UCHAMBUZI WA DANIEL MJEMA: Balozi Nchimbi alivyoanzisha safari ya maridhiano kiana

Ukimsikiliza Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi alipokuwa akizungumza katika Misa Takatifu ya mazishi ya Mwadhama Polucarp Kardinali Pengo, unaweza kudhani ni maneno ya kisiasa, lakini ukweli ameanzisha safari ya maridhiano.

Alichokisema Balozi Nchimbi ni nadra sana kusikia kutoka kwa makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao ni wahafidhina (conservatives) ambao hawataki mabadiliko na wanachukulia upinzani kama uadui au ni dhambi kuwa mpinzani.

Ni kama vile waliukubali mfumo wa vyama vingi vya siasa kwa shingo upande lakini kauli ya Balozi Nchimbi huenda ikafungua ukurasa mpya kwamba hakuna chama au kiongozi mwenye hati miliki ya Tanzania, bali ni watanzania wenyewe.

Ukisoma Ibara ya 3(1) ya Katiba inasema Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa na ili uingie katika uongozi ndani ya vyombo vya Dola, maana yake lazima udhaminiwe na chama cha siasa.

Licha ya Katiba yetu hii ya mwaka 1977 na sheria nyingine za nchi ikiwamo Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2019 kutambua uhalali wa vyama vya upinzani, wapo wahafidhina ndani ya CCM wanachukulia upinzani kama ni uadui fulani.

Ndio maana nimetangulia kusema kauli ya Balozi Nchimbi ni kama ameanzisha safari ya maridhiano kutokana na taifa letu kugawanyika vipande vipande na kuibuka kwa chuki na moja ya sababu ni dhana kuwa upinzani unakandamizwa.

Inawezekana, nasema inawezekana, hata ghasia zile za siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 29,2025, zinaweza kuwa pamoja na mambo mengine, zilichochewa na chuki za vijana wanaoona vyama vya upinzani havipewi fursa sawa na Serikali.

Siku hiyo ya Misa Takatifu ya mazishi ya Kardinali Pengo, Balozi Nchimbi aliwataka watanzania kujua kwamba katika nchi hii kila mtu ana nafasi na wajibu wa kuitumikia na kwamba katika utumishi wa nchi, watu wasitegeane.

Akasema kila mtu aitumikie nchi yake kwa nguvu zake zote na kusema “Nimekuwa nikiyasema haya mara nyingi hata mambo ya kugombana kivyama vyama mie siyapendi sana ni ujinga tu. Nchi yenu moja, nchi yenu wote mnagombana nini?”.

Akaongeza kusema “mtakuwa mashahidi hata nilipokuwa Katibu mkuu wa CCM, nikisikia mwana CCM ameongea maneno ya hovyo dhidi ya mpinzani nilikuwa nakemea mara moja kwa sababu ni ujinga tu”, na akaweka msisitizo kuwa:-

“Kwa sababu vyama vya siasa navyo vimeundwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi. Mtu anapojiunga  na chama kingine maana yake naye anataka kutumikia nchi yake kwa njia nyingine lakini utumishi ni utumishi,”mwisho wa kumnukuu.

Nimetangulia kusema ni kama Balozi Nchimbi ameanzisha safari ya maridhiano kwa sababu kama wakubwa wengine ndani ya CCM wakiimba wimbo kama wa Balozi Nchimbi, nina uhakika maridhiano ni jambo linalowezekana kabisa.

Huko tulipotoka na tulipo, tunashuhudia mpasuko mkubwa ambao hauwezi kutuacha salama na kila mtu ni shahidi wa chaguzi zinavyofanyika na kuacha makovu yanayosababishwa na majeraha ambayo uponyaji wake ni mgumu.

Ningekuwa na mamlaka na ikiwa kama sehemu ya kuuandaa umma na maridhiano baada ya ripoti ya Jaji Chande kutolewa, ningefuta kesi zote zenye sura ya kisiasa kama ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Tundu Antipasi Lissu.

Kama alivyosema Balozi Nchimbi, vyama vya upinzani vimeundwa kupitia ibara ile ya 3(1) ya Katiba yetu inayotambua uwepo wa mfumo wa vyama vingi vya siasa, hivyo yeyote anayechaguliwa, awe CCM au upinzani, ni mtanzania mwenzetu.

Lakini katika kampeni za uchaguzi mkuu 2015 na 2020 tulisikia wanasiasa wenye majina makubwa tu wakihubiri siasa za chuki kuwa endapo wananchi wangechagua wagombea wa upinzani Serikali ya CCM isingewaletea maendeleo.

Yaani ni kama mtanzania akitumia haki yake ya kikatiba kuwa upinzani ili awatumikie watanzania kupitia njia tofauti na CCM anachukuliwa kama ni adui na ndio maana nasema tukienda na msimamo wa Balozi Nchimbi tutalitibu hili taifa.

Ukisoma Ibara ya 13 ya Katiba yetu inasema watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria na ni marufuku kutungwa kwa sheria itakayoleta ubaguzi wa Kiitikadi.

Ukienda ndani zaidi ukasoma Ibara ndogo ya 4 inasema ni marufuku kwa mtu yeyote kubaguliwa na mtu au mamlaka inayotekeleza madaraka yake chini ya sheria au katika utekelezaji wa kazi au shughuli yoyote ya Mamlaka ya Nchi.

Ibara ndogo ya 5 imefafanua vizuri sana neno ubaguzi kuwa  maana yake ni kutimiza haja, haki au mahitaji mengineyo kwa watu mbalimbali kwa kuzingatia utaifa wao, kabila, pahala walipotokea, maoni yao ya kisiasa, rangi, dini au jinsia.

Kama alivyosema Balozi Nchimbi ambaye naungana naye kwa asilimia 100, vyombo vyetu kama Polisi na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), vitoe uwanja sawa kwa vyama vya siasa kwani kila mmoja ana haki ya kuitumikia nchi yake.

Ninafahamu, safari ya maridhiano ambayo itaanzishwa baada ya ripoti ya Tume ya Jaji Chande, itagusia maeneo mengine kama utekaji na kupotea kwa watu na vurugu zile za Oktoba 29, lakini tuanze na ushauri huu rahisi wa Balozi Nchimbi.

Daniel Mjema ni mwandishi wa habari na mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Anapatikana kwenye namba 0656600900