Mtandao wa utapeli wanaswa na laini 198, kadi 148 za benki

Morogoro. Jeshi la Polisi mkoani Morogoro limefanikiwa kuvunja mtandao wa utapeli wa simu, maarufu halohalo, baada ya kuwakamata watuhumiwa 10.

Katika operesheni hiyo, polisi pia wamekamata laini 198 za simu na kadi 148 za benki kutoka taasisi mbalimbali za kifedha.

Watuhumiwa hao walikamatwa Machi 3, 2026 katika operesheni maalumu iliyofanyika Kitongoji cha Magoha, Kata ya Lumemo, Mji wa Ifakara, wilayani Kilombero.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 5, 2026 mjini Morogoro, Kamanda wa Polisi Mkoa, Alex Mkama, amesema kuwa katika operesheni hiyo watuhumiwa saba walikamatwa wakiwa na laini 110 za simu kutoka mitandao mbalimbali.

Laini hizo zilisajiliwa kwa majina ya watu wengine na kutumika kupiga simu kwa lengo la kuwatapeli wananchi.

Kamanda Mkama amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Cassian Liganga (28), Juma Fay (25), Halid Mwanzage (24), Amord Udindo (21), Mjelwa Mjelwa (22), Moses Litaka (21) na Michael Mboga (22), wote wakazi wa Lumemo wilayani Kilombero.

“Katika msako wa askari wetu, pia wamemkamata Amani Mwakipesile (26), wakala wa kusajili laini za simu na mkazi wa Mnalani wilayani Kilombero, akiwa na laini 88 za simu zilizosajiliwa kwa majina ya watu mbalimbali, ambazo huwauzia wahalifu wanaofanya utapeli,” amesema Kamanda Mkama.

Kamanda Mkama amewataja watuhumiwa wengine waliokamatwa kuwa ni Patrick Godfrey (22), mkazi wa Mlabani, na Fredrick Ngwasi, maarufu kwa jina la Chepe (32), waliokuwa wakitafutwa kwa tuhuma za kuhusika na matukio ya utapeli kwa njia ya simu kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa Mkama, watuhumiwa hao wanadaiwa kufanikiwa kuwaibia baadhi ya waathirika zaidi ya Sh12 milioni katika eneo la Mbagala, mkoani Dar es Salaam kwa kutumia mbinu za ulaghai kupitia simu.

Katika hatua nyingine, polisi wamemkamata Nyamhanga Marwa (28), mkazi wa Ruaha wilayani Kilosa, akiwa na kadi 148 za benki zenye majina ya watu tofauti.

Kadi hizo zinadaiwa kutumika kuingilia akaunti za watu na kuchukua fedha kinyume cha sheria.

Kamanda Mkama amesema upelelezi unaendelea ili kuwabaini washirika wengine wa mtandao huo wa utapeli na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

Amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa waathirika wa matukio hayo ni wafanyabiashara wa mazao ya chakula kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Dodoma, Mwanza, Tanga na Zanzibar.

Kutokana na hali hiyo, amewataka wananchi kuwa makini wanapofanya miamala ya fedha kwa njia ya simu na kuepuka kutuma fedha kwa watu wasiowafahamu.

“Utapeli wa mitandaoni hauna mipaka na unaweza kufanywa na mtu akiwa sehemu yoyote duniani, hivyo wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari ili kuepuka kuingia katika mtego wa matapeli,” amesema Kamanda Mkama.