Zaidi ya wakazi 13,200 wa Kata ya Tegeruka pamoja na vijiji jirani katika Wilaya ya Musoma Vijijini mkoani Mara wanatarajiwa kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za afya kwa ngazi ya kituo cha afya na kuendelea baada ya Serikali kutoa Sh250 milioni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Kituo cha Afya Kataryo.
Wakazi hao wanalazimika kutembea zaidi ya kilimomita 14 kwenda Hospitali ya Wilaya ya Butiama kufuata huduma za afya, ikiwepo ya kujifungua.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa kituo hicho kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi aliyefanya ziara katani hapo leo Machi 5, 2026, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Musoma Vijijini, Dk Joseph Fwoma amesema ujenzi huo ulioanza Septemba 2025, umefika asilimia 90.
Amesema mbali na Serikali kutoa fedha hizo, wakazi wa kata hiyo pia wamechangia zaidi ya Sh16 milioni kwa ajili ya ujenzi huo ambao unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.
Amesema ujenzi huu wa awamu ya kwanza unahusisha jengo la wagonjwa wa nje, maabara, mfumo wa maji taka na jengo la huduma ya mama na mtoto.
“Nafurahi kukujulisha kuwa mbali na kuchangia fedha kwa ajili ya ujenzi huu, wananchi wa hapa pia wamejenga nyumba ya mtumishi,” amesema.
Baadhi ya wakazi wa kata hiyo wameishukuru Serikali kwa mradi huo, huku wakiomba fedha kwa ajili ya ujenzi kwa awamu ya pili zitolewe mapema ili mradi uweze kukamilika na kutoa huduma ilivyokusudiwa.
Wamesema kukosekana kwa huduma za afya katika kata hiyo ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazowakabili, hali ambayo imekuwa ikisababaisha madhara kwao, vikiwepo vifo vitokanavyo na uzazi.
“Mjukuu wangu alifariki wakati anazaliwa, mama yake alipata uchungu usiku na tulikosa usafiri wa kumpeleka hospitalini, laiti kama tungekuwa na kituo hapa haya yasingetokea kwani tungepata huduma mapema,” amesema Veronica Mganga, mkazi wa Kijiji cha Kataryo.
Shida Daudi amesema hali inakuwa mbaya zaidi hasa nyakati za mvua kwani usafiri unakuwa wa shida na kulazimika kutumia gharama kubwa.
“Hebu fikiria mama anataka kujifungua usiku halafu barabara ndio kama hivyo mlivyoziona, kuna wakati hata bodaboda wanakataa kumbeba mgonjwa, tunaomba kituo chetu kikamilike haraka ili kituhudumie,” amesema.
Akizungumza baada ya kuzindua ujenzi huo, RC Mtambi amesema mradi huo unalenga kutimiza lengo la Serikali la kusogeza huduma bora za kijamii karibu na wananchi.
Ameagiza mamlaka zinazohusika kuhakikisha kituo hicho kinapata huduma za maji na umeme ndani ya siku saba, ili huduma zitakapoanza kutolewa kusiwepo na kikwazo cha aina yoyote.
Kuhusu barabara, Kanali Mtambi amesema suala la ubovu wa barabara kuelekea katika kituo hicho atalishughulikia haraka iwezekanavyo, atakwenda kukutana na Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) mkoa huo ili ukarabati wa barabara hiyo iliyoharibiwa na mvua uweze kuanza mara moja.
“Kuwepo kwa majengo ni kitu kimoja, huduma ya kuridhisha ni kitu kingine, nikuagize mkurugenzi hakikisha kila kitu kinakuwepo ili huduma ikianza wananchi wanufaike, sio huduma ziinaazna kutolewa nusu nusu mara hakuna umeme mara maji hayapo,” amesema
Ameongeza kuwa ofisi yake inaanza kufanya ufuatiliaji ili Serikali kuu iweze kutuma fedha ili kituo hicho kiweze kukamilika kwa haraka.