Ninja aelezea uzoefu anaoupata Championship

BEKI wa zamani wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ anayeichezea Transit Camp inayoshiriki Championship, alisema anajifunza vitu vingi kutoka ligi hiyo anayocheza kwa mara ya kwanza, huku akifichua huko zaidi nguvu inatumika sana.

Ninja aliyezaliwa Zanzibar Januari 21, 1998 akiwa na umri wa miaka 27 hivi sasa, alisema ugumu wa Ligi ya Championship ni kwa zile mechi zisizoonyeshwa zinakuwa na makosa mengi na ni nadra mchezaji kujitambua na kujirekebisha kama hatakuwa mtu wa kujifunza na kuzingatia malengo ya mbele.

“Ni watu wachache wanaweza wakakufuata na kukurekebisha, vinginevyo inakuwa ngumu kujua unakosea kwa faida ya kupandisha kiwango.

“Napata uzoefu mwingine tofauti na ule niliyoupata Ligi Kuu Bara, baada ya kukaa bila timu niliona nijipange upya kwa kujiunga na Transit Camp.

“Faida ya mechi inayoonyeshwa ni ngumu kufanyika makosa mengi, tofauti na kutoonyeshwa ambapo makosa yanazidi lakini wapo baadhi ya watu wachache ukikosea wanakuambia hiki siyo sahihi.

“Kuhusu upande wa maisha, timu ninayoitumikia ipo vizuri, tofauti na ninavyosimuliwa na wachezaji wa timu zingine na maisha ya soka yanahitaji uvumilivu wa juu, kuna kipindi unakuwa juu na kipindi unashuka ambacho kinahitaji mapambano na kutokukata tamaa,” alisema Ninja.

Kwa mara ya kwanza, Ninja alijiunga na Yanga msimu wa 2017-2018, baadaye akapata nafasi ya kwenda kucheza MFK Vyskov ya Jamhuri ya Czech msimu wa 2019-2020 iliyomtoa kwa mkopo LA Galaxy 11 ya Marekani.

Msimu wa 2020/21, akarejea Yanga, iliyomtoa kwa mkopo Dodoma Jiji alipokwenda kucheza msimu wa 2021-2022, mkataba wake ulipomalizika, akatua FC Lubumbashi msimu wa 2023-2024 na 2024-2025 aliichezea FC Lupopo zote za DR Congo, kabla ya msimu huu kutua Transit Camp.