UONGOZI wa Namungo FC, uko katika mazungumzo ya kumwongezea mkataba mpya mshambuliaji wa kikosi hicho, Mkongomani, Fabrice Ngoy, baada ya mabosi wa timu hiyo kuridhishwa na kiwango chake.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa Namungo, Ally Suleiman alisema mazungumzo na nyota huyo ili kuongeza mkataba mpya yameanza na yamefikia katika hatua nzuri, baada ya kuridhishwa na kiwango chake tangu amejiunga na kikosi hicho.
“Tumeanza taratibu mapema ili kuepusha migongano inayoweza kutokea mwishoni mwa msimu baada ya mkataba wake kuisha, ni mchezaji mzuri ambaye tunaamini kwa kipaji na umri wake atatusaidia sana katika michuano mbalimbali,” alisema Suleiman.
Kwa upande wa mshambuliaji huyo ambaye kwa sasa ndiye anayeongoza chati ya ufungaji katika Ligi Kuu Bara msimu huu kwa kufunga mabao mengi akiwa nayo manane, alisema suala la hatima yake ni mapema kulizungumzia, japo malengo yake ni kuendelea kufanya vizuri.
Nyota huyo ameaminiwa na kocha, Juma Mgunda, licha ya uwepo wa washambuliaji wengine wakiongozwa na mkongomani mwenzake, Heritier Makambo aliyetoka TRA United zamani Tabora United na Abdulaziz Shahame ‘Haaland’, aliyetokea kikosi cha TMA FC.
Ngoy alijiunga na Namungo msimu wa 2023-2024, akitoka Kitayosce iliyobadilishwa jina na kuitwa Tabora United na sasa TRA United, baada ya kuifungia mabao 15 ikiwa Ligi ya Championship, nyuma ya kinara, Edward Songo wa JKT Tanzania aliyefunga 18.
Mshambuliaji huyo alitua hapa nchini kwa mara ya kwanza msimu wa 2022-2023, akitokea Real Nakonde FC ya Zambia na msimu wa 2023-2024, alifunga bao moja tu, huku 2024-2025, akifunga mawili na sasa msimu wa 2025-2026, tayari amefunga manane.