Dar es Salaam. Jumla ya chupa 1,795 za dawa tiba zenye asili ya kulevya zimekamatwa zikiwa zimefichwa ndani ya basi la abiria linalofanya safari zake kati ya Tanzania, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kukamatwa kwa dawa hizo ni matokeo ya operesheni iliyofanywa kwa ushirikiano kati ya maofisa wa forodha katika mpaka wa Mtukula na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) iliyobaini uwepo wa boksi 105 za Pethidine zenye chupa 1,045, boksi 31 za Morphine Sulphate zenye chupa 310 na boksi 44 za Fentanyl zenye chupa 440.
Dawa hizo zilikamatwa katika basi la Kampuni ya SR Classic kutoka DRC, linalofanya safari zake kati ya Uganda, Tanzania na DRC, wakati likiingia nchini kupitia mpaka wa Mutukula.
Kamishna Jeneralia wa DCEA, Aretas Lyimo akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumatano Machi, 4 2026, amesema kiwango hiko ni kikubwa zaidi kukamatwa katika miaka ya karibuni.
Amesema inaonekana dawa hizo zinatumika kama mbadala wa dawa za kulevya za viwandani hususani heroin.
Sehemu ya shehena ya bangi aina ya skanka iliyokamatwa Januari na Februari, 2026.
“Dawa hizi zipo kwenye kundi la afyuni (opioids) ambazo hutumika hospitalini kwa ajili ya kupunguza maumivu makali kwa wagonjwa wa upasuaji, saratani, ajali na selimundu.
“Zinapoingia mikononi mwa watu wasiostahili, hugeuka kuwa dawa za kulevya zenye uwezo mkubwa wa kusababisha uraibu na hata vifo kutokana na kuathiri mfumo wa fahamu, upumuaji na mapigo ya moyo,” amesema Lyimo.
Aidha, watu saba wamekamatwa wakituhumiwa kuhusika na dawa hizo ambazo kisheria zinadhibitiwa chini ya Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya pamoja na Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba.
Hata hivyo, uingizaji na usambazaji wa dawa za nakotiki nchini unaruhusiwa kufanywa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) pekee.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema mamlaka hiyo itaendelea kupambana na wafanyabiashara haramu wa dawa za kulevya pamoja na dawa tiba zenye asili ya kulevya ili khakikisha hazichepushwi na zinawafikia wagonjwa wanaohitaji dawa hizo badala ya kutumiwa na wahalifu kama mbadala wa dawa za kulevya.
Kwa nini dawa hizi ni hatari
Ingawa dawa hizo ni muhimu katika kupunguza maumivu makali kwa wagonjwa wa saratani, ajali au wanaofanyiwa upasuaji, wataalamu wa afya wanaonya matumizi yake yasiyo sahihi yanaweza kugeuka kuwa tishio kwa maisha ya binadamu.
Akizungumza na Mwananchi, daktari wa usingizi na tiba ya maumivu, Richard Mhando amesema dawa hizo zipo kwenye kundi la opioids na hufanya kazi kwa kuathiri moja kwa moja mfumo wa fahamu.
“Opioids hupunguza maumivu kwa kuingilia namna ubongo unavyopokea taarifa za maumivu. Tatizo linakuja pale zinapotumika bila uangalizi wa daktari, kwani zinaweza kusababisha utegemezi wa haraka sana,” amesema.
Dk Mhando amesema Fentanyl ni miongoni mwa dawa zenye nguvu zaidi katika kundi hilo.
“Ni kali mara kadhaa zaidi ya morphine. Dozi ndogo tu ikitumika vibaya inaweza kushusha pumzi kwa kasi na kusababisha kifo.”
Akizungumzia athari za muda mfupi, mtaalamu wa afya ya akili, Rehema Lusekelo amesema watumiaji wa dawa hizo bila usimamizi huanza kwa kupata hali ya utulivu au furaha ya muda mfupi.
“Hisia hii huwafanya wengi kuzirudia. Kadri mwili unavyozoea, mtu huhitaji kiwango kikubwa zaidi ili kupata athari ileile. Hapo ndipo utegemezi na uraibu huanza.
“Opioids hushusha kasi ya kupumua. Wakati mwingine tunampokea mgonjwa akiwa anapumua kwa shida sana au pumzi imesimama kabisa. Bila huduma ya haraka, kifo kinaweza kutokea ndani ya dakika chache,” amesema.
Amesema mbali na kupumua, dawa hizo pia huathiri moyo na mfumo wa mmeng’enyo wa chakula.
Mtaalamu wa dawa (famasia), Elias Bugano amesema dawa hizo
zimedhibitiwa kisheria kwa sababu maalumu.
“Ni dawa za kitabibu zinazotakiwa kusimamiwa kwa umakini mkubwa. Zikitoka kwenye mnyororo rasmi wa usambazaji, zinaweza kuleta madhara makubwa kwa jamii,” amesema Bugano.
Licha ya juhudi mbalimbali zinazoendelea kufanyika kudhibiti mihadarati, bangi aina ya skanka imeendelea kusumbua nchini, katika operesheni zilizofanyika katika kipindi cha Januari na Februari kiasi kikubwa cha skanka kimekamatwa.
Jontwa Samwel Mwaikonyole (43) mkazi wa Gogoni Kibamba, alikamatwa akiwa na kilogramu 81.883 za skanka zikiwa ndani ya gari aina ya Scania lenye namba za usajili wa Afrika ya Kusini CAA 129054 na trailer namba CAA 22911 lililokuwa limebeba matunda aina ya tufaa. (Apple).
Eneo la Chanika Buyuni watuhumiwa Masudi Rajabu (38) na mwenzake Shafii Mohamed (30) walikamatwa wakiwa na kilogramu 488.64 za skanka.
Aidha, katika ukaguzi wa mabasi ya abiria jijini Mbeya, watuhumiwa sita walikamatwa kwa nyakati tofauti wakisafirisha bangi aina ya skanka.
Aina mbalimbali ya dawa tiba zenye asili ya kulevya zilizokamatwa kwenye basi la abiria linalofanya safari zake kati ya Tanzania, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Watuhumia hao ni Lenard Paulo (21) mkazi wa Sirali Mara, alikamatwa na kilogramu 46.46, Maria Kandonga (18) na wenzake Monica Kandonga (41) na Ibrahim Mwakibete (26) wote wakazi wa Mbeya, walikamatwa wakiwa na kilogramu 9.68, mtuhumiwa Joseph Mkwala (30) raia wa Malawi alikamatwa na kilogramu 4.62 na Esther Mbise (22) mkazi wa Mbeya alikamatwa na kilogramu 16.1 za skanka.
Mkoani Arusha, watuhumiwa Fatuma Mussa Mohamed (45) maarufu kwa jina la Mama Arapha na mwenzake Elibaraka Martin Kingu (29) maarufu kwa jina Baraka walikamatwa wakiwa na bunda 937 za mirungi zenye uzito wa kilogramu 363.45.
“Mama Arapha ni mhalifu wa muda mrefu aliyekuwa akiendesha mitandao ya safirishaji wa mirungi.
Vilevile, katika operesheni zilizofanyika mikoa ya Tabora, Tanga, Arusha, Mwanza, Shinyanga, Katavi, Mtwara, Mara, Morogoro, Kigoma, Ruvuma na Kilimanjaro zilikamatwa tani 5.24 za dawa za kulevya aina ya bangi, tani 4.04 za mirungi pamoia na gramu 72 za heroin.