BAADA ya Dabi ya Kariakoo iliyomalizika kwa matokeo ya 0-0, Yanga ikaanza maandalizi ya kwenda Singida kuwafuata wenyeji wao Singida Black Stars, huku Simba wakipata mteremko fulani wakipumzika huku wakitoa ratiba ya mechi zao tano watakazocheza mwezi huu Machi.
Sasa basi kitendo hicho kimemwibua bosi mmoja wa Yanga.
Aliyeibua mjadala huo ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Alexander Ngai akionyesha kushangazwa na ratiba ya mechi tano zinazofuata za Simba akilinganisha na ratiba ya mechi za Yanga.
Ngai aliweka ratiba ya mechi tano za Simba ambazo itacheza Machi 7 dhidi ya B19 katika Kombe la Shirikisho la CRDB, kisha ikifuatiwa na mechi nne za Ligi Kuu Bara ikianza na Singida black Stars ugenini, Machi 11.
Baada ya mechi hiyo, Simba itasafiri kuifuata TRA United, Machi 14, baadaye Pamba Jiji (Machi 19), kisha itarudi nyumbani kurudiana na TRA United (machi 22).
Ngai aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram: “Tumemaliza dabi siku moja, sijui nini kipo hapa, angalia ratiba ya hawa jamaa (Simba) na yetu.”
Kiongozi huyo akamalizia kwa kusema: “Tuna safari ndefu sana.”
Baada ya ratiba hiyo ya Simba, Ngai ameweka ratiba ya Yanga ambayo jana Machi 5 ilikuwa ugenini kucheza mechi ya ligi dhidi ya Singida Black Stars. Baada ya hapo, itarudi nyumbani kupambana na Polisi Tanzania, Machi 8 ikiwa ni mechi ya Kombe la Shirikisho la CRDB.
Ikimaliza mechi hizo Yanga itarudi kwenye Ligi ikiifuata Tanzania Prisons (Machi 12), kisha Azam (Machi 15) na TRA United (18), hizi zote itakuwa ugenini.
Baada ya posti hiyo, alipotafutwa na Mwanaspoti, Ngai alisema bado anashangaa kwa nini Simba haijapangiwa mechi baada ya kucheza mchezo wa dabi.
“Hamjaelewa? Ni hivi, tumecheza na hawa jamaa Zanzibar Machi Mosi, tukarudi wote siku moja mjini lakini sisi tuna mechi Singida wenzetu watacheza Machi 7, hiyo ni sawa?” alihoji Ngai.
“Huyu Singida alicheza na Coastal Union juzi tu (Machi 2), lakini tumepangiwa kucheza naye, kwa nini hawa wenzetu wasicheze?
“Ungeweza kuelewa kama sisi tungekuwa na kiporo lakini wote tuna michezo sawa, lakini bado wamepewa mapumziko tena karibu siku tano wakati sisi hatuna mapumziko, ndio waendelee kushangilia sare au kuna sababu nyingine?.”
Akizungumzia hilo, Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Karim Boimanda alisema taratibu za kikanuni ndizo zimesababisha mchezo unaofuata wa Ligi wa Simba uwe Machi 11.
“Ratiba ya mechi za viporo inapopangwa huwa inaangaliwa pia na hizo timu nyingine zina ratiba gani. Sasa ni sahihi Simba ilicheza Machi Mosi na Yanga na kikanuni wangeweza kucheza Machi 4 au 5 kama ambavyo imekuwa kwa Yanga na Azam kwa vile muda wa saa 72 za kutoka mechi moja au nyingine unakuwa umetimia.
“Lakini Coastal Union wao wamecheza na Singida Black Stars, Machi 2 hivyo ukipanga wacheze na Simba, Machi 4 maana yake watacheza chini ya saa 72 jambo ambalo kikanuni siyo sawa. Na ukisema mechi uipange Machi 5, Simba siku ya Machi 7 wana mchezo wa Kombe la Shirikisho la CRDB, hivyo pia watakuwa hawajatimiza saa 72 kama kanuni inavyoelekeza,” alifafanua Boimanda.