Viwanda Mkoani Pwani Vyatakiwa Kuboresha Mazingira ya Kazi

Global Publishers
March 4, 2026
0 Comments


Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Rahma Kisuo, ameziagiza menejimenti za viwanda Mkoani Pwani kuboresha mazingira ya kazi na maslahi ya wafanyakazi ili kuwa na uzalishaji endelevu na wenye tija.

Ametoa agizo hilo katika ziara yake ya kufuatilia utekelezaji wa sheria mbalimbali za kazi ikiwemo Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 katika maeneo mbalimbali ya kazi Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani. Akizungumza kwa nyakati tofauti katika viwanda vilivyotembelewa, Naibu Waziri Kisuo amesema pamoja na viwanda hivyo kufanya kazi nzuri ya uzalishaji na kutekeleza sheria za kazi, ziara yake imabaini dosari ndogo ndogo zinazopaswa kurekebishwa na wahusika.


“Tumetembelea baadhi ya maeneo katika viwanda hivi na kujionea hali ilivyo. Kimsingi wanafanya vizuri japokuwa kuna kasoro chache tulizozibaini ikiwemo baadhi ya wafanyakazi kutokuwa na mikataba ya ajira pamoja na kutokidhi baadhi ya viwango vya
usalama na afya mahali pa kazi,” amesema Naibu Waziri Kisuo.

Amewaagiza watendaji kutoka Ofisi yake na Mamlaka nyingine za udhibiti, kutenga muda maalum wa kufanya ukaguzi wa kina katika viwanda hivyo ili kutoa ushauri stahiki wa maboresho yanayohitajika kwa wawekezaji.
Aidha, amewapongeza wamiliki wa viwanda husika kwa uzalishaji wenye mchango mkubwa katika uchumi wa nchi kupitia kodi inayolipwa serikalini pamoja na kuzalisha ajira nyingi kwa Watanzania.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda, ambaye aliambatana na Naibu Waziri katika ziara hiyo, ameeleza baadhi ya mapungufu yaliyobainika katika mifumo ya usalama na afya ya viwanda vilivyotembelewa ikiwa ni pamoja na mazingira ya kazi yenye joto kali, vumbi la makaa ya mawe kutapakaa katika mazingira, upungufu wa vifaa kinga na ukosefu wa alama za
usalama.
Amemhakikishia Naibu Waziri kuwa watalaam wake watashirikiana na mamlaka nyingine kufanya ukaguzi wa kina ambao utawezesha wawekezaji kupata ushauri unaohitajika ili kuboresha mazingira yao ya uzalishaji.
Kwa upande wao, viongozi wa viwanda vilivyotembelewa akiwemo Bw. Jacob Lerise, Msimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala katika Kiwanda cha uundaji magari cha GF Vehicle Assemblies Ltd, wamemshukuru Naibu Waziri na watendaji wake na kuahidi kutekeleza maagizo mbalimbali yaliyotolewa katika ziara hiyo.

Ziara hiyo ya siku mbili Wilayani Kibaha Mkoani Pwani imefanyika katika kiwanda cha bidhaa za usafi cha Keds Tanzania Co. Ltd, Aluminium Trailers Ltd ambao ni waundaji wa trela za malori, kiwanda cha kuunda magari cha GF Vehicle Assemblies Ltd pamoja
kiwanda cha sabuni na vipodozi cha Creative Intertraders Ltd.