Jukwaa la Rising Woman kukutanisha  wadau zaidi ya 400 Dar kesho

Dar es Salaam. Wadau wakiwamo wanawake zaidi ya 400 kutoka sekta mbalimbali nchini, wanatarajiwa kushiriki katika Jukwaa la Sita la The Citizen Rising Woman Initiative (RWI) linalofanyika kesho Ijumaa Machi 6, 2026 katika Ukumbi wa Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam.

Jukwaa hili linafanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani inayoadhimishwa kila ifikapo Machi 8 na kaulimbiu yake inasema isemayo: “Give to Gain: Elevate Her Rise,” ikimaanisha:  “Toa ili Upate: Inua Safari ya Mafanikio ya Mwanamke.”

Jukwaa hili linaloandaliwa kila mwaka na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), huwakutanisha wanawake na wadau mbalimbali kwa lengo la kujadili uwezeshaji wa wanawake, kubadilishana uzoefu na kujenga mitandao ya kitaaluma.

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Machi 5, 2026  kuhusu na jukwaa hilo, Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Mpoki Thomson amesema kampuni hiyo inaendelea kudumisha urithi wake wa uandishi wa habari unaoibua ajenda muhimu na kusimulia hadithi zinazochochea mabadiliko chanya katika jamii.

Amesema mpango wa kila mwaka wa Rising Woman Initiative ni sehemu ya dhamira hiyo ya kuendeleza majadiliano na juhudi za kuwawezesha wanawake katika nyanja mbalimbali.

“Mpango wetu wa kila mwaka wa The Citizen Rising Woman Initiative ni ukumbusho wa kudumu wa dhamira hiyo,” amesema.

Thomson amesema mwaka huu wataanza na ‘Jukwaa la CRDB’ litakalozungumzia masuala yote ya ushirikiano na Benki ya CRDB.

Amesema kupitia ushirikiano huo, viongozi wa sekta binafsi pamoja na watunga sera wanakutana kujadili maendeleo ya wanawake na namna watakavyohakikisha juhudi za kuwawezesha zinakuwa endelevu.

Amesema jukwaa hilo la CRDB litawakutanisha  wanawake viongozi, wajasiriamali na wataalamu 300 na litaongozwa na kaulimbiu isemayo “Wanawake, Utajiri na Ustawi: Kuwezesha Upangaji Imara wa Fedha na Uwekezaji wenye Kujiamini.

Majadiliano katika jukwaa hilo yanatarajiwa kujikita katika uwezeshaji wa kifedha kwa wanawake pamoja na ustawi wa muda mrefu.

Baadhi ya wazungumzaji katika jukwaa hilo ni  Tully Ester Mwambapa, Mkurugenzi wa Masuala ya Kampuni wa CRDB Bank Plc na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation.

Wengine ni Fredrick Nshekanabo, Ofisa Mkuu wa Fedha wa CRDB Bank Plc; Profesa Neema Munisi Mori, Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB Bank Plc; pamoja na Godfrey Rutasingwa, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa CRDB Bank Plc.

Kwa upande wake, Mkuu wa Masoko, Mawasiliano ya Kampuni na Uendelevu wa MCL, Edson Sosten amesema Jukwaa la Rising Woman Initiative linaunga mkono malengo ya Dira ya Taifa 2050 inayolenga kujenga uchumi shindani na jumuishi.

Amesema ili kufanikisha dira hiyo, ni muhimu wanawake kuwezeshwa kikamilifu washiriki katika uongozi, ubunifu na maendeleo ya sekta mbalimbali za uchumi.

“Wanawake wanapoinuka, safari ya maendeleo ya Tanzania inakuwa imara na endelevu zaidi,” amesema.

Sosten amesema tangu kuanzishwa kwake 2021, zaidi ya wanawake viongozi 350 wameangaziwa kupitia jukwaa hilo huku taasisi 55 zikitambuliwa kwa mchango wao katika kuendeleza usawa wa kijinsia.

Amesema kaulimbiu ya mwaka huu inasisitiza kuwekeza katika uongozi wa wanawake si hisani, bali ni uwekezaji wa kimkakati kwa maendeleo ya Taifa na utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.

Katika hafla ya jioni, jopo la majadiliano litawakutanisha viongozi kutoka serikalini, sekta binafsi na mashirika ya maendeleo.

Miongoni mwa wazungumzaji watakaoshiriki ni  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo; Tully Ester Mwambapa wa CRDB Bank Plc; pamoja na Karen Giathi, Naibu Mwakilishi Kaimu wa UN Women Tanzania.

Majadiliano hayo yataongozwa na Khalila Sandrah Mbowe, Mtendaji Mkuu wa Unleashed Africa Ventures, huku yakiratibiwa na Blandina Kilama, Naibu Katibu Mtendaji wa Biashara na Ubunifu katika Tume ya Taifa ya Mipango.

Katika majadiliano hayo ya takribani dakika 50, washiriki watajadili ulinganifu wa sera na Dira ya Taifa 2050, uwekezaji wa taasisi katika kuwawezesha wanawake pamoja na mifumo ya uwajibikaji ili kuhakikisha ujumuishaji unaleta matokeo yanayopimika.

Aidha, masuala ya vitendo kama vile kuandaa kizazi kipya cha viongozi wanawake, upatikanaji wa mitaji, ujumuishaji wa masuala ya kijinsia katika mipango na bajeti pamoja na faida za kiuchumi zinazotokana na uwekezaji kwa wanawake yatajadiliwa.

Waandaaji wanasema majadiliano hayo yanalenga kuonyesha kuwa uwezeshaji wa wanawake si suala la kisera pekee bali ni mkakati muhimu wa kuleta mabadiliko ya kitaifa na kuimarisha ushiriki wa wanawake katika uchumi wa Tanzania.

Wadhamini na washirika wanaounga mkono mpango wa The Citizen Rising Woman Initiative ni  NMB Bank Plc, Gateway Terminal, WanaClick, AngloGold Ashanti, Serengeti, KPMG, Geita Gold Mine, CRDB Bank Plc, Women and Girls VS International, Africa Global Logistics, Softcare, Matrik, AVS, Z Studio na Smart.