Aucho mambo safi Singida BS, rasmi arejea kazini

UONGOZI wa Singida Black Stars, umetangaza kumsamehe kiungo wa timu hiyo, Khalid Aucho na kumrejesha kazini kuanzia leo Machi 5, 2026 baada ya kufanyika kwa majadiliano na tathmini ya kina kufuatia tukio lililotokea wakati wa mazoezi ya timu.

Februari 27, 2026, uongozi wa Singida Black Stars ulitangaza kumsimamisha Aucho kwa miezi mitatu kwa tuhuma za utovu wa nidhamu na kuchelewa kazini. Mbali na Aucho, pia kipa Amas Obasogie, naye anatumikia adhabu ya miezi mitatu kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazohusiana na upangaji wa matokeo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na klabu hiyo, Aucho ameomba radhi kwa kosa lililotokea, jambo lililofanya uongozi kuwasilisha suala hilo mbele ya Kamati ya Nidhamu ili kulijadili na kulifanyia uamuzi.

Baada ya majadiliano, Kamati ya Nidhamu ilifikia uamuzi wa kumuondolea adhabu aliyokuwa amepewa awali na kuruhusu arejee kikosini kuendelea na majukumu yake kama kawaida.

Klabu hiyo imeeleza kuwa, uamuzi huo umezingatia hatua ya kujutia iliyooneshwa na mchezaji huyo pamoja na dhamira yake ya kurekebisha mwenendo wake ndani ya timu.

Aidha, Singida Black Stars imeendelea kusisitiza umuhimu wa nidhamu, uwajibikaji na weledi kwa wachezaji wote ili kuendelea kulinda heshima na mafanikio ya klabu hiyo. 

Jana Jumatano, Machi 4, 2026, Aucho aliomba radhi kwa uongozi wa klabu hiyo, benchi la ufundi, wachezaji wenzake pamoja na mashabiki kupitia ujumbe aliouandika katika ukurasa wake wa Instagram.

Katika ujumbe huo, Aucho aliandika kuchukua muda kutafakari kuhusu tukio lililosababisha sintofahamu ndani ya timu na kukiri kuwa lilileta hali ya kukatisha tamaa kwa baadhi ya watu waliokuwa wakimzunguka.

“Bila kujali hali iliyotokea, ninaomba radhi kwa dhati kwa uongozi, wachezaji wenzangu, mashabiki na kila mtu anayehusishwa na nembo ya klabu hii tunayoivaa kwa fahari. Ninasikitika kuona tukio moja la uamuzi usio sahihi likifunika dhamira yangu kwa timu,” aliandika Aucho.

Kiungo huyo raia wa Uganda pia alieleza kuwa anaelewa imani hujengwa kupitia mwenendo thabiti, taaluma na heshima, huku akisisitiza kuwa yupo tayari kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuisaidia timu kufikia malengo yake.

Aidha, Aucho aliwashukuru mashabiki wa Singida Black Stars kwa kuendelea kumuunga mkono na kumuonesha upendo licha ya changamoto zilizotokea, akiahidi kuendelea kuitumikia klabu kwa kujituma na kudumisha maadili ya umoja, nidhamu na taaluma ndani ya timu.