Wakulyamba, Nyamhanga, Shilogile waagwa kwa gwaride rasmi

Moshi. Jeshi la Polisi nchini limewaaga makamishna wake watatu wastaafu katika gwaride maalumu lililofanyika leo Machi 4, 2026, wenyewe wakijivunia kufanikisha operesheni kubwa ndani ya jeshi hilo.

Makamishna walioagwa ni aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba, pamoja na Makamishna Albert Nyamhanga na Faustine Shilogile.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Camillus Wambura, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, pamoja na wakuu wa jeshi wastaafu Simon Sirro na Omary Mahita.

Akizungumza baada ya gwaride, Kamishna Wakulyamba amesema moja ya mafanikio yake makubwa ilikuwa mwaka 2017 alipokuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, ambapo aliendesha operesheni ya mwezi mmoja kupambana na wahalifu wenye mrengo wa itikadi kali, akafanikiwa kukomesha vuguvugu hilo lililosababisha hofu miongoni mwa wananchi.

“Mwaka 2017 moja ya mambo ambayo nitayakumbuka sana maisha mwangu niliendesha operesheni ya mwezi mmoja nikiwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, dhidi ya wahalifu ambao walikuwa na mrengo wa itikadi kali nikafanikiwa kukomesha na kumaliza lile vuguvugu.

Amesema, “Nilikamata silaha tisa na watuhumiwa wawili ambao walikuwa wamebeba silaha ikiwemo SMG saba, pisto moja na gobore moja.Tukio hili tuliweza kulidhibiti ndani ya mwezi mmoja, baada ya kupata taarifa za mtawanyiko wao na kuanza kufuatilia tukishirikiana na makao makuu.Tulifuatilia maeneo yote ambayo walikuwa wamejikita na kufanikisha kudhibiti.”

Kamishna Wakulyamba amesema operesheni ile ilipelekea kupungua kwa matukio ya uhalifu katika mkoa huo ambao ulikuwa na matukio makubwa ya kiuhalifu.

Kwa upande wake, Kamishna Albert Nyamhanga amesema anajivunia kuondoka ndani ya Jeshi baada ya miaka 32 ya utumishi, akisisitiza kwamba kuzingatia misingi ya nidhamu, haki, weledi na uadilifu ndiyo nguzo ya mafanikio ndani ya Jeshi la Polisi.

Ameongeza kuwa, alishirikiana na viongozi wa juu kuunda mpango wa maboresho ya jeshi ambao unaendelea kutekelezwa hadi sasa.

“Kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya nidhamu, haki, weledi na uadilifu ndio msingi wa mafanikio ndani ya Jeshi kwa ujumla, misingi hii ndio imenifikisha mimi hapa nilipo, kufikia ngazi ya ukamishna sio kazi ndogo lakini kwa nyadhifa ambazo nimepewa kupitia cheo hicho na vyeo vingine, ni kutokana na kuaminika pamoja na kuzingatia misingi hiyo,”amesema Kamishna Nyamhanga

Amesema, “Ninachojivunia ni kwamba niliaminiwa na viongozi wa juu wa Serikali na wa Jeshi la Polisi, kazi walizokuwa wananipa tangu nikiwa na vyeo vya chini ilionyesha kwamba wananiamini na mimi nilionyesha imani hiyo kwa kufanya kazi mpaka hapa nilipofikia cheo cha Kamishna wa Polisi.”

Naye Kamishna Faustine Shilogile amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wananchi na Jeshi la Polisi, akisema unaleta uhusiano mzuri ndani ya jamii na kurahisisha kazi za ulinzi.

Pia amefanikisha kuhakikisha kila kata nchini inakuwa na polisi jamii, hatua ambayo anasema imezaa matunda kwa wananchi.

“Naomba wananchi waendelee kushirikiana na Jeshi la Polisi wao ndio wanawafahamu wahalifu na ndio wanaishi na wahalifu, mwananchi akitoa taarifa kazi inaweza kufanyika , ushirikiano ni muhimu sana,”amesema Kamishna mstaafu Shilogile.