Ziara ya Dk Mwigulu yaweka hatarini ajira za watendaji mikoani

Dar es Salaam. Huenda ziara zilizofanywa na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, katika mikoa ya kaskazini zikaweka hatarini nafasi za baadhi ya watendaji serikalini kutokana na kubainika kwa kasoro za kiutendaji.

Katika ziara hiyo iliyoanzia Mkoa wa Tanga Februari 13, 2026, kisha Kilimanjaro, Arusha na Manyara, Dk Mwigulu aliwabananisha watendaji wa Serikali akitaka kupatiwa ufafanuzi wa kina kuhusu dosari alizozibaini au taarifa za usimamizi wa miradi.

Katika ziara hiyo, kwa nyakati tofauti, Dk Mwigulu alilazimika kuwachangisha fedha baadhi ya watendaji wa Serikali ili kumlipa mzabuni aliyetekeleza mradi kwa muda mrefu, lakini hakulipwa na halmashauri sehemu ya fedha iliyobaki.

Kupitia ziara hiyo, wananchi wa mikoa ya Tanga, Arusha, Manyara na Kilimanjaro walipata fursa ya kuwasilisha kero zilizopatiwa ufumbuzi wa papo hapo, huku nyingine Dk Mwigulu akiahidi kuzifanyia kazi kwa hatua zaidi.

Mbali na hilo, katika baadhi ya wilaya au maeneo ya mikoa aliyopita Dk Mwigulu, aliacha maagizo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza kwa kina matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo kwa kile alichokiita “kichaka cha gharama” kinachotumiwa kuhalalisha upotevu wa fedha za umma.


Aidha, Dk Mwigulu aliiagiza Takukuru kuchunguza utekelezaji wa miradi mbalimbali ili kubaini na kuwahoji baadhi ya watendaji wa Serikali.

Mbali na wakuu wa mikoa, wilaya, makatibu tawala wa mikoa na wilaya, pamoja na wakurugenzi ambao mamlaka yao ya uteuzi ni Rais, wapo pia baadhi ya wakuu wa idara ambao, kwa kushirikiana na wateule hao, wameonekana kuelemewa.

Miongoni mwa mambo yaliyoibuka katika ziara ya Dk Mwigulu aliyoifanya katika mikoa hiyo ni pamoja na ubadhirifu wa fedha za umma, uzembe wa watendaji na migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

Changamoto nyingine zilizojitokeza katika ziara hiyo ni pamoja na baadhi ya watendaji wa Serikali kulumbana (wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wakuu wa idara), miradi kutokamilika kwa wakati ilhali Serikali imeshatoa fedha, na migogoro ya ardhi.

Wakati hayo yakijiri, baadhi ya wachambuzi wa siasa wanasema ni wakati mwafaka kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kutumia kalamu yake ili kuchukua hatua kwa watumishi na watendaji wa Serikali waliobainishwa na Dk Mwigulu.

Lakini wachambuzi wengine wamekwenda mbali zaidi, wakihoji uwepo wa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wanaoshindwa kutatua au kushughulikia baadhi ya kero zilizo ndani ya uwezo wao hadi Waziri Mkuu afike.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa George Kahangwa, anasema inasikitisha kuona kuwa baada ya miaka mingi ya uhuru bado kuna mambo ya ajabu yanayodaiwa kufanyika na watumishi wa umma.

Hata hivyo, Profesa Kahangwa anasema kilichofanywa na Dk Mwigulu ni sahihi kwa sababu anafuatilia kazi za Serikali, lakini si lazima viongozi wanapotekeleza wajibu huo wakute madudu katika halmashauri husika, bali wakute kazi nzuri ikiendelea.

“Nadhani anapoibua jambo moja mahali fulani, basi lipige kelele nchi nzima. Mfano, kama kuna mwananchi ameonewa haki zake, Dk Mwigulu anapotatua hilo hadharani, basi ujumbe ufike kila mahali.

“Lakini mambo kama haya tunajiuliza, wakuu wa mikoa huwa wanafanya nini kwa haya yanayotokea katika maeneo yao wakati wapo? Wakuu wa wilaya kazi yao ni nini hasa? Kuna mambo ambayo hayahitaji kiongozi wa ngazi ya kitaifa wakati wao wapo,” anasema.

Profesa Kahangwa anasema likija suala la Rais Samia kutumia kalamu, ni pamoja na kuwauliza wakuu wa mikoa na wilaya walikuwa wapi wakati changamoto hizo zinajitokeza katika maeneo yao.

“Ni bora kalamu iongee ili wale wanaosubiri hadi Waziri Mkuu afike ndipo wachukue hatua wabadili mtazamo. Watendaji wanatakiwa kuwajibika. Sasa unakuaje mkuu wa mkoa au wilaya halafu huwasaidii wananchi?” anahoji Profesa Kahangwa.

Kuhusu malumbano ya wakuu wa wilaya na wakurugenzi, Profesa Kahangwa anasema bado imeendelea kuwa changamoto nchini, hivyo lazima ifike mahali majukumu ya watendaji hao yawekwe wazi ili kuepusha mwingiliano wa utendaji baina yao.

Naye mchambuzi mwingine, Said Miraji, anasema malumbano baina ya watendaji yanachangiwa na baadhi yao kutokuwepo na miongozo ya kazi iliyo wazi, na mwisho wa siku hawajui mamlaka yao yanaanzia na kuishia wapi.

Miraji anasema maeneo ambayo yamebainika watendaji wamefanya makosa, suluhisho si kuwasema au kuwahamisha na kuwashusha vyeo, bali kuwachukulia hatua za kisheria.

“Ningekuwa Waziri Mkuu nimekuta vitu kama vile, nisingeongea kitu, bali ingeongea kalamu huku nyuma. Rais Samia alishasema yeye hataongea sana bali itaongea kalamu, natamani kuona kalamu ikiongea.

“Kalamu inaongea namna gani? Simamisha mtu kupisha uchunguzi. Kama anaonekana ana hatia, peleka mahakamani ambayo itaamua kama ana kosa au hana. Kama ana kosa, ahukumiwe kwa mujibu wa sheria,” anaeleza Miraji.

Miraji anasema Serikali inatumia fedha nyingi kupeleka miradi ya maendeleo kwa wananchi, lakini baadhi ya watumishi wa umma wanawaangusha kwa kutotimiza wajibu wao, na mwisho wa siku lawama zinakwenda kwa viongozi wakuu.

“Ushauri wangu, Rais Samia atumie kalamu. Hata kama hakuwa na nia hiyo, yaani Waziri Mkuu anakutana na vitu unabaki unajiuliza hapa mkuu wa mkoa alikuwa wapi au mkuu wa wilaya? Au Waziri Mkuu ndiye anabaini mgogoro kati ya mkurugenzi na mkuu wa wilaya?” anahoji Miraji.

Kwa upande wake, mchambuzi wa siasa na maendeleo, Dk Hezron Makundi, anawatahadharisha baadhi ya watendaji wa Serikali waliopewa dhamana kwamba Serikali haijalala, hivyo wanapaswa kubadilika na kujirekebisha katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Wanapaswa kutambua mifumo ya Serikali bado inafanya kazi, na kila mtendaji katika nafasi yake anapaswa kuwajibika, kwa sababu asipofanya hivyo atawajibishwa.”

Kuhusu ziara ya Dk Mwigulu, Dk Makundi anasema: “Imekaa kiutendaji kwa maana ya ufuatiliaji, ufanisi na utendaji wa Serikali katika ngazi ya chini.”

Akihitimisha ziara ya siku tano mkoani Tanga, Dk Mwigulu alimwagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe, kurudi katika Halmashauri ya Muheza na kusafisha watumishi wote waliohusika na ubadhirifu wa fedha za jengo la ofisi.


Akiwa wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, mkazi mmoja (fundi) alimwambia Dk Mwigulu anaidai halmashauri ya wilaya hiyo Sh2.8 milioni tangu mwaka 2022 na hakuwahi kulipwa, jambo lililomshangaza Waziri Mkuu, aliyeamuru alipwe mara moja.

Katika mkutano wa hadhara wa kupokea kero, mfanyabiashara Josephine Shirima alimweleza Dk Mwigulu kuwa mali zake zilizokuwa dukani katika eneo la stendi ndogo zilichukuliwa na mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Wilaya ya Arusha, Dominic Mollel, na mbunge wa Moshi Vijijini, Morris Makoi.

Changamoto ya usimamizi hafifu wa miradi ya maendeleo ni suala lililojitokeza katika kila mkoa alioufanyia ziara Dk Mwigulu, akifananisha hali hiyo na “mchezo mchafu” wa kugawana fedha za umma zilizotengwa kwa miradi.

Aidha, akiwa wilayani Mbulu, Dk Mwigulu alipokea kero na hoja 305 kutoka kwa wananchi wa wilaya hiyo, huku akiahidi kuanzisha utaratibu madhubuti wa kuzishughulikia kwa wakati na kwa uwajibikaji unaopimika.

Migogoro, malumbano ya viongozi Serikalini

Katika kikao cha majumuisho cha Mkoa wa Manyara, Dk Mwigulu alikemea vitendo vya baadhi ya watendaji wa Serikali kulumbana wenyewe kwa wenyewe bila kutatua changamoto zilizopo katika maeneo yao.

“Nimepokea dondoo ya migogoro au mizozo, na mimi nawatonya msiponisikia, mtakutana na anayeongea kwa kalamu. Sasa nyinyi ndugu zangu, ninaposikia mkurugenzi na mkuu wa wilaya… haya mambo hayapendezi.

“Nimesikia hali ya namna hiyo Kiteto mnazo rasharasha hizo. Nitangulie kuwatonya, acheni hizo. Jikiteni kutatua masuala ya wananchi na kusukuma miradi ya maendeleo,” alisema Dk Mwigulu.

Kwa nyakati tofauti, Rais Samia amekuwa akiwaonya watendaji wa Serikali wanaolumbana wenyewe kwa wenyewe badala ya kutekeleza majukumu yao, akisema hatasita kuwachukulia hatua.

Kuhusu migogoro kati ya wakulima na wafugaji, Dk Mwigulu aliagiza mawaziri sita wa kisekta kukutana na kuainisha maeneo yote yenye changamoto hiyo, kisha kutafuta suluhisho la kudumu.