Dar es Salaam. Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman amewahimiza Watanzania na waumini wa Kiislamu kuzidisha maombi na ibada ndani ya mwezi wa Ramadhani ili Taifa lirudi katika hali ya haki na utengamano, baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu.
Amesema jambo kubwa lililopo ni kila mmoja kuiombea nchi irudi katika mstari wa haki na utengamano na maridhiano ya kisiasa, baada ya kumalizika mchakato huo uliofanyika Oktoba 29, 2025.
“Hatua hii itatuwezesha kulikwamua Taifa lirudi katika njia ya umoja na mshikamano na hatimaye kuishi kwa amani na utulivu,” amesema Othman.
Othman ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar mstaafu, ameeleza hayo leo Alhamisi Machi 5, 2026 wakati akiwasalimia wananchi wa mikoa ya kichama ya Wete, Micheweni na Kaskazini Pemba katika mwendelezo wa ziara yake kisiwani Pemba.
Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud akizungumza na wananchi wa Wete alipokwenda kuwasalimia na kuwafariji katika utaratibu wake wa kuwatembelea.
Kwa mujibu wa Othman, kuitengeneza nchi ni jambo la heri, hivyo kila mwananchi ana jukumu la kuzidisha maombi yatakayoleta utengamano wa kijamii.
Mwenyekiti huyo yupo katika ziara ya kuwafariji, kwa hali na mali, wananchi wanyonge na wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo za maradhi.
Ziara hiyo inakwenda sambamba na kuwahamasisha watu wazidishe dua, kuliombea Taifa ili kurudisha hali ya maelewano miongoni mwao.
“Kama mnavyofahamu katika chama chetu tuna utaratibu aliotuachia mzee wetu, Maalim Seif Sharif Hamad (marehemu) na sisi tumeona ni vyema tuundeleze,” amesema.
Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud akizungumza na wananchi wa Wete alipokwenda kuwasalimia na kuwafariji katika utaratibu wake wa kuwatembelea.
Mwenyekiti wa Mkoa wa Kichama wa Wete Pemba, Juma Khamis Ali, amemshukuru Othman kwa namna anavyofanya ziara ya kuwatembelea na kuwafariji wananchi mbalimbali.
“Hi ni kazi kubwa, tunakupongeza sana na tunamuomba Mungu akupe nguvu, uhai na maisha marefu, ili uendelee kubeba matumaini ya Wazanzibari na Watanzania wote,” amesema Ali.