SMZ kununua mafuta lita milioni 100 kukabiliana na athari za vita 

Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetangaza mipango ya kununua takriban lita milioni 100 za mafuta kwa lengo la kuzihifadhi kama akiba ya kitaifa kutokana na mzozo wa kijeshi unaoendelea kati ya Iran, Marekani na Israel, ambao umeleta hofu ya ongezeko la bei kwenye soko la dunia.

Hatua hii imechukuliwa huku mataifa mengi yakishughulikia ugumu unaotabiriwa wa usambazaji wa mafuta na ongezeko la bei ya bidhaa hizo.

SMZ imesema akiba ya miezi mitatu itasaidia kulinda uchumi wa visiwa na kuhakikisha upatikanaji wa mafuta kwa huduma za msingi haukatiki endapo mgogoro huo wa kimataifa utaendelea au kusababisha upungufu wa petroli na dizeli.

Imesema, ingawa meli za nje za mafuta zimezuiwa zisitoke, bado Serikali inafanya mazungumzo na mataifa jirani kuhakikisha mafuta yanapatikana na kuhifadhiwa Tanga pamoja na Dar es Salaam.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Machi 4, 2026 na Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Nadir Abdullatif katika mkutano na waandishi wa habari wa kuelezea mafanikio ya siku 100 za Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi. 

“Zanzibar haitaathirika na vita vinavyoendelea kwa sasa hususani katika suala la mafuta kwani Serikali imejipanga kununua lita milioni 100 na kutumika katika kipindi cha miezi mitatu ijayo,” amesema Nadir.

Pia, Waziri huyo amesema mafuta yaliyopo yana uwezo wa kutosha hadi kufikia kipindi cha Sikukuu ya Idd El fitri na ndio maana wameamua kutafuta njia mbadala za kuhakikisha Zanzibar haitakuwa miongoni mwa watakaoathirika na vita hivyo.

Hivyo, amewataka wananchi wasiwe na hofu juu ya hilo kwa kuwa mafuta yatakuwepo, ila bei haitakuwa kama ilivyo wakati huu kwa sababu hata duniani imepanda.

Akitoa ufafanuzi wa namna ya kukubaliana na hilo amesema, kila mwezi Zanzibar inatumia mafuta lita milioni 18 hadi 20 kwa mwezi, hivyo lita milioni 100 zitatosha kuwafikisha kwa miezi mitatu hadi hali itakapotulia.

Amesema, Licha ya kununua mafuta nje, bado wizara itahakikisha inatumia kwa umakini mafuta ya ndani, ili kuwafanya wananchi waendelee na shughuli zao za kawaida.

Katika hatua nyengine, wizara hiyo imesema imewekeza Sh800 bilioni katika kutengeneza miundombinu ya umeme Zanzibar na tayari imeshapokea vifaa kafhaa, zikiwemo transfoma nne.

Hata hivyo, Wizara hiyo imeomba radhi kwa wananchi juu ya changamoto wanazozipitia ikisema chanzo ni miundombinu chakavu.

Pia, amesema umeme uliopo ni megawati 135 na kuna upungufu wa megawati 65 za umeme zilizosababishwa na uwepo wa miradi mikubwa iliyojengwa kwa kipindi kifupi jambo lililochangia kuongezeka kwa matumizi ya umeme.

Amesema Wizara kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco) imefanya matengenezo ya majenereta 30 ili kutoa huduma kwa wananchi.

Ameeleza, Wizara inatambua shida wanayopitia wananchi katika suala la umeme na Serikali imeingia makubaliano na mikataba mikubwa ili kumalizika tatizo mwaka 2028.

NNaye aibu Waziri wizara hiyo,  Seif Kombo Pandu amesema Serikali imetenga Sh14 bilioni kutatua changamoto ya maji kisiwani hapa.

Pia, amesema wizara hiyo imezindua mfumo wa maji utakaosaidia kutambua uharibifu wa miundombinu na kupima kiwango cha maji na uhitaji wake.

Amesema Wizara kupitia mradi wa Exim Bank umeunganishia maji nyumba 4,730 kisiwani Pemba na 10,000 kwa Mkoa wa Kaskazini Unguja.