Bonasi yaibua ushindani BDL | Mwanaspoti

NAHODHA wa Stein Warriors, Mwalimu Herry amekiri kuna mabadiliko makubwa katika mchezo huo, yakichangiwa na udhamini pamoja na bonasi zinazotolewa kwa wachezaji.

Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam imekuwa ikipiga hatua kila msimu kutokana na kuwepo kwa wadhamini tofauti na miaka ya nyuma na hii imeongeza ushindani kwa wachezaji wakiwania pia kupata bonasi.

Herry aliliambia Mwanaspoti wadhamini wamekuwa wakitoa bonasi kwa  kila mchezaji kwa timu itakayoshinda hali iliyoongeza ushindani kwa timu zote.

“Bonasi hizo zinazotolewa kwa kila mchezaji, zimefanya kila mchezaji ahamasike kufanya mazoezi kwa lengo la kujiweka fiti kabla ya kuanza msimu wa ligi hiyo mwaka huu,” alisema Herry na kuongeza, kwa upande wa maandalizi ya wachezaji hao, wafanye mazoezi binafsi kwa bidii kabla ya kuanza msimu wa ligi mwaka huu. 

Kuhusu maandalizi yake ya ligi, alisema amekuwa akifanya mazoezi asubuhi na jioni na timu yake katika  uwanja wa kampuni ya mafuta (TPDC).

Akizungumzia mashindano ya Kanda ya Tano ya Afrika yaliyofanyika Kenya mwaka jana, alisema alijifunza mbinu za uchezaji kutoka kwa wachezaji katika timu tofauti.

“Tulikutana na wachezaji wenye viwango vikubwa, licha ya Stein Warriors kushiriki mashindano hayo kwa mara ya kwanza,

tulishika nafasi ya tano,” alisema Herry na kumtaja Ally Dibo wa Vijana ‘City Bulls’, ndiye mchezaji anayemvutia hapa nchini.

Pia alisema kuondoka kwa nyota wao, Sisco Ngaiza na Jonas Mushi waliojiunga na Dar City hakutaiathiri  timu yao na nafasi zao zitazibwa wakati wa usajili. 

Herry anayecheza nafasi ya namba 4, aliwahi kuzichezea Pazi, Dar City, UDSM Outsider miaka ya nyuma katika Ligi ya BDL na kuyataja mafanikio yake makubwa aliyapata mwaka 2025 alipojiunga na Kampuni ya Stein Warriors.