:::::::
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima, amesema mwanamke anapotumia nishati safi ya kupikia anapata muda zaidi wa kushiriki shughuli za uzalishaji, ubunifu na malezi bora ya familia.
Akizungumza leo Machi 4, 2025 katika kongamano la wanawake wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) la kuhamasisha matumizi ya nishati safi, lililofanyika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, Gwajima amesema nishati safi inakomboa wanawake na kuwapa hadhi na fursa katika jamii
“Katika muktadha wa kitaifa serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuharakisha matumizi ya nishati safi ya kupikia. Ikiwemo kuharakisha umeme ufike katika maeneo yote ya mijini na vijiji. Na kuchochea matumizi ya umeme, gesi asilia na teknolojia bunifu za kupikia.
“Kazi hii Muheshimiwa Rais ameisimamia vizuri sana. Umeme umetanda nchini katika maeneo ambayo yalisubiri kwa muda mrefu lakini yameweza kupatikana katika awamu ya sita,”amesema Waziri Gwajima ambaye ni mgeni rasmi kwenye kongamano hilo.
Amesema mara nyingi watu wamekuwa na dhana potofu, kwamba umeme ni gharama ukitumia kwenye kupikia.
“Lakini siyo kweli hata kidogo, maendeleo ya teknolojia ya kisasa yameleta majiko yaliyotengenezwa kwa kutumia umeme kidogo sana. Na yanapatikana kwa bei nafuu yapo kila pahala”amesema Waziri Gwajima



