Magumu waliyopitia wananchi Ushetu kuvuka mto Igombe, Serikali…

Ushetu. Wananchi wa kata ya Ulowa na Ubangwe wameeleza changamoto waliyoipitia kuvuka mto Igombe ikiwamo ndugu zao kupoteza maisha sambamba na kuwasababishia umaskini.

Wamesema kukamilika kwa ujenzi wa daraja Ubangwe kumefufua matumaini ya ustawi wao, kwani sasa wana uhakika wa kuvuka kwenda upande wa pili bila baada ya  Serikali kuwapatia suluhu ya tatizo hilo.

Wameeleza hayo leo Alhamisi, Machi 5, 2026 wakati wa ziara ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi iliyoingia siku ya pili mkoani Shinyanga.

Pamoja na kufuatilia uhai wa chama, pia Kihongosi anakagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi.

Wananchi hao wamesema kabla ya ujenzi wa daraja hilo, maisha yao yalikuwa ya mashaka haya kipindi cha masika, kwani hawakuweza kuvuka kwenda ng’ambo ya pili.

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi akiangalia eneo la mto Igombe lilipojengwa daraja la Ubagwe



Muarabi Kasubi mkazi wa Ulowa amesema kwa miaka mingi walilazimika kuvuka kwa mitumbwi nyakati za mvua hali ilikuwa mbaya zaidi kwani usafiri huo haukuwa rafiki na mara kadhaa kumewasababishia ndugu zao vifo wakati wa kuvuka.

“Hata gharama za usafiri kuvuka kwa mtumbwi zilikuwa juu, ilikuwa Sh3000, lakini baada ya ujenzi wa daraja la Ubangwe nauli imeshuka tunatumia Sh1,000 kuvuka kwa Hiace (daladala), tunategemea nauli ishuke zaidi ya hapo, hii ni faraja kwetu,”amesema.

Mkazi mwingine, Sophia Kaswahili amesema ilikuwa changamoto kwa kina mama wajawazito kuvuka eneo hilo nyakati za masika wanapokwenda kupata huduma hospitali.

“Tumepitia mateso kuvuka mto Igombe kabla ya daraja hili, vifo vya mara kwa mara vilikuwa vikitokea, nyakati za mvua ilikuwa ni shida kubwa, wale wa huku walibaki huku, wa kule wa kule,” amesema.

Mkazi mwingine, Adam Maneo amesema kukwama kuvuka mto Igombe kuliwasababishia hasara ikiwamo wakulima kukwama kusafirisha mazao yao.

“Hatukuweza kuvuka kwenda kokote, nyakati za mvua mawasiliano yalikatika, wa Ulowa tulibaki Ulowa na Ubangwe walibaki huko, kukamilika kwa ujenzi wa daraja hili ni kama kumerejesha faraja mpya kwetu wananchi wa Ushetu,” amesema.

Katika ukaguzi wa ujenzi wa daraja hilo, Kihongosi amesema kukamilika kwake kutapunguza hasara kwa wakulima, wafugaji na wafanyabiashara.

Amesema adha waliyopitia wananchi wa Ushetu sasa imefikia tamati chini ya Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika eneo hilo ambalo msimu wa mvua ilikuwa hauwezi kwenda ng’ambo ya pili na mara kadhaa kusababisha vifo.


Amesema ujenzi wa daraja hilo linalounganisha mikoa ya Tabora, Geita na Shinyanga  umefanyika ndani ya miaka minne iliyopita kwanza ukigharimu Sh13.5 bilioni, sambamba na ujenzi wa madaraja mengine mawili ya Kasenga na Ng’hwande yaliyopo Ushetu.

Ameeleza kuridhishwa na maendeleo ya mradi huo ambao umekamilika na hivi sasa upo katika kipindi cha uangalizi ili mkandarasi atakapokabidhi kazi, mradi usiwe na changamoto.

Akizungumzia ubora wa daraja hilo, Kihongosi amesema thamani ya fedha kwenye mradi huo imeonekana na kuwasisitiza wananchi ni wajibu wao sasa kuulinda mradi huo.

“Mnafahamu mmetoka wapi na Chama cha Mapinduzi, mlikuwa hamna umeme, vituo vya afya na miundombinu hii, vyote vimeletwa na Serikali ya Rais Samia, hivyo ni wajibu wenu kuombea nchi iwe na amani, ikitoweka hautalima tumbaku unayolima, hautafuga wala kufanya chochote,” amesema Kihongosi.

Mapema asubuhi kabla ya kukagua mradi wa ujenzi wa daraja hilo, Kihongosi alikagua mradi wa umeme wa Rea kwenye kata ya Kisuke Jimbo la Ushetu.

Katika mradi huo unaoingiza megawati tano kwenye gridi ya Taifa, Kihongosi amesema mradi huo ni mzuri kuhakikisha wananchi wanapata umeme.

“Wakati nakuja hapa (Ushetu) 2021 2022, Ushetu haikuwa hivi, imekuwa na maendeleo kama ambavyo Ilani ya Chama cha Mapinduzi inaelekeza kupeleka maendeleo nchi nzima.

“Kinachofanyika hapa ndicho kinachofanyika kwingine, nchi yetu ni kubwa hivyo tumpongeze Rais Samia kwa kuhakikisha maendeleo yanafika kote,” amesema Kihongosi.

Pia, Kihongosi amempongeza Mbunge wa Ushetu, Emmanuel Charahani kwa uchapakazi wake na kupongeza umoja na mshikamano walionao wabunge wa Shinyanga.

“Chama kinapokuta mambo ni mazuri hakina ugomvi na mtu, tukikuta mambo ni mabaya tutakemea,” amesema Kihongosi.

Awali, Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba alisema katika Halmashauri ya Ushetu tayari makandarasi wapo maeneo ya miradi kwenye vijiji 136.

“Bado vijiji 100 na ushee, hivi umeme utawaka kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa 2029,” amesema Makamba akibainisha mradi huo uliogharimu Sh11 bilioni, umefanya CSR kwa kuwajengea wananchi zahanati.

Mganga mkuu wa wilaya (DMO), Baraka Msumi akijibu kero ya upatikanaji dawa



Kwa upande wake, Charahani ameshukuru kwa zahanati hiyo na kuomba ijengwe na chumba cha kujifungulia, jambo ambalo Salome alisema tayari zahanati imekamilika, ujenzi wa chumba cha kujifungulia upo ndani ya halmashauri yao, watalifanyia kazi ikiwamo kuweka vifaa tiba ili wananchi waanze kutibiwa.