Dar es Salaam. Wakati mageuzi ya sekta ya elimu yakishika kasi nchini, Serikali imeitaka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mitaala iliyoboreshwa ili kuhakikisha mabadiliko hayo hayaishii kwenye sera pekee, bali yanaonekana darasani.
Wito huo umetolewa leo Jumatano, Februari 4, 2026 na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, alipofanya ziara yake ya kwanza katika taasisi hiyo tangu ateuliwe kushika wadhifa huo.
Akizungumza na menejimenti na watumishi wa taasisi hiyo, Wanu amesema tathmini ya mara kwa mara ndiyo itakayobaini mapungufu na kutoa nafasi ya kufanya maboresho ya haraka kabla changamoto hazijaathiri ubora wa elimu.
“Nashukuru kwa taarifa yenu ya utekelezaji wa majukumu mbalimbali ambayo inatoa picha halisi ya kazi kubwa inayofanywa na taasisi hii. Hata hivyo, nawaomba muimarishe tathmini ya utekelezaji wa mitaala iliyoboreshwa ili changamoto zozote zibainike mapema na kufanyiwa kazi kwa haraka,” amesema.
Mbali na hilo, ameipongeza TET kwa kuendelea kuwekeza katika matumizi ya teknolojia ya kidijitali kusogeza huduma za elimu karibu na walimu na wanafunzi, akisema hatua hiyo ni mwelekeo sahihi wa mageuzi ya elimu ya kisasa.
“Nimefurahishwa kuona TET inavyoendelea kutumia teknolojia katika kusogeza huduma za elimu karibu zaidi na walimu na wanafunzi. Hatua hii inaongeza ufanisi, inapunguza gharama na kupanua wigo wa upatikanaji wa elimu bora, hasa katika maeneo ya mbali yenye changamoto za miundombinu,” amesema.
Amesisitiza kuwa mageuzi ya mitaala hayatakuwa na maana iwapo walimu, wasimamizi wa elimu na wadau hawatayatumia kikamilifu majukwaa ya kidijitali yaliyoandaliwa kusaidia utekelezaji wake.
Hata hivyo, amekiri kuwepo kwa changamoto zinazoikabili sekta hiyo, zikiwemo udhaifu wa miundombinu ya Tehama, upungufu wa mitambo ya uchapaji, uhaba wa wataalamu katika baadhi ya masomo na gharama za vifurushi vya intaneti.
Amesema Serikali inazitambua changamoto hizo na itaendelea kushirikiana na wadau wa elimu, sekta binafsi, taasisi za utafiti na washirika wa maendeleo ili kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma, akitaka fedha zinazotolewa zitumike kwa ufanisi na kwa kuzingatia malengo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk Aneth Komba, amesema taasisi hiyo kwa kushirikiana na wadau inaendelea kufanya tafiti mbalimbali zitakazosaidia kuboresha ufundishaji na ujifunzaji.
Dk Komba ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutenga fedha kwa wakati kwa ajili ya uandishi, uchapaji na usambazaji wa vitabu vya mitaala iliyoboreshwa katika shule zote nchini, na kuahidi taasisi hiyo itaendelea kusimamia majukumu yake kwa weledi na ubunifu zaidi.