Unguja. Hatimaye sintofahamu kati ya Serikali na wananchi wa nyumba za Kikwajuni imefikia tamati baada ya pande zote kukubaliana kupisha eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa nyumba za kisasa.
Februari 4, 2026, Mwananchi liliripoti mvutano huo uliotokana na hofu ya wananchi kuondolewa bila uhakika wa kurejea baada ya mradi kukamilika. Mradi huo wa miaka miwili utagharimu dola za Marekani milioni 45 (Sh115.425 bilioni) na utahusisha ujenzi wa nyumba 1,095 za ghorofa nne na tano.
Katika eneo hilo kuna nyumba 158 zilizojengwa mwaka 1969, ambapo 59 zinamilikiwa na wananchi na nyingine zipo chini ya Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC). Serikali imetenga Sh1.8 bilioni kwa ajili ya malipo ya kujikimu kwa wakazi watakaohama kwa kipindi cha miaka miwili ya utekelezaji wa mradi.
Sehemu ya majumba ya Kikwajuni ambayo yatabomolewa na kujengwa nyumba za kisasa katika eneo hilo
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Zanzibar, Rahma Kassim Ali, amesema makubaliano yamefikiwa na wote wenye nyumba na wapangaji watalipwa fedha za kujikimu na kurejeshwa baada ya mradi kukamilika. Wenye nyumba watarudishiwa makazi yao, huku wapangaji wakipewa kipaumbele kupanga upya kulingana na uwezo wao.
Katibu wa kamati ya wananchi, Omar Nassor Suleiman, amesema asilimia 99 ya wenye nyaraka wamehakikishiwa kurejea, huku wasiokuwa na nyaraka wakiahidiwa kupewa kipaumbele, ingawa si kwa maandishi. Wananchi wengi tayari wamesaini mikataba na kupokea malipo.
Kwa mujibu wa utaratibu wa malipo, chumba kimoja hulipwa Sh150,000 kwa mwezi, viwili Sh300,000 na vitatu Sh450,000. Kwa nyumba zenye vyumba vinne, wastani wa malipo kwa miaka miwili ni Sh14.8 milioni, vyumba vitatu Sh10.6 milioni na viwili Sh7.6 milioni.
Mkuu wa ZHC, Sultan Said Suleiman, amesema ujenzi utaanza Machi mwaka huu na utahusisha pia maduka, eneo la biashara na msikiti mkubwa.