WAZIRI MBARAWA ASISITIZA THAMANI YA FEDHA KATIKA UJENZI WA CHUO CHA USAFIRI WA ANGA WA BILIONI 78


 :::::::

Waziri wa Uchukuzi, Makame Mbarawa, ametoa maelekezo kwa wasimamizi wa mradi wa ujenzi wa Chuo cha Usafiri wa Anga kuhakikisha thamani ya ujenzi inaendana kikamilifu na fedha zilizotolewa na Serikali.

Akizungumza Machi 4, 2026 wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Profesa Mbarawa alisisitiza kuwa ni lazima kupatikane “value for money” katika utekelezaji wa mradi huo wa shilingi bilioni 78. 

Alieleza kuwa kila hatua ya ujenzi inapaswa kuzingatia michoro, usanifu na viwango vya kitaalamu vilivyokubaliwa ili kuhakikisha fedha za umma zinaleta matokeo yaliyokusudiwa.

Alisema mradi huo ni wa kimkakati na unakuja mara moja, hivyo hauhitaji uzembe wowote katika usimamizi wake. Alitoa wito kwa wasimamizi na wataalamu waliopo eneo la mradi kusimamia kwa karibu kazi ya mkandarasi ili kuhakikisha ubora unaendana na kiwango cha uwekezaji uliofanywa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hassal Msangi, alisema mradi huo ni wa kimkakati kwa Serikali na umeendelea vizuri tangu ulipoanza kutekelezwa Agosti mwaka jana baada ya kusainiwa kwa mkataba Julai 3. Alibainisha kuwa mkandarasi alipatikana kwa ushindani na ana uzoefu wa kutosha, huku akisimamiwa na mshauri wa mradi pamoja na meneja wa mradi mwenye taaluma ya uhandisi wa kiraia.

Naye Mkurugenzi wa Chuo cha Usafiri wa Anga Tanzania, Lisiji Kanji, alisema kukamilika kwa miundombinu hiyo kutaongeza uwezo wa chuo kupokea wanafunzi kutoka wastani wa 2,000–2,500 kwa mwaka hadi kufikia kati ya 5,000 na 7,000, hatua itakayosaidia kupunguza utegemezi wa kuwasomesha wataalamu nje ya nchi.