Mtaalamu azungumzia faida, fursa katika sekta ya gesi

Dar es Salaam. Mtaalamu wa Nishati ya Gesi kutoka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Mhandisi Geturu Bosinge, amesema watu wengi hawana ufahamu wa kutosha kuhusu faida za nishati ya gesi asilia katika matumizi mbalimbali, ikiwemo magari na mafuta.

Amesema sekta ya gesi asilia ina fursa nyingi ambazo bado hazijafahamika wala kutumiwa kikamilifu na wananchi na wahandisi. Bosinge, ambaye ni Meneja wa Idara ya Gesi Asilia Iliyobanwa (CNG), ametoa kauli hiyo wakati akiwasilisha mada kwenye maadhimisho ya Siku ya Wahandisi Duniani yaliyofanyika DIT leo Machi 4, 2026, yakiwa na kaulimbiu “Uhandisi Mahiri kwa Mustakabali Endelevu kupitia Ubunifu na Ubadilishaji wa Kidijitali.”

Amesema matumizi ya gesi asilia yana faida za kimazingira na kiuchumi, kwani hayachafui mazingira kama mafuta ya petroli na dizeli, na pia hupunguza gharama kwa takribani asilimia 60, hususan katika magari yanayotumia mfumo huo.

“Lakini watu wengi bado hawajapata uelewa huu, hivyo inahitajika elimu ya kutosha,” amesema.

Kuhusu fursa zilizopo, Bosinge amesema ongezeko la matumizi ya gesi katika magari limefungua nafasi kwa wahandisi katika kubadili na kufunga mifumo hiyo. Ameeleza kuwa tangu mwaka 2018, zaidi ya magari 8,000 yamefungwa mfumo wa gesi Dar es Salaam, huku DIT ikihudumia zaidi ya magari 4,000. Kwa sasa, kuna karakana 16 zilizofunguliwa na wahandisi waliofundishwa DIT, pamoja na vituo 10 vya kujazia gesi na mipango ya kuongeza vingine na kuanzisha vituo vinavyotembea.

Aidha, amesema bado kuna fursa katika usambazaji wa mitungi na utengenezaji wa vifaa vya majiko ya gesi, akihimiza wahandisi kuendeleza ubunifu katika teknolojia za gesi asilia.

Kwa upande wake, Rais wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania, Mhandisi Asa Mwaipopo, amesema Machi 4 ya kila mwaka huadhimishwa Siku ya Kimataifa ya Uhandisi kwa Maendeleo Endelevu, kwa kutambua mchango wa uhandisi katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs).

Amesema maendeleo ya teknolojia za kidijitali, akili bandia na mifumo mahiri yanabadilisha namna ya kupanga na kutekeleza miradi, na kuwataka wahandisi kuongoza mabadiliko hayo kwa kuzingatia maadili na ushirikishwaji.

Tanzania pia itakuwa mwenyeji wa wiki ya 12 ya uhandisi Afrika ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) na mkutano wa 11 wa uhandisi Afrika utakaofanyika Septemba 13–17, mwaka huu, fursa aliyoitaja kuwa muhimu kwa kubadilishana maarifa na kuonesha ubunifu.

Mkuu wa Idara ya Uhusiano na Viwanda wa DIT, Dk Gaudence Tesha, akifungua maadhimisho hayo, amewataka wahandisi kutumia taaluma yao kwa manufaa ya jamii na maendeleo ya Taifa.