Serikali ionyeshe njia ya kusaidia wanyonge

Kwa mara nyingine, Tume ya Ushindani wa Haki wa Kibiashara Zanzibar (ZFCC) imewaonya wafanyabiashara wanaokiuka bei elekezi za vyakula zilizopangwa na Serikali.

Tume hiyo imewataka wabandike bei za bidhaa zao mahali panapoonekana wazi, na kuonya kuwa watakaokiuka maelekezo hayo watachukuliwa hatua za kisheria.

Kwa mtazamo wa kawaida, hatua hiyo inaweza kuonekana kuwa ni jitihada za kulinda maslahi ya walaji, hususan katika mwezi wa Ramadhani ambamo mahitaji ya vyakula huongezeka.

Ni kipindi ambacho Serikali pia hupunguza ushuru kwa baadhi ya bidhaa ili kuweka nafuu kwa wananchi.

Hata hivyo, pamoja na nia hiyo njema, yapo maswali na malalamiko yanayohitaji kuchunguzwa kwa kina ili kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa pande zote.

Baadhi ya wafanyabiashara wanalalamika kuwa wanamiliki shehena ya bidhaa zilizoingizwa nchini mwezi mmoja au miwili kabla ya punguzo la ushuru kuanza kutumika.

Bidhaa hizo zilitozwa ushuru wa kawaida, hivyo gharama zake ni kubwa zaidi. Wanapoelekezwa kuuza kwa bei mpya elekezi bila kuzingatia hali hiyo, wanalazimika kuuza kwa hasara.

Endapo madai haya yana ukweli, basi ni muhimu kwa mamlaka husika kuyafanyia tathmini ili kuepusha taswira ya uonevu au matumizi mabaya ya mamlaka.

Hoja nyingine inayotolewa ni kwamba wakati wafanyabiashara wanasisitizwa kutoa nafuu kwa walaji, Serikali yenyewe imeongeza kwa zaidi ya asilimia 25 kodi za majengo yake yanayotumika kwa biashara ya vyakula miezi michache iliyopita. Ongezeko hilo linaongeza mzigo kwa wafanyabiashara, ambao hulazimika kutafuta namna ya kufidia gharama hizo.

Swali la msingi ni pengo la ongezeko la kodi litazibwa vipi kama si kwa kurekebisha bei za bidhaa?

Aidha, yapo malalamiko yanayohusu utendaji wa baadhi ya watendaji wa Mamlaka ya Mji Mkongwe na taasisi nyingine za Serikali.

Wafanyabiashara wanadai kuwa wanapojaribu kuwasilisha malalamiko au ushauri, hawasikilizwi ipasavyo.

Hali hii hujenga hisia kwamba maamuzi hufanywa bila ushirikishwaji wa wadau, jambo linalokwenda kinyume na misingi ya utawala bora.

Kumekuwapo pia madai ya matumizi ya nguvu kupita kiasi katika operesheni za ukaguzi na usimamizi wa biashara. Baadhi ya askari wanaodaiwa kuvaa mavazi yanayoficha nyuso wamehusishwa na vitendo vya kupiga, kupora au kuwanyanyasa wafanyabiashara.

Matukio kama hayo, endapo yanatokea, yanapaswa kuchunguzwa kwa uwazi na wahusika kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria. Ulinzi wa sheria haupaswi kuwa chanzo cha hofu au ukandamizaji.

Wakati huo huo, ZFCC ina wajibu mpana zaidi ya kusimamia bei elekezi pekee. Inapaswa pia kuimarisha udhibiti wa uuzaji wa vyakula visivyo salama au dawa zilizokwisha muda wa matumizi. Wanaojihusisha na vitendo vinavyohatarisha maisha ya wananchi kwa manufaa ya kibiashara wanastahili kuchukuliwa hatua kali za kisheria. Kulinda afya ya umma ni jukumu lisilohitaji mzaha.

Kwa upande mwingine, ipo haja ya kuangalia ada na tozo zinazotozwa na taasisi za Serikali zisizo na ushindani. Baadhi ya taasisi huongeza ada bila mashauriano mapana na wadau au uwazi wa kutosha.

Mfano uliotajwa mara kwa mara ni mabadiliko ya mfumo wa namba za vyombo vya moto, ambapo gharama mpya zimeonekana kuwa kubwa ikilinganishwa na makadirio ya gharama halisi za uzalishaji.

Hoja hapa si kupinga mabadiliko, bali ni kutaka uwiano kati ya gharama na tozo halisi. Vilevile, malalamiko yapo kuhusu adhabu za kuegesha magari katika maeneo yasiyo na alama za wazi za marufuku.

Baadhi ya madereva hudai kutozwa faini au kufungwa minyororo bila maelezo ya kutosha, hali inayosababisha usumbufu wa muda na fedha.

Hata katika mazingira ya dharura, kama kumpeleka mgonjwa au kusimama kwa muda mfupi, malalamiko yanaonyesha kukosekana kwa unyumbufu unaozingatia utu.

Ushindani wa haki ni msingi wa uchumi imara. Hata hivyo, usawa huo unapaswa kuonekana kwa pande zote, kwa wafanyabiashara na kwa taasisi za umma.

Serikali na vyombo vyake vinapaswa kuepuka taswira ya kutumia mamlaka bila kuwajibika, huku vikisisitiza nidhamu kwa sekta binafsi. Ulinzi wa walaji ni muhimu, lakini nao uende sambamba na mazingira rafiki na ya haki kwa wafanyabiashara.

Mwisho wa yote, suluhu ya kudumu ipo katika uwazi, ushirikishwaji wa wadau na utekelezaji wa sheria kwa haki bila upendeleo. Hapo ndipo malengo ya kulinda walaji na kukuza biashara yatakapokutana kwa manufaa ya jamii nzima.