Dar es Salaam. Miaka ya hivi karibuni, kumeibuka changamoto inayolalamikiwa na watumiaji wengi wa barabara ya ongezeko la vyombo vya moto vinavyowekewa taa kali kupita kiwango, kwa madai ya urembo au kuongeza mwanga.
Hata hivyo, licha ya maelezo hayo, baadhi ya madereva wanadai mwanga huo umekuwa chanzo kipya cha ajali, hususan nyakati za usiku ambako umakini wa dereva hutegemea zaidi uwezo wa kuona kwa uwazi.
Barabara kuu, za pembezoni mwa miji, pamoja na zile zinazoelekea mikoani na nchi jirani, licha ya umuhimu wake kiuchumi na kijamii, zimekumbwa na kadhia hiyo ya taa kali zisizo na viwango, huku baadhi ya madereva wakiongeza taa za ziada mbele ya magari yao au kubadilisha kabisa mfumo wa taa za kiwandani.
Madereva wa pikipiki, bajaji, magari madogo na malori wamesema mwanga huo mkali unapunguza uwezo wa kuona kwa sekunde kadhaa wanapokutana uso kwa uso na vyombo hivyo.
Wanaeleza sekunde hizo chache za kupoteza umakini zinaweza kusababisha kugongana, kutoka nje ya barabara au kupoteza mwelekeo, hususan katika barabara za masafa marefu zenye mwendo kasi ambako magari hukutana kwa kasi kubwa.
Mwananchi imebaini tabia ya baadhi ya wamiliki wa vyombo vya moto kubadilisha taa za kawaida na kuweka kali aina ya LED zisizo na viwango, imeongezeka si tu katika maeneo ya mijini, bali pia katika barabara za masafa marefu na zile zinazoelekea mipakani.
Wapo wanaofunga taa za ziada bila kuzingatia miongozo ya kiusalama, hali inayoongeza ukali wa mwanga kwa watumiaji wengine wa barabara.
Katika mazingira hayo, makundi mbalimbali ya madereva yameanza kutoa malalamiko yao hadharani, wakisisitiza kuwa, mwanga mkali usiozingatia viwango umeongeza hatari ya ajali katika safari za usiku na unahitaji kudhibitiwa kwa nguvu ya sheria.
Dereva wa pikipiki Tabata, Charles Kalungu amesema wamekuwa waathirika wakubwa kwa sababu hawana kinga kama ilivyo kwa magari.
“Unapokutana na gari lina taa kali sana, macho yanakuwa kama yamefunikwa ukungu kwa pikipiki, sekunde moja tu ya kupoteza umakini inaweza kukuangusha,” amesema Kalungu.
Amesema hata madereva wenzao wa pikipiki wamekuwa wakiweka taa za aina hiyo ikiwemo zile za urembo wa rangi wengine wakiweka za taa za magari.
Dereva wa bajaji wa kituo cha Ubungo, Karim Seseme amesema hali ni mbaya zaidi katika makutano yenye mwanga hafifu au wanapokuwa wanakatiza barabara kuu.
“Taa zinapokuwa kali kupita kiasi na hazishushwi, unajikuta unafumba macho au kupunguza mwendo ghafla, hapo unaweza kusababisha ajali,” amesema Seseme.
Kwa upande wa magari madogo, baadhi wanakiri kuweka taa kali kwa madai ya kuongeza uwezo wa kuona mbali barabarani, hasa wanaposafiri safari ndefu kama ya kuelekea mikoani. Hata hivyo, wenzao wanapinga wakisema hatua hiyo inawaumiza watumiaji wengine.
“Unaweza kuona vizuri, lakini dereva anayekuja upande wa pili anapata shida usalama ni wa wote na hii inatupa wakati mgumu barabarani hususani kwa barabara nyembamba,” amesema dereva wa teksi Majid Masoud.
Pia, amesema kwa safari za mikoani zinawasaidia kutokana na ugeni wa barabara, kwani wapo wanaowafanyia makusudi kwa kumulika taa kali.
Pius Isaya dereva wa lori anayesafirisha mizigo kuelekea mikoa ya Kaskazini, na nchi jirani amesema ni hatari zaidi katika barabara kuu zenye magari mengi ya masafa marefu.
“Ukikutana na gari lina taa kali au za urembo unapoteza umakini kwa sekunde kadhaa na kwa lori lenye mzigo mzito, huwezi kusimama ghafla. Hapo ndipo ajali kubwa hutokea,” amesema Isaya.
Chama cha madereva wa malori
Akizungumza na Mwananchi Machi mosi, 2026, Katibu wa Chama cha Madereva wa Malori Tanzania, Muhidini Sangoti amesema moja ya changamoto kubwa inayochangia ajali barabarani ni matumizi ya taa zisizokubalika kisheria kwenye baadhi ya magari.
Amesema baadhi ya madereva wamekuwa wakiongeza taa za ziada zisizo na viwango, zikiwamo taa kali za rangi mbalimbali au taa nyingi nyuma ya gari, jambo linalowachanganya madereva wanaokuwa nyuma yao.
“Kuna taa maalumu za kiwanda ambazo zinaashiria breki, kusimama au kukata kushoto na kulia lakini sasa wengine wameweka taa nyingi zisizoeleweka, dereva wa nyuma anashindwa kujua ipi ni ishara sahihi,” amesema Sangoti.
Ametolea mfano wa tukio la hivi karibuni lililotokea eneo la Mikumi mkoani Morogoro, dereva mmoja alipata ajali baada ya kuchanganywa na mwanga mkali na taa nyingi zilizokuwa zimewekwa kwenye gari lililokuwa mbele yake.
“Gari ya mbele yake iliwasha mataa mengi ambayo hayana maana kwenye gari, hivyo dereva wa lori alijikuta amefunga breki ghafla na kusababisha ajali.”
Baada ya tukio hilo, amesema chama hicho kilishirikiana na Jeshi la Polisi kumkamata dereva husika na kuchukuliwa hatua za kisheria, ikiwamo kunyang’anywa leseni.
Kutokana na hali hiyo, Sangoti amesema chama hicho tayari kimekaa kikao na Kamanda wa Polisi Kikosi cha Barabarani Mkoa wa Pwani kujadili namna ya kudhibiti changamoto hizo kwa sababu mkoa huo ni lango kuu la magari yanayoingia Dar es Salaam kutoka mikoa mingine na hata nje ya nchi.
“Tumekubaliana kufanya operesheni maalumu kuanzia Machi 3 hadi 5 mwaka huu, tukishirikiana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani lengo ni kudhibiti hizo taa ambazo zimewekwa bila kufuata taratibu na kuimarisha usalama barabarani,” amesema Sangoti.
Amesema kabla ya operesheni hiyo, chama kitapitia makundi sogozi ya madereva na kutoa matangazo ya uelimishaji ili kila dereva awe na taarifa sahihi kuhusu sheria na wajibu wake.
Kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168 (R.E. 2002), ni kosa kwa mmiliki au dereva wa chombo cha moto kufunga au kutumia taa zisizo na viwango vilivyowekwa kisheria, pamoja na vimulimuli au ving’ora bila kibali maalum kutoka mamlaka husika.
Sheria hiyo pia inapiga marufuku matumizi ya taa za rangi maalumu kama bluu au nyekundu kwa vyombo visivyo vya dharura, huku ikisisitiza kila chombo cha moto kinapaswa kuwa na vifaa vinavyokidhi matakwa ya kiusalama bila kuathiri watumiaji wengine wa barabara.
Akizungumza na Mwananchi Machi mosi, 2026, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, William Mkonda amesema operesheni maalumu zinaendelea katika barabara sambambana uelimishaji endelevu.
Amesema sheria ipo wazi na wanaendelea na usimamizi na vitendo vyote vya kuikwaji wa sheria za usalama barabarani vinachukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
Kwa sasa, operesheni hizo zinawalenga walioongeza taa kinyume cha sheria, waliofunga ving’ora na vimulimuli pasipo kuzingatia taratibu, pamoja na wanaotumia namba zisizotambulika na mamlaka za usajili na makosa mengine hatarishi na kero kwa watumiaji wengin wa barabara.
“Sheria ipo wazi na tutaendelea na usimamizi wa sheria kwa kufanya operesheni endelevu, sambamba na uelimishaji endelevu. Aidha, vitendo vyote vya ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani vinachukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria,” amesema Mkonda.
“Usimamizi wa sheria na uelimishaji ni masuala endelevu katika kuhakikisha barabara zinaendelea kuwa salama, watumiaji wote wa barabara wakijengewa uwezo vyema juu ya sheria, kanuni na taratibu za matumizi bora na salama ya barabara, basi barabarani kutaendelea kuwa sehemu salama kwetu sote,”amesema Mkonda.
Mkonda amesema kwa wale wachache ambao kwao kutii sheria wanahitaji shuruti, watashurutishwa kwa kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria.