaidi ni kuona watu wa Singida wakiwa nyuma ya timu yao.”

Mara ya mwisho timu hizo zilipokutana ilikuwa katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026, ambapo Yanga ilishinda bao 1-0 hatua ya nusu fainali.

Katika msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara 2024-2025, Singida Black Stars ilipoteza kwa bao 1-0 nyumbani kabla ya kufungwa tena mabao 2-1 Dar.

Najjar alisema wataingia uwanjani wakiwa na mtazamo wa kupambana bila kuhofia ukubwa wa wapinzani.

 “Tunaiheshimu Yanga lakini tutacheza kwa kujiamini na kwa uwezo wetu wote,” alisema.

Alieleza pia ameimarisha safu ya ulinzi na kushambulia kwa pamoja kama timu, akiamini mshikamano utakuwa silaha muhimu kwao. Pia amewataka wachezaji wake kuongeza umakini katika utumiaji wa nafasi, akisema mechi za aina hiyo huamuliwa na makosa madogo.

Baada ya kumaliza na Yanga, Singida Black Stars yenye pointi 19 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa nafasi ya tisa baada ya mechi 11, itakuwa na kibarua kingine cha kucheza dhidi ya Simba, Machi 11 mwaka huu katika mwendelezo wa ligi hiyo. Kabla ya hapo, Machi 8, 2026 itaikaribisha Songea United katika hatua ya 32 Bora ya Kombe la Shirikisho.