Samia ardhi kliniki, chachu ya kupunguza migogoro ya ardhi Simiyu

Simiyu. Uzinduzi wa kliniki ya ardhi, maarufu Samia Ardhi Kliniki umeelezwa kuwa chachu ya kupunguza migogoro ya ardhi mkoani Simiyu na faraja kwa vyombo vya utoaji haki, hususan mahakama.

Akizungumza Machi 4, 2026 mjini Bariadi wakati wa uzinduzi huo, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Simiyu, Husein Mtembwa, amesema kuanzishwa kwa kliniki hiyo kutasaidia kupunguza mlundikano wa mashauri yanayotokana na migogoro ya ardhi, ambayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la kesi katika mahakama za mkoa huo.

Amesema kupitia jukwaa hilo, wananchi watapata fursa ya kusikilizwa na kupatiwa ufumbuzi wa haraka kabla migogoro haijafika mahakamani, hatua itakayosaidia kupunguza gharama na muda wa usikilizaji wa mashauri.

“Sehemu kubwa ya mashauri tunayopokea yanahusu migogoro ya ardhi. Kupitia kliniki hii, wananchi watapata elimu na usuluhishi wa mapema kabla ya kufikia hatua ya kufungua kesi mahakamani,” amesema.

Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Simiyu, Denis Rugemalira akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa Samia Ardhi Kliniki mkoani humo. Picha na Samwel Mwanga



Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Simiyu, Denis Rugemalira, amesema lengo la Samia Ardhi Kliniki ni kuamsha chachu kwa wananchi, hususan wanawake, kujitokeza kumiliki ardhi kisheria.

Amesema mkoa huo umejiwekea lengo la kutoa hati miliki 3,000 kwa mwaka, lakini hadi sasa hati 1,441 ndizo zimetolewa, kati ya hizo 405 ni za wanawake sawa na asilimia 28 pekee.

 “Tunahitaji kuona uwiano wa umiliki wa ardhi kati ya wanaume na wanawake unakuwa sawa. Bado wanawake wanamiliki ardhi kwa kiwango kidogo ukilinganisha na wanaume,” amesema.

Akifungua rasmi kliniki hiyo ya siku sita, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha, amesema lengo kubwa ni kuwapatia wanawake elimu kuhusu umiliki na usimamizi wa ardhi ili waweze kudai na kulinda haki zao.

“Mfumo dume bado upo kwa kiwango kikubwa katika baadhi ya maeneo ya mkoa wetu. Tunataka kuona wanawake wanapewa kipaumbele katika kushughulikia changamoto za ardhi na wanapata haki yao ya kumiliki mali,” amesema.

Pendo Shija, mkazi wa Maswa ambaye amepatiwa hati miliki ya ardhi amesema kliniki hiyo imekuja wakati muafaka kwani wanawake wengi wamekuwa wakinyimwa haki ya kumiliki ardhi za familia.

 “Mara nyingi ardhi inaandikishwa kwa jina la mume pekee. Mwanamke akifiwa au kuachika anakosa pa kuanzia. Kliniki hii itatusaidia kujua haki zetu,” amesema.

Naye Victoria Zavala kutoka mjini Bariadi amesema migogoro mingi ya ardhi vijijini inatokana na ukosefu wa elimu.

 Stela Manyonyi ni mkazi wa wilaya ya Busega amesema kuwa Samia Ardhi Kliniki itakuwa suluhisho la kudumu la migogoro ya ardhi, kuongeza usawa wa kijinsia katika umiliki wa ardhi na kupunguza mzigo wa mashauri katika mahakama zilizoko katika mkoa huo.