Watuhumiwa 50 wakamatwa kwa tuhuma za wizi, kukutwa na nyara za Serikali

Dodoma. Polisi Mkoa wa Dodoma linawashikilia watuhumiwa 50 kwa makosa mbalimbali, yakiwemo ya wizi, udanganyifu, dawa za kulevya na kukutwa na nyara za Serikali.

Taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma iliyotolewa leo Jumatano, Machi 4, 2026, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Gallus Hyera, imesema watuhumiwa hao walikamatwa katika msako uliofanywa na jeshi hilo kuanzia Januari mosi  hadi Februari 28, mwaka huu.

Kamanda Hyera amesema jeshi hilo limeendelea kutekeleza majukumu yake ya kulinda raia na mali zao kwa kufanya misako na oparesheni mbalimbali, kuzuia na kupambana na uhalifu, ambapo jumla ya watuhumiwa 50 wamekamatwa kwa tuhuma za makosa mbalimbali.

Ameyataja makosa hayo kuwa ni kupatikana na dawa za kulevya aina ya bangi kilo 5, kete 25 na gramu 500, shambulio la kudhuru mwilini, wizi wa ng’ombe mmoja, kupatikana na gobole kinyume cha sheria, unyang’anyi kwa kutumia silaha, kujipatia fedha kwa udanganyifu na kupatikana na nyara za Serikali, nyama pori kilo tatu.

Amesema makosa mengine ni kupatikana na mazao ya msituni, gunia kumi za mkaa bila kuwa na kibali, kufanya biashara ya vileo baada ya muda, kucheza kamari bila kibali, uzembe na uzururaji pamoja na kupatikana na mali zinazodhaniwa kuwa za wizi ambazo ni runinga tano, jokofu moja na pikipiki nane, sita zikiwa zimesajiliwa na mbili hazina namba za usajili.

“Kikosi cha usalama barabarani kimefanikiwa kudhibiti ajali za barabarani kwa kukamata madereva kwa makosa mbalimbali na kuwafutia leseni pamoja na kuwatoza faini madereva tisa,” amesema.

Amesema kikosi hicho pia kimeendelea kutoa elimu ya matumizi salama ya barabara kwa watumiaji wake na kugawa vifaa vya kuongozea magari kwa wanafunzi wa shule za msingi ili kuwasaidia kuvuka wanapoenda na kutoka shuleni.

Kwa upande wa mafanikio ya kesi mahakamani, Kamanda Hyera amesema washtakiwa 58 wamehukumiwa vifungo mbalimbali kutokana na makosa mbalimbali.

‎Pia amesema jeshi hilo limefanikiwa kurejesha mali zilizofanikiwa kutambuliwa na wahusika baada ya kesi hizo kutolewa hukumu mahakamani. Mali hizo ni pamoja na runinga tatu, pikipiki, jokofu, nguo na mali nyingine nyingi.

Jeshi hilo wamewasisitiza waliopotelewa na mali kwenda kituo cha polisi kilichopo karibu na Hospitali ya Rufaa Dodoma kuzitambua mali zao ili wapatiwe, huku likiwahimiza wananchi kuendelea kufichua uhalifu na wahalifu ili kuhakikisha usalama, amani na utulivu unaimarika wakati wote.